Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Anayedaiwa kinara biashara ya mirungi anaswa Same

Uteketezaji wa mirungi kwenye baadhi ya mashamba wakati wa operesheni iliyofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wilayani Same.



Muktasari:

  • Anadaiwa  kwa zaidi ya miaka 30 amekuwa akiongoza mitandao ya biashara haramu ya mirungi. Nyumba yake yakutwa imezungukwa na mashamba ya mirungi.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imemkamata Interindwa Kirumbi (67), maarufu mama Dangote anayedaiwa kuwa kinara wa biashara ya mirungi.

Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kumetokea wakati wa operesheni maalumu iliyofanyika kwa siku saba Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro ambayo iliwezesha pia kuteketezwa ekari 285.5 za mashamba ya mirungi.

Kwa mujibu wa DCEA, Interindwa ni kinara wa biashara haramu ya mirungi nchini aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu.

Kamishna Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo akiwa katika operesheni ya uteketezaji wa mashamba ya mirungi iliyofanyika wilayani Same, Kilimanjaro.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Machi 26, 2025, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amedai kuwa mtuhumiwa huyo ni mzalishaji na msambazaji mkubwa wa dawa za kulevya aina ya mirungi nchini.

Amesema mama huyo ambaye mara kadhaa amekuwa akivikwepa vyombo vya ulinzi na usalama amekamatwa nyumbani kwake katika kijiji cha Likweni.

“Kwa zaidi ya miaka 30, amekuwa akiendesha mitandao ya biashara haramu ya mirungi na kusimamia masoko ya dawa hizo za kulevya katika maeneo mbalimbali nchini, licha ya kujua kuwa ni kinyume cha sheria.

“Tulifanikiwa kumfuatilia na kumvamia nyumbani kwake, ambako amezungukwa na mashamba ya mirungi. Huyu mama tayari tumeshakabidhi kwenye vyombo vya dola kwa hatua zaidi,” amedai Kamishna Lyimo.


Mirungi bado ni tatizo Same

Kamishna Lyimo amesema mwaka juzi mamlaka hiyo ilifanya operesheni wilayani humo na kutoa elimu kwa wananchi ili waachane na kilimo cha mirungi na badala yake wajikite katika kilimo cha mazao mbadala pamoja na ufugaji.

Uteketezaji wa mirungi kwenye baadhi ya mashamba wakati wa operesheni iliyofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wilayani Same.

Hata hivyo, elimu hiyo haikufua dafu kwa baadhi ya watu ambao wameendelea kujihusisha na kilimo hicho cha dawa za kulevya na kuendelea kuathiri Watanzania.

“Mwaka juzi tuliteketeza jumla ya ekari 535 za mashamba ya mirungi. Kwa kushirikiana na uongozi wa wilaya, tulitoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya dawa za kulevya, ikiwemo mirungi.

“Lengo lilikuwa kuwawezesha wakazi wa eneo hili kujikita katika kilimo cha mazao mbadala na ufugaji kama njia ya kujiongezea kipato” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Pamoja na elimu hiyo amesema uongozi wa wilaya ya Same na Wizara ya Kilimo na Mifugo  waliwapelekea wananchi wa maeneo hayo miradi ya ufugaji wa nguruwe na kugawa miche ya kahawa, iliki na mazao mengine.

“Kutokana na juhudi hizo, wananchi wengi wameachana na kilimo cha mirungi na kuanza kulima mazao mbadala, japo wapo wananchi wachache waliokaidi na kuendelea na kilimo na biashara ya mirungi.”

Muonekano wa baadhi ya maeneo yanayozalisha mirungi katika wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro

Kutokana na hilo Lyimo amesema mamlaka itaendelea kufanya operesheni kuhakikisha wananchi wote wanaojihusisha na biashara ya mirungi wanakamatwa na hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yao.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunatokomeza biashara na matumizi ya mirungi hapa nchini hasa ikizingatiwa kuwa, eneo hili la Same ni kitovu cha uzalishaji mirungi nchini hali inayohatarisha ustawi wa Taifa letu ndio maana tunafanya operesheni hizi endelevu nchi nzima kuhakikisha tunadhibiti uzalishaji, usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya za mashambani na viwandani ili zisiendelee kuathiri wananchi,” amesema Lyimo.

Akizungumzia hilo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ekondi, Agnes Mshana amekiri kutambua uwepo wa watu wanaojihusisha na kilimo cha mirungi na wao kama Serikali wameendelea kutoa elimu juu ya madhara ya mirungi ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kupata mazao mbadala ili kuepukana na kilimo hicho.