Polisi wapewa angalizo usimamizi wa mifumo

Muktasari:
- Mambosasa asema cheo si mapambo wala zawadi, ni stahili ya mtumishi anayetimiza wajibu wake.
Dar es Salaam. Askari wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini (DPA), wametakiwa kusimamia mifumo ya jeshi hilo na kuangalia changamoto zilizoainishwa kwenye ripoti ya Tume ya Kuboresha Mifumo na Taasisi za Haki Jinai nchini.
Pia, wametakiwa kuwekeza katika majukumu yanayotimiza dhima nzima ya jeshi hilo, ili wote wanufaike na matunda ya kazi wanayoifanya.
Julai 2023, Tume ya kuangalia namna ya kuboresha Taasisi za Haki Jinai iliwasilisha ripoti kwa Rais Samia Suluhu Hassan ikionyesha malalamiko ya wananchi kubambikiwa kesi, huku matukio yasiyofaa kwa jamii kwa baadhi ya askari yakiongezeka hasa katika vituo vya Polisi.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Othman Chande alisema pamoja na mambo mengine malalamiko yaliyoelekezwa kwa jeshi hilo ni udhaifu wa jeshi hilo, ambalo walishauri lifumuliwe.
Akizungumza leo Februari 17, 2024 wakati wa hafla ya kuwaaga watumishi waliomaliza muda wao na kuwapongeza waliofanya vizuri mwaka 2023, Mkuu wa Chuo hicho, Dk Lazaro Mambosasa amewataka wajisimamie kwa mujibu wa sheria ya jeshi hilo, badala ya kusubiri maelekezo kutoka makao makuu.
“Tusimamie mifumo ya Jeshi la Polisi tuangalie changamoto zilizoainishwa katika ripoti ya Tume Haki Jinai ambalo Jeshi la Polisi likielekezwa ni mambo gani linapaswa kubadilika,” amesema Dk Mambosasa.
Dk Mambosasa ambaye amesema amepandishwa cheo juzi, kutoka Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACAP) kuwa Naibu Kamishna (DCP), amewataka askari kuwa mabalozi wazuri wa Jeshi la Polisi ili kuwa watumishi wema.
“Mimi ni mstaafu mtarajiwa, likizo yangu ya kustaafu nitaianza Desemba mwaka huu na Februari mwakani nitaondoka rasmi, cheo hiki nimesafiria miaka minane, cheo si mapambo wala zawadi, ni stahili ya mtumishi anayetimiza wajibu wake na mwajiri akaona matunda yako,” amesema.
Amebainisha kuwa Jeshi la Polisi lina jukumu la kuisaidia Tanzania kuwa mahali salama pa kuishi, lakini pia kuvutia wawekezaji kwa kuwa sehemu yenye vurugu hawawezi kuwekeza.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Operesheni na Mafunzo (CP), Awadhi Juma Haji, Naibu Kamishna Mkuu wa Kitengo cha Utawala Makao Makuu (DCP), Anthony Rutashuburugukwa aliwataka askari kila baada ya mwaka kufanya tathmini ya malengo waliyojiwekea.
Amesema ni muhimu kuangalia ni wapi hamkutimiza wajibu wenu na wapi mnapaswa kujipanga ili malengo yenu yatimie.
“Si wote wanaofikia hatua ya kustaafu kwa heshima, ziko njia nyingi za mtumishi kukoma kuna shida ya kiafya, kufukuzwa kazi na wakati mwingine kushushwa cheo, kwa mliobaki kafanyeni kazi kwa bidii ikawe ni kichocheo cha ninyi kupanda madaraja,” amesema Rutashuburugukwa.
Ameueleza uongozi wa chuo hicho kwa mujibu wa kitabu cha mwongozo wa Jeshi la Polisi (PGO), wale wote waliofanya vizuri wanastahili kupongezwa, amewataka askari hao kuongeza bidii, nidhamu na weledi.