Prime
Bundi aweka kambi Moshi mjini, Mchengerwa ageuka mbogo
Muktasari:
- Julai 25, Waziri Mchengerwa alifanya kikao na watumishi wa Mkoa wa Kilimanjaro ambapo alisema Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Mwajuma Nasombe yupo timu ya Meya na wote wanasuguana na Mbunge wa Jimbo hilo, Ibrahim Shayo hali ambayo inaweza kuipa wakati mgumu CCM katika uchaguzi mkuu 2030.
Moshi. Ni kama msuguano wa kisiasa unaotikisa Jimbo la Moshi mjini haujapatiwa ufumbuzi na sasa Waziri wa Afya, ambaye ni waziri mlezi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mohamed Mchengerwa amewashukia Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe, Mkurugenzi wa Mwanga, Mwanashabani Mrope na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumo.
Haya yanajiri miezi michache tu tangu Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira kufanya ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro na moja ya ajenda aliyoishughulikia katika vikao vya ndani ni msuguano wa kisiasa unaolitikisa Jimbo la Moshi mjini.
Hii ni baada ya vikao vya kamati ya siasa ya wilaya na mkoa kufanyika kwa nyakati tofauti vikihusisha kamati za usalama na maadili bila kupata muafaka huku kada na viongozi wawili wa CCM wakitajwa kuwa kiini cha mgogoro.
Machi Mosi, 2026 kulifanyika kikao cha maridhiano chini ya mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Hamid, kwa faragha hadi usiku bila kupata ufumbuzi wa mgogoro huo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaaban Mlewa, Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Nurdin Babu, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mbunge wa Moshi mjini Ibrahim Shayo, Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumo.
Wengine waliohudhuria kikao ni mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC), Seleman Mfinanga, Katibu Mwenezi wa CCM Manispaa ya Moshi, Athman Ally na Diwani wa Kata ya Bomambuzi, Juma Raibu na mwenyekiti CCM wilaya, Faraji Swai.
Juzi, Julai 25,2026, Waziri Mchengerwa alifanya kikao na watumishi wa Mkoa wa Kilimanjaro ambapo alisema Mkurugenzi wa Manispaa yupo timu ya meya na wote wanasuguana na Mbunge wa Jimbo hilo, Ibrahim Shayo hali ambayo inaweza kukipa wakati mgumu CCM katika uchaguzi mkuu wa 2030.
Mchengerwa alienda mbali na kueleza kuwa kama angekuwa waziri mwenye mamlaka ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) angefanya uamuzi mgumu siku hiyohiyo.
“Na hapa nasikia mkurugenzi anavutana na mbunge, mkurugenzi yeye yupo upande wa Meya, mbunge yupo na wananchi. Meya na mbunge wanavutana. Si tumemaliza uchaguzi! Mkurugenzi unavutana na mbunge (hamtaki mbunge).
“Mkurugenzi alivutana na mbunge aliyeondoka unataka mbunge wa aina gani. Hebu nisaidie mkurugenzi. Waziri Mkuu alipokuja hapa alitoa maagizo. Hebu niambie mkurugenzi na hii sio mara ya kwanza,” alisema Mchengerwa.
Alisema: “Mkurugenzi unafanya kazi nzuri ya kukusanya mapato lakini huna ushirikiano na mwakilishi wa wananchi, utawapa kazi kubwa CCM.”
Aidha, Mchengerwa alisema mbunge ana nafasi yake ya kuwasaidia wananchi na kuwasemea hivyo amuache afanya kazi yake.
“Mara ya mwisho yalitokea haya haya mkurugenzi hamtaki mbunge, sasa unataka mbunge wa aina gani, kwa nini usimpe nafasi mbunge akafanya kazi yake kuwasaidia wananchi, unategemea utakaa hapa miaka mitano? Umeshakaa hapa miaka mitatu, mimi nakufahamu na aliyekupendekeza uje hapa ni mimi, nikiwa Waziri wa Tamisemi.
“Na hata huko ulipotoka uligombana na watu mimi nimenyooka sana, kama umezoea kutoambiwa mimi nakwambia kwa sababu sio utaratibu wangu mimi nimenyooka sana,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Ningekuwa Tamisemi ningefanya uamuzi mgumu. Sio kwa Mkurugenzi tu hata kwa wenyeviti wa halmashauri kwa sababu najua mipaka yangu ya kazi. Ningefanya uamuzi hapahapa mnabahati sipo huko.”
