Prime
Sababu polisi wastaafu kupewa tena ajira mpya

Msemaji Mkuu wa Serikali
Mapema, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema hana taarifa rasmi ya mikataba ya muda, lakini akajikita kwenye uwezeshaji wa Jeshi la Polisi kibajeti na kivifaa.
Alisema ndani ya miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita, imekuwa ikiongeza bajeti ya jeshi hilo.
“Mwaka 2020/21 bajeti ya Polisi ilikuwa Sh565 bilioni na mwaka 2023/24 bajeti yake imefikia Sh798 bilioni na hiyo inamaanisha Serikali inatoa kipaumbele katika uboreshaji wa Jeshi la Polisi si tu kwa watumishi wake, bali pia vifaa vya kazi, ikiwemo ofisi,” alisema.
Matinyi aliongeza ndani ya kipindi hicho, magari ya Polisi 290 yalinunuliwa na pikipiki 105 na jumla ya vituo vya Polisi 18 na ofisi 10 za makamanda wa mikoa vimejengwa.
“Hii ni mifano tu ya sehemu inayoletwa na ongezeko la bajeti na Serikali imenuia kuliimarisha Jeshi la Polisi kwa ajili ya usalama wa raia na mali zao,” alisema Matinyi.
Walichokisema askari polisi
Kulingana na taarifa zilizolifikia Mwananchi kutoka mikoa mbalimbali nchini, askari wa vyeo vya chini na vya kati waliostaafu mwaka jana na mwaka huu wameitwa kurejea kazini kwa mkataba maalumu wa miaka miwili ambayo uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu utafanyika.
“Ni kweli kuna hilo jambo, ila si la lazima kuomba. Yaani waliostaafu na kama unajiona una nguvu basi unaruhusiwa kuingia mkataba, ni wa miaka miwili tu. Kwa kweli sijui sababu, ila nahisi ni kuongeza nguvu kazi,” alisema mmoja wa askari mkoani Mbeya.
“Kuna mwenzangu alistaafu Julai mwaka jana naye amechangamkia hiyo fursa kwa sababu unajua sisi wa vyeo vya chini kama Konstebo, Sargent (Sajini) na Major (Stesheni Sajini) tunastaafu tukiwa na nguvu zetu kabisa,” alidokeza.
Kulingana na kanuni za Jeshi la Polisi, askari mwenye cheo cha kuanzia Konstebo hadi Sajini hutakiwa kustaafu kwa lazima anapotimiza umri wa miaka 45, wakati Inspekta ni miaka 55 na Mrakibu Msaidizi (ASP) hadi Kamishina ni miaka 60.
Ofisa wa Polisi mwenye cheo cha ASP mkoani Ruvuma alisema utaratibu huo ni mzuri, hasa ikizingatiwa kuwa kuanzia mwaka 2015 alipoingia Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli, ajira zilikuwa za nadra hadi alipoingia Rais Samia.
“Ukizingatia ajira zilisimama kwa muda mrefu hadi alipokuja mama yetu mpendwa (Rais) na hapo hapo askari wanastaafu na wengine hata kufa, ni lazima nguvu kazi iliyopo isingetosha kusimamia uchaguzi kwa ufanisi.
“Pamoja na ofa, sio kila askari aliyestaafu atachukuliwa. Hapana. Kuna vigezo, kimojawapo ni lazima ukubali kwa hiari, uwe na afya njema na uwe na rekodi nzuri ya utendaji na tabia. Kuna kamati kabisa itawachuja hawa watu,” alieleza.
“Hili sio la askari wa chini tu, hili ni la wote, ndiyo maana unaona kuna wakubwa walishastaafu tangu mwaka jana unawaona wako kazini kama hapo Dar es Salaam na CCP (Chuo cha Polisi Moshi). Ni jambo jema sana Serikali imefanya,” alisisitiza.
Ofisa huyo alisema ipo haja ya Serikali kupitia utaratibu wa askari wa vyeo vya chini kustaafu mapema wakiwa na nguvu na wale wa vyeo vya juu kwenda hadi miaka 60, wakati kazi za shuruba zinafanywa na hao wa vyeo vya chini.
“Mimi nafikiri hawa wa vyeo vya chini sheria iwaruhusu kustaafu kwa hiyari akifika 55 na kama ana nguvu aende hadi 60, lakini tunaruhusu vijana wenye nguvu, wenye ujuzi na uzoefu wanaingia mitaani si sawa,” alieleza ofisa huyo.
Askari wa cheo cha Koplo Jijini Arusha ameipongeza Serikali kwa uamuzi wa kuwapa mikataba wenzao waliostaafu na kupendekeza utaratibu huo usisubiri tu wakati wa uchaguzi, bali ufanyike miaka yote, hasa kwa askari wale wa vyeo vya chini.
Kwa upande wake, askari mwingine aliyestaafu Januari 2024 akiwa mkoani Morogoro, alisema tayari amejaza nyaraka zote zinazotakiwa za mkataba wa miaka miwili, hivyo anasubiri mrejesho wake.
Alichosema Rais Samia
Septemba 4 mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa maofisa wakuu waandamizi wa Jeshi la Polisi uliofanyikia jijini Dar es Salaam, alilitaka jeshi hilo kujipanga katika kuhakikisha chaguzi zijazo zinafanyika kwa amani bila kuigawa nchi.
Alisema Serikali anayoiongoza inakwenda kulitafutia fedha Sh125 bilioni, ili kuliwezesha jeshi hilo linaloongozwa na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camillius Wambura kutekeleza majukumu yake katika kipindi hicho.
“Mwakani tuna uchaguzi wa Serikali za mitaa, nitataka Jeshi la Polisi liwe makini katika maeneo mbalimbali kusimamia haki itendeke na kusimamia usalama katika chaguzi zetu ziende kwa njia ya usalama.
“Nilimwambia IGP Wambura, akasema sawa, ila akasema ana changamoto, akanileta bajeti ya karibu Sh125 bilioni ambayo nakwenda kupekua na ikiwezekana niipate yote, ili Jeshi la Polisi changamoto zote ziondoke muweze kufanya kazi vizuri,” alisema Rais Samia na kuongeza:
“Tegemezi letu ni nyie, ndiyo mnalinda mali na usalama wetu, hatuna jeshi lingine.”
Alisema anakwenda kuihangaikia bajeti hiyo aliyoelezwa, “ili niwawezeshe msimame vyema na mkasimamie vyema chaguzi zetu. Nasema kila siku Tanzania ni moja, hakuna Tanzania nyingine, tukiiweka vizuri ni sisi au tukiipasua pasua ni sisi.
“Tunakwenda kuliwezesha Jeshi la Polisi, tunakwenda kuliwezesha ili muweze kufanya ile sehemu yenu ya kuiweka vizuri hii Tanzania yetu,” alisema Rais Samia.