Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rushwa, ufisadi unavyowatesa viongozi Afrika

Muktasari:

Sheria ni msumeno. Kukamatwa kwa mwanasheria mkuu wa zamani wa Nigeria, Mohammed Adoke kunaonekana kuwa ni mwendelezo wa serikali za Afrika kushughulikia viongozi waliofanya vitendo viovu wakati wakiwa madarakani.


Dar es Salaam. Sheria ni msumeno. Kukamatwa kwa mwanasheria mkuu wa zamani wa Nigeria, Mohammed Adoke kunaonekana kuwa ni mwendelezo wa serikali za Afrika kushughulikia viongozi waliofanya vitendo viovu wakati wakiwa madarakani.

Mbali na serikali hizo, Marekani imeongeza nguvu kwa kuwabana wale inaowatuhumu kwa makosa ya rushwa, ikitangaza kuwazuia kuingia katika nchi hiyo kubwa duniani.

Adoke alikamatwa akiwa Dubai mapema wiki hii, ikiwa ni miezi saba tangu taasisi ya kupambana na rushwa ya Nigeria kutoa hati ya kumkamata ikiwa ni sehemu ya uchunguzi mkubwa wa kashfa ya sekta ya mafuta, akituhumiwa kuuza eneo la mafuta linalojulikana kwa jina la OPL 245 kwa dola 1.3 bilioni za Kimarekani.

Kwa mujibu wa Mike Ozekhome, ambaye ni mwanasheria wake, Adoke alikamatwa na polisi wa kimataifa (Interpol) Jumatatu baada ya kwenda Dubai ambako alikuwa na miadi ya kumuona daktari.

Aprili mwaka huu, Tume ya kupambana na ufisadi Nigeria ilitoa hati za kumkamata Adoke na Waziri wa zamani wa mafuta wa nchi hiyo, Dan Etete na meneja wa kampuni ya mafuta ya Italia, Eni.

Adoke ni mmoja wa viongozi wa juu wa serikali za Afrika ambao wamekumbana na kadhia kama hiyo katika miaka ya karibuni, hasa mwaka huu.

Viongozi hao wamejikuta katika misukosuko wanapomaliza muda wao. Wapo waliojihusisha na vitendo vya rushwa na matumizi mabaya fedha za wananchi ambazo zilipaswa kutumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo na matumizi mabaya ya madaraka.

Hivi karibuni baadhi viongozi wamechukuliwa hatua mbalimbali nje ya nchi zao na baada ya kustaafu, jambo ambalo wengi walitamani kulishuhudia.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Innocent Shoo alisema suala hilo ni gumu kutokea katika nchi nyingi za Afrika kwa kuwa mfumo wa kikatiba kwa nchi nyingi za Afrika unawabeba viongozi badala ya wananchi.

Shoo alisema kwa kawaida kikatiba mwananchi ndiye anapaswa kutetewa zaidi kuliko kiongozi, jambo ambalo ni tofauti.

“Kiongozi alikuwa ni mtu ambaye hawezi kuguswa, anakula pesa akimaliza anaondoka zake, lakini mfumo wa kikatiba ukiwa mzuri kama nchi za Ulaya na Marekani hata rais anafungwa na ndiyo maana sasa hivi tunaona Rais Donald Trump anavyosumbuliwa kwa sababu katiba inaruhusu,” alisema Shoo

Alisema barani Afrika bado viongozi wana nguvu kuliko taasisi ambazo zinaonekana kuwa dhaifu, ukijumuisha Bunge, Mahakama kwa sababu mtu mmoja akisema kitu wote wananyamaza jambo linalomfanya kuwa hata na uwezo wa kupindua maamuzi ya kimahakama.

Lakini akasema hali inaanza kubadilika.

“Siku hizi kuna mageuzi ya kikatiba katika nchi za Afrika ya mashariki, watu wameelimika na taasisi nyingi zisizo za kiserikali zimekuwa zikiingilia suala hili na kuelimisha jamii. Afrika inahitaji taasisi imara na siyo watu imara lakin,” alisema.

Naye Bubelwa Kaiza, mkurugenzi wa taasisi ya utawala bora ya Fordia, alisema watu wengi Afrika hawana uelewa kuhusu mambo ya utawala, jambo ambalo limefanya viongozi kujifanyia wanavyotaka na kuonekana hawana hatia.

“Hii ni kwa sababu nchi nyingi za Afrika bado zinaishi katika utamaduni wa zamani wa kuwaachia machifu kila kitu, jambo ambalo linafanya wananchi kushindwa kuwauliza viongozi kitu chochote wanachofanya,” alisema.

“Kwa sababu hiyo watu wamekuwa wakimuona Rais kuwa mtu tofauti mara tu baada ya kuchaguliwa, tofauti na aliyekuwa mtaani. Kinyume na hali ilivyo katika nchi za Ulaya na Marekani ambako wanaendeshwa kikatiba na kisheria.”

Alisema itachukua muda kwa nchi za Afrika kuanza kuwachukulia hatua viongozi wa serikali wanaofanya maovu wanapokuwa madarakani kwa sababu katiba nyingi za Afrika ni kizazi cha katiba za wakoloni.

Wakati wakiona udhaifu katika katiba za nchi za Afrika, tuhuma za rushwa zinamkabili pia Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Kenya, Amos Wako ambaye sasa amepigwa marufuku kuingia na kufanya biashara na Marekani.

Marekani pia imezuia familia ya Wako kuingia nchini humo akiwamo mke wake, Flora Ngaira na mtoto wake wa kiume, Julius.

Katika hatua nyingine, polisi nchini Afrika kusini walimtia mbaroni waziri wa zamani wa usalama na kada mwandamizi wa ANC kwa tuhuma za ufisadi.

Bongani Bongo ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais wa Afrika Kusini, anatuhumiwa kutoa hongo kwa wakili wa kesi ya Serikali katika uchaguzi wa Bunge mwaka 2017.

Suala hilo limefika mbali zaidi baada ya Julai mwaka huu Waziri wa Fedha wa Kenya, Henry Rotich kusimamishwa kazi ikiwa ni siku moja baada ya kushtakiwa mahakamani kwa ufisadi.

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, waziri wa zamani wa afya alimakatwa kwa madai ya kutumia vibaya fedha zilizotolewa kwa ajili ya ugonjwa wa ebola.

Nchini Msumbiji, waziri wa zamani wa fedha, Manuel Chang aliyekamatwa akiwa Afrika Kusini, aliombwa kurejeshwa nchini kwake kujibu mashtaka ya matumizi mabaya ya fedha.