Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi yawaita askari wastaafu kwa mkataba

Muktasari:

  • Kulingana na kanuni za Jeshi la Polisi, askari mwenye cheo cha kuanzia Konstebo hadi Sajini hutakiwa kustaafu kwa lazima anapotimiza umri wa miaka 45 wakati Inspekta ni miaka 55 na Mrakibu Msaidizi (ASP) hadi Kamishina ni miaka 60.

Dar/mikoani. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imetoa ofa kwa askari polisi waliostaafu kurejea kazini kwa mkataba, ili kuliongezea nguvu jeshi hilo kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.

 Ofa hiyo inayomtaka mwombaji awe amestaafu ama mwaka 2023 au mwaka 2024, awe na afya njema, awe na rekodi ya tabia njema na mwenendo mwema na mkataba huo inatolewa kwa miaka miwili tu.

Baadhi ya askari wa vyeo vya chini katika mikoa ya Mara, Shinyanga, Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Njombe, Mbeya na Lindi wamepongeza uamuzi huo, lakini wakashauri kama ni kuliongezea nguvu jeshi hilo, uamuzi huo uendane na vifaa. 

Kwa mujibu wa askari hao waliozungumza na Mwananchi Digital, vifaa vya mwisho kununuliwa, hususan magari ilikuwa kwa mkupuo kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015 na kwamba mengi yanayotumika hivi sasa katika mikoa mbalimbali ni chakavu au “spana mkononi.”

Magari hayo yaliponunuliwa, vyama vya upinzani vilidai Serikali ilikuwa imenunua magari ya washawasha 777 kwa thamani ya Sh420 bilioni na hoja hiyo iliibuka mara kwa mara bungeni, huku ikikanushwa na Hamad Masauni, wakati huo akiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani. 

Masauni ambaye sasa ni Waziri wa wizara hiyo, amesema magari ya washawasha (ya kumwaga maji kutawanya watu) yaliyokuwa yamenunuliwa nchi nzima yalikuwa 32 tu. 


Kuongezwa muda jambo binafsi

Alipotafutwa Waziri Masauni azungumzie suala la askari wastaafu kuongezewa muda leo Aprili 4, 2024 amesema hilo ni jambo binafsi na si kwa kwamba linafanyika kwa wote.

“Miaka yote kigezo hicho kipo, na ni suala la kawaida katika kazi. Mtu anafanya kazi ukishafika muda wa kustaafu anastaafu kutoa nafasi kwa vijana wengine ili apumzike, lakini ikitokezea kuna umuhimu mtu au kuna haja fulani anaongezewa (muda) na iko hivyo Serikalini,” amesema.

Amesema suala la kuongezewa mtu anatakiwa kuomba mwenyewe. “Ikitokezea wawili, watatu au wanne inategemeana na haja si kwa sababu ya uchaguzi, kwani ni mara ya kwanza tunaingia katika uchaguzi? Miaka yote tumekuwa tukifanya uchaguzi.

“Kama ikitokezea kuna askari wanahitajika ni jambo la mtu mmoja mmoja na si la watu wote,” amesema.

Mapema, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi alipoulizwa kuhusu suala amesema hana taarifa rasmi ya mikataba ya muda, lakini amejikita kwenye uwezeshaji wa Jeshi la Polisi kibajeti na kivifaa.

Amesema ndani ya miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita, imekuwa ikiongeza bajeti ya jeshi hilo. 

“Mwaka 2020/21 bajeti ya Polisi ilikuwa Sh565 bilioni na mwaka 2023/24 bajeti yake imefikia Sh798 bilioni na hiyo inamaanisha Serikali inatoa kipaumbele katika uboreshaji wa Jeshi la Polisi si tu kwa watumishi wake, bali pia vifaa vya kazi ikiwemo ofisi,” amesema. 

Matinyi ameongeza kuwa ndani ya kipindi hicho, magari ya Polisi 290 yalinunuliwa na pikipiki 105 na jumla ya vituo vya Polisi 18 na ofisi 10 za makamanda wa mikoa vimejengwa.

