Prime
Watatu waachiwa huru usafirishaji gramu 997.91 za heroini

Muktasari:
- Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama hiyo imesema upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha kesi hiyo pasipo kuacha shaka kwani mnyororo wa utunzaji wa kielelezo haukuzingatiwa.
Arusha. Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imewaachia huru washtakiwa watatu walioshtakiwa kwa kosa la kusafirisha gramu 997.91 za dawa za kulevya aina ya heroini.
Hukumu iliyowaachia huru washtakiwa hao imetolewa Mei 23, 2025 na Jaji Sedekia Kisanya aliyesema upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha shitaka hilo pasipo kuacha shaka.
Walioachiwa huru ni Mohamed Ramadhani, Khalid Ally, Said Mohamed Ngokonda na Said Adinan( ambaye aliachiwa tangu upande wa mashitaka ulivyomaliza kesi yake na kukutwa hana kesi ya kujibu) ambao wote walitetewa na mawakili, Alfredy Haonga, Benjamin Magen, Subira Mhando na Nehemia Nkoko.
Jamhuri ilidai awali kuwa Desemba 24, 2019, katika Ofisi za Azam Marine zilizopo Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam, washtakiwa hao walikutwa wakisafirisha dawa hizo za kulevya.
Tangu mwanzo wa kesi washtakiwa hao walikana kuhusika na kosa hilo na upande wa mashitaka uliowakilishwa na mawakili wa Serikali waandamizi wawili, uliita mashahidi 15 na kuwasilisha vielelezo 16 kuthibitisha shitaka hilo.
Shahidi wa pili, Ofisa usalama wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Augustine Marco, alieleza akiwa zamu ya kawaida katika sehemu ya kukagua mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, alikuwa na jukumu la kusimamia uhakiki wa mali za abiria zinazoelekea Zanzibar.
Alieleza katika ukaguzi wake aliona mfuko wa salfeti wa mchele ukipitishwa kwenye skana, uliokuwa ndani ya begi ambalo lilikuwa mkononi mwa mbeba mizigo kutoka Azam Marine, Kasema Magota ambaye alikuwa shahidi wa tatu katika kesi hiyo.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, baada ya kuona kwenye skrini na kuhisi kuna kitu kibaya aliamua kuchunguza kilichomo ndani yake.
Alieleza kuwa shahidi wa tatu alijibu kuwa mfuko huo ulikuwa na mchele na alipewa katika ofisi ya Azam Marine kwa maelekezo ya kuupakia kwenye meli iliyokuwa inakwenda Zanzibar.
Kutokana na kutokuridhika na maelezo hayo, Augustine aliagiza mfuko huo ufunguliwe ambapo ndani yake walikuta mfuko wa nailoni ulioonekana ukiwa na poda iliyokuwa ikitoa harufu kali.
Alieleza kumjulisha msimamizi wake (Mariam Mkumba) ambaye naye aliwasilisha suala hilo kwa Ofisa Polisi anayehusika na Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Koplo Anna.
Baadaye shahidi wa tano, Sajenti Pashua, alifika kwenye eneo la tukio na kuchukua mzigo huo ambao shahidi wa tatu pamoja na wa nne, Ismail Issa ambaye pia ni mfanyakazi wa Azam Marine ambaye awali alipokea mfuko huo wa mchele kutoka kwa mtumaji.
Uchukuaji wa mzigo huo ulirekodiwa katika cheti cha ukamataji ambacho kilisainiwa na mashahidi hao (wa tatu na nne) ambao walikuwa kama washukiwa kwa wakati huo.
Shahidi wa tano, alifunga kifurushi chenye unga huo ulioshukiwa kuwa dawa za kulevya huku Augustine akiwa shahidi wa kujitegemea na mfuko wa mchele huo lilifungwa kwa kamba ili iwe rahisi kubeba na kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Bandari.
Baada ya kuwasili, mfuko wa mchele, kifurushi kilichofungwa, na simu mbili za mkononi zilikabidhiwa kwa shahidi wa tisa, Khamis Mkeng'ndo kama mlinzi wa vielelezo hivyo.
Ilielezwa mahakamani Khamis alirekodi vitu hivyo na kuvihifadhi kwenye chumba cha vielelezo na Desemba 27,2019 alikabidhi bahasha kwa shahidi wa kwanza, Ally Kashmidu ili kuwasilishwa kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia wa Serikali (GCLA).
Kielelezo hicho kilipokelewa na shahidi wa 11 ambaye ni mkemia wa serikali kutoka GCLA, Kaijunga Triphon, aliyechukua sampuli zake na kupima na vipimo kuonyesha zilikuwa ni dawa za kulevya aina ya heroini.
Kasema na Ismail walikamatwa kuanzia siku ya tukio ambapo shahidi wa tatu alidai mzigo huo ulipelekwa na mshtakiwa wa kwanza (Mohamed) ambaye ni mteja wao wa kawaida huku shahidi wa nne akidai mzigo huo ulipaswa kumfikia mshtakiwa wa tatu (Said) aliyekuwa Zanzibar.
Ismail alieleza kuwa, mshtakiwa wa kwanza ndiye aliyetoa majina na namba za simu za mpokeaji, ambazo ziliandikwa kwenye gunia na kurekodiwa kwenye risiti iliyotolewa baada ya malipo ya gharama za usafiri zinazohitajika.
