Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu maji kujaa Mto Mzinga zatajwa, Tarura yaeleza mikakati

Muktasari:

  • Mto Mzinga wenye zaidi kilometa 30 umeanzia wilayani Kisarawe hadi Temeke ambapo maji yake unamwaga katika Bahari ya Hindi.

Dar es Salaam. Wakati wananchi wa mitaa ya Kata ya Zingizwa wilayani Ilala jijini Dar es Salaam wakipaza sauti kuhusu kujaa maji katika Mto Mzinga kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, mamlaka zimetaja sababu na hatua wanazochukua kutatua kero hiyo.

Kata ya Zingiziwa inaundwa na mitaa minane ya Ngobedi, Zingiziwa, Lubakaya, Gogo, Kimwani, Nzasa, Somelo na Zogo Ali.

Mwananchi leo Jumanne Aprili 29, 2025 imefika katika eneo hilo na kushuhudia wananchi wanavyopata adha kuvuka kufuata huduma za kijamii na wengine kujitafutia riziki kutokana huku wakitozwa kati ya Sh500 hadi Sh1,000 kwa vijana walioamua kujiajiri kuifanya kazi hiyo.

Kujaa maji katika eneo hilo kumeelezwa hujirudia mara kwa mara mvua zinaponyesha na kusimamisha shughuli za kiuchumi na kijamii, huku wananchi wakieleza wameshazilalamikia mamlaka lakini zimeshindwa kuchukua hatua.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mamlaka hizo akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema sababu ya kujaa maji katika mto huo kumechangiwa na shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo na ujenzi.

“Ni kutokana na shughuli hizo za kibinadamu, mto unazidiwa na ukiangalia hata kwenye madaraja yake kumejaa uchafu na hivyo kusababisha maji kubadili njia yake ya asili yanapotakiwa kwenda,” amesema Mpogolo.

Mpogolo amesema ni kutokana na hilo wamekuwa wakitumia sheria ndogondogo na zile za Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kuwaadhibu wahusika sambamba na kuendelea kutoa elimu kwa kushirikiana na Wenyeviti wa Serikali za Mtaa.

Pamoja na changamoto hizo, Mkuu huyo wa Wilaya, Mpogolo amesema tayari wameanza kushugulikia tatizo hilo ambapo wanajenga madaraja saba ya mawe kwenye mto huo katika Mtaa wa Mwanagati na Magole huku Sh900 milioni zikiwa zimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ya Zingiziwa, Jafari Masanja amesema licha ya kujitahidi kutoa elimu, wananchi wamekuwa wazito katika kufuata sheria za mazingira.

“Katika changamoto hii utakuwa  kuna wale walionunua viwanja vya hatua 12 kwa 10 karibu na mto halafu anataka kujenga nyumba kubwa ndio mwisho wa siku anavamia hadi eneo la mto,” amesema Masanja.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo amesema wamekuwa wakishirikana na ofisi ya kanda namba saba katika kuhakikisha wanaojenga wanakuwa na vibali japo ni ngumu kusimamia watu wote.

Wito wake Masanja ameomba Serikali iangalie changamoto hiyo kwa jicho la tatu kwa kile alichoeleza wameshawasilisha kero hiyo katika ngazi mbalimbali lakini kunaonekana kuwa na uzito katika kulishughulikia.

“Changamoto hii tunaomba ishughulikiwe haraka ukizingatia shughuli zote za kijamii za Kata zinapatikana, huku ikiwemo kituo cha afya ambacho uwekezaji wake umeigharimu serikali zaidi ya Sh700 milioni, tuna ofisi ya Kata, mahakama ya mwanzo na wananchi tegemeo lao ni hii barabara ambapo mto Mzinga unakatisha,”amesema Mwenyekiti huyo.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) Mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Mkinga amesema kero ya kujaa maji katika eneo hilo wanaijua na tayari katika bajeti inayoanza Julai mwaka huu wametengea fedha Sh650 milioni za kujenga madaraja mawili makubwa ili maji yaweze kwa urahisi na tayari kumeshafanyiwa usanifu.

Sambamba na hilo, Mkinga amesema mpango ni barabara hiyo ya Zingiziwa kujengwa kwa kiwango cha lami, ambapo wanatarajia kuingiza katika bajeti ya mwakani au DMDP awamu ya pili.

Aidha amesema sababu zinazochangia eneo hilo kujaa maji mbali na shughuli za kibinadamu pia ni mabadiliko ya tabia nchi hali inayosababisha maji kubadili mwelekeo wake.

Wito wake kwa wananchi kuendelea kuvuta subra kwa kuwa serikali inalishughulikia huku akieleza changamoto za ubovu wa barabara zipo maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

Aidha kwa maeneo ambayo wananchi wanaona imefika hatua ya kuhatarisha usalama wao, kukatika mawasiliano, amewataka wasisite kutoa taarifa ili hatua za haraka zichukuliwe na za muda mfupi ikiwemo kuweka mawe ili pafaye kupitika.