“Hii ni mifano tu ya sehemu inayoletwa na ongezeko la bajeti na Serikali imenuia kuliimarisha Jeshi la Polisi kwa ajili ya usalama wa raia na mali zao,” amesema Matinyi.


Walichokisema askari polisi

Kulingana na taarifa zilizolifikia Mwananchi Digital kutoka mikoa mbalimbali nchini ni kuwa askari wa vyeo vya chini na vya kati waliostaafu mwaka jana na mwaka huu ambao wameitwa kurejea kazini kwa mkataba maalumu wa miaka miwili ambayo uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu. 

“Ni kweli kuna hilo jambo, ila si la lazima kuomba. Yaani waliostaafu na kama unajiona una nguvu basi unaruhusiwa kuingia mkataba ni wa miaka miwili tu. Kwa kweli sijui sababu, ila nahisi ni kuongeza nguvu kazi,”amesema mmoja wa askari mkoani Mbeya.

“Kuna mwenzangu alistaafu Julai mwaka jana naye amechangamkia hiyo fursa kwa sababu unajua sisi wa vyeo vya chini kama Konstebo, Sargent (Sajini) na Major (Stesheni Sajini) tunastaafu tukiwa na nguvu zetu kabisa,” amedokeza. 

Kulingana na kanuni za Jeshi la Polisi, askari mwenye cheo cha kuanzia Konstebo hadi Sajini hutakiwa kustaafu kwa lazima anapotimiza umri wa miaka 45 wakati Inspekta ni miaka 55 na Mrakibu Msaidizi (ASP) hadi Kamishina ni miaka 60.

Ofisa wa Polisi mwenye cheo cha ASP mkoani Ruvuma amesema utaratibu huo ni mzuri hasa ikizingatiwa kuwa kuanzia 2015 alipoingia Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli, ajira zilikuwa za nadra hadi alipoingia Rais Samia.

“Ukizingatia ajira zilisimama kwa muda mrefu hadi alipokuja mama yetu mpendwa (Rais) na hapo hapo askari wanastaafu na wengine hata kufa ni lazima nguvu kazi iliyopo isingetosha kusimami uchaguzi kwa ufanisi.

 “Pamoja na ofa, sio kila askari aliyestaafu atachukuliwa. Hapana. Kuna vigezo kimojawapo ni lazima ukubali kwa hiyari, uwe na afya njema na uwe na rekodi nzuri ya utendaji na tabia. Kuna kamati kabisa itawachuja hawa watu,” ameeleza. 

“Hili sio la askari wa chini tu, hili ni la wote, ndio maana unaona kuna wakubwa walishastaafu tangu mwaka jana unawaona wako kazini kama hapo Dar es Salaam na CCP (Chuo cha Polisi Moshi). Ni jambo jema sana Serikali imefanya,” amesisitiza.

Ofisa huyo amesema ipo haja ya Serikali kupitia utaratibu wa askari wa vyeo vya chini kustaafu mapema wakiwa na nguvu na wale wa vyeo vya juu kwenda hadi miaka 60, wakati kazi za shuruba zinafanywa na hao wa vyeo vya chini.

“Mimi nafikiri hawa wa vyeo vya chini sheria iwaruhusu kustaafu kwa hiyari akifika 55 na kama ana nguvu aende hadi 60, lakini tunaruhusu vijana wenye nguvu, wenye ujuzi na uzoefu wanaingia mitaani si sawa,” ameeleza ofisa huyo.

Askari wa cheo cha Koplo Jijini Arusha ameipongeza Serikali kwa uamuzi wa kuwapa mikataba wenzao waliostaafu na kupendekeza utaratibu huo usisubiri tu wakati wa uchaguzi, bali ufanyike miaka yote hasa kwa askari wale wa vyeo vya chini.

Kwa upande wake, askari mwingine aliyestaafu Januari 2024 akiwa mkoani Morogoro, amesema tayari amejaza nyaraka zote zinazotakiwa za mkataba wa miaka miwili, hivyo anasubiri mrejesho wake.