Shahidi wa 14, Inspekta Masawika baada ya kuelezwa taarifa hizo alishirikiana na wenzao wa Zanzibar kwa lengo la kumtafuta na kumkamata mshtakiwa wa tatu, jukumu walilopewa SSP Omar, Juma Omar Khamis (shahidi wa sita), na Abdi Ali Mohamed (shahidi wa nane).
Maofisa hao walienda katika ofisi za Azam Marine zilizopo Malindi, Zanzibar na kukutana na shahidi wa nane, Maulid Sharia Ame ambaye alifuata maelekezo ya maofisa hao wa polisi na kuwasilisha na mshtakiwa wa tatu kumjulisha akafuate mzigo wake ambapo alipofika alikamatwa.
Kwa mujibu wa shahidi wa sita, mshtakiwa wa tatu alikana kumiliki mfuko huo na kueleza alitumwa na mshtakiwa wa pili ambaye kwa wakati huo alikuwa akisubiri nje ya ofisi hizo akiwa kwenye gari, ambaye pia alikamatwa na wakati wa mahojiano alidaiwa kukiri mzigo ni wake.
Shahidi wa 14,alieleza kuwa mshtakiwa wa kwanza alimjulisha kuwa alipokea mfuko huo kutoka kwa mshtakiwa wa nne ambaye alikuwa akiishi Kivule (Dar es Salaam) , ila alikamatwa Desemba 29,2019 katika eneo la Mam Lodge jijini Tanga alipokutwa na mkewe na watoto wake.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa na familia yake walikuwa wakipanga kutorokea Mombasa, Kenya ambapo alikamatwa na fedha pesa za Kenya milioni tano, Dola za Marekani 5,000, simu nne na hati saba za kusafiria.
Baada ya kumalizika kwa kesi ya upande wa mashitaka, Mahakama iliona kuwa upande wa mashitaka ulifanikiwa kutengeneza kesi ya kujibu dhidi ya washtakiwa wa tatu na kumuachia huru mshtakiwa wa nne.
Utetezi wa washitakiwa
Mohamed, alieleza Desemba 24, 2019 alikuwa Kijiji cha Kisiju, Pwani alikoenda kumtembelea mama yake akikana hajawahi kufika ofisi za Azam Marine ,wala hamfahamu mshtakiwa wa tatu na hahusiki na dawa hizo za kulevya.
Khalid ambaye ni mfanyabiashara anayeuza nafaka nyumbani kwake, Gulioni Zanzibar alidai kukamatwa Desemba 25,2019 na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Jang'ombe Mjini Magharibi, alipokutana na mshtakiwa wa tatu.
Alidai alilazimishwa kukiri kuwa ni mshirika wa mshtakiwa wa tatu na alipopelekwa Dar es Salaam alikana kielelezo hicho ambacho kilikuwa kimeandikwa Khalid Ali, na kudai jina lake ni Khalid Ali Mohamed na kuwa kuna watu wengi wenye jina la Khalid Ali.
Akijitetea mahakamani hapo mshtakiwa wa tatu, alidai yeye ni mkazi wa Kwerekwe, Unguja, Zanzibar, akijishughulisha na biashara ya kuuza televisheni na simu za mkononi za mitumba.
Alidai baada ya kukamatwa na kufikishwa katika Kituo cha Polisi cha Skuli Jang'ombe, Zanzibar, alielezwa kuwa anachunguzwa kuhusiana na luninga zilizoibiwa na baadaye kuhamishiwa Dar es Salaam alikoelezwa anashikiliwa kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kuelvya.
Kuhusu kielelezo cha tatu alidai jina lililoandikwa kwenye kielelezo hicho ni Said Mohamed, si lake, kwani jina lake kamili ni Said Mohamed Ngakonda.
Uamuzi Jaji
Jaji Kisanya baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili alieleza kuwa kwa kuzingatia kifungu cha 3(2)(a) cha Sheria ya Ushahidi, jukumu la kuthibitisha kesi ni la upande wa mashitaka ambao wana wajibu wa kuthibitisha vipengele vyote muhimu vya kosa bila kuacha shaka yoyote.
Amesema suala kuu la kuamuliwa ni iwapo washtakiwa walihusika na usafirishaji wa dawa hizo za kulevya na kuwa Mahakama hiyo inaona ni muhimu kuzingatia masuala madogo matatu.
Jaji Kisanya ametaja masuala hayo ni iwapo hizo ni dawa za kulevya, iwapo watuhumiwa au yeyote kati yao ameunganishwa kwa njia yoyote ile na umiliki au usafirishaji wa mfuko huo uliokutwa na dawa hizo.
Nyingine ni kuzingatia iwapo viwango vya kisheria, ikiwa ni pamoja na utunzaji wa vielelezo tangu vimekamatwa hadi kufikishwa mahakamani na kuwa baada ya kupitia kwa makini ushahidi wote uliotolewa, Mahakama hiyo inaona kuwa upande wa mashitaka haujafanikiwa kuthibitisha ushahidi kamili.
Amesema katika ukamataji huo pia hakukuwa na shahidi wa kujitegemea kama inavyotakiwa chini ya Kifungu cha 38(3) cha CPA na Kifungu cha 48(2)(d) (i) cha DCEA.
Jaji Kisanya amesema kutokana na kutofautiana na mapungufu yaliyobainika, Mahakama haijaridhika kwamba upande wa mashitaka umetekeleza wajibu wake wa kuthibitisha mlolongo wa ulinzi wa kielelezo hicho cha pili, hivyo kesi hiyo haijathibitishwa na kuamuru waachiwe huru.