“Ningemsimamisha meya kwa sababu ni mamlaka ya Waziri wa Tamisemi, mimi najua mipaka yangu ya kazi ili kusudi kuweka usawa watu wafanye kazi. Ningemsimamisha na tungekuwa na uchaguzi,” alisema Mchengrwa.
Mwanga nako hakujapoa
Akiwa katika kikao hicho, pia aligusia mkuu wa wilaya ya mwanga na mkurugenzi wa halmashauri hiyo kutokuelewana wao kwa wao, akisema hali hiyo inachelewesha maendeleo kwa wananchi.
“Haya, kule Mwanga, mkuu wa wilaya anavutana na mkurugenzi. Mwashabani alihamishwa kutoka Korogwe alikuwa anavutana na watendaji, kaja hapa anavutana na mkuu wa wilaya. Mkurugenzi unamtaka nini mkuu wa wilaya, mnagombana nini,” alihoji Mchengerwa.
Alisema: “Mnavutana nini? Serikali ni moja mnachelewesha maendeleo ya wananchi. Kila mtu ajue mipaka yake mkuu wa wilaya ana mamlaka makubwa kwenye wilaya yake. Mkurugenzi ana mamlaka makubwa kwenye eneo lake, lakini lazima tuzungumze lugha moja. Kwa sababu ninyi mkivutana hawa wananchi watakuwa kwenye hali gani, Mnaenda kukipa taabu chama.”
Azungumzia mshikamano
Mchengerwa alisema hakuna wakati ambapo viongozi wanatakiwa kushikamana wakati kama huu kutokana na mambo yanayoendelea.
“Hakuna wakati ambapo tunahitaji kushikamana kama wakati huu.Hakuna wakati ambapo viongozi wa Serikali tunapaswa kushikamana kama huu kwa sababu kuna mambo mengi yanaendelea,” alisema Mchengerwa.
Aliongeza; “Kuna watu wasiotamani kuona nchi hii inatawaliwa, wanatamani kuona inapasuka na walijaribu miaka mingi kuhakikisha chama tawala kinabomoka. Hakuna wakati ambapo sisi Watanzania tunahitaji kushikamana kuwa wazalendo kwa nchi yetu kama wakati huu.”
Aliwataka viongozi wabadilike kwani cheo ni kizuri ukiwa nacho, cheo kikiondoka wewe sio kitu, hata simu watu hawapokei. “Tubadilike tuwasaidie wananchi. Nchi hii ina kila kitu, ina rasilimali zote, tunahitaji kufanya kazi kwa bidii, tunahitaji kuwa waadilifu, wanyenyekevu na kupiga vita rushwa”
"Mngekuwa kwenye mamlaka yangu nishawaondoa, kwenye wizara yangu wananifahamu, waulizeni wananijua, mambo kama haya nakuweka pembeni wala sikuachi ukitoka wewe yupo mwenye uwezo na anafanya kazi vizuri,"
Alipotafutwa kwa njia ya simu Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe, hakutaka kuzungumzia suala hilo akisema amemwachia Mungu.
“Sina comment (maoni) kwenye hilo, Mwenyezi Mungu ndiye anayejua zaidi,” amesema Mkurugenzi huyo
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mwanga, Mwashabani Mrope alipoulizwa kuhusu kauli ya Waziri Mchengerwa amesema, "Wewe ni mamlaka ya uteuzi au ya Rais? Hapana, nono, na kukata simu.
Akizungumzia kauli ya Mchengerwa, Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumo amesema kuwa endapo waziri angejipa muda wa kutosha angeweza kuujua ukweli badala ya kusikiliza upande mmoja pekee.
“Mheshimiwa waziri akijipa muda ataujua ukweli. Muda mara nyingi huwa ni jibu sahihi sana, sisi tumesema tutanyamaza maana kunyamaza nako ni jibu lakini naamini Mheshimiwa Waziri akijipa muda ataujua ukweli,"amesema Kidumo.
Kidumo ameongeza kuwa, Waziri akipata nafasi ya kujua ukweli, atagundua mambo ambayo hakuyafahamu awali kabla ya kutoa uamuzi.
"Nina uhakika akijua ukweli atajilaumu sana kwa nini hakusikiliza na kujipa muda kusikiliza upande wa pili. Kujua ukweli upo hivi... na alichoambiwa, nina uhakika atajilaumu sana kwa nini asingejipa muda akapata ukweli kuliko uamuzi aliofanya,"amesema Kidumo