Prime
'Black Tax' inavyokwamisha vijana kujijenga kiuchumi
Muktasari:
- Ingawa si kodi inayotozwa na Serikali, wataalamu wamesema kwa baadhi ya vijana mzigo huo una athari zinazofanana na kodi kwa sababu hupunguza uwezo wa kuweka akiba
Dar es Salaam. Mshahara ukiingia mwisho wa mwezi, vijana wengi huanza kupanga namna ya kulipa kodi ya nyumba, nauli, chakula na kuweka akiba.
Lakini kabla hawajafikia malengo hayo, simu huanza kuita mzazi akihitaji fedha za matumizi, mdogo ada ya shule, ndugu matibabu, mwingine mtaji wa biashara au mchango wa shughuli za kifamilia.
Kwa wengi, hali hiyo haitokei mara moja bali imekuwa sehemu ya maisha ya kila mwezi, wataalamu wa uchumi na fedha wanaieleza kama ‘Black Tax’, dhana inayomaanisha wajibu wa kijamii unaomlazimu mtu aliyefanikiwa kifedha kuwasaidia wazazi, ndugu na jamaa wanaomtegemea.
Ingawa si kodi inayotozwa na Serikali, wataalamu wamesema kwa baadhi ya vijana mzigo huo una athari zinazofanana na kodi kwa sababu hupunguza uwezo wa kuweka akiba, kuwekeza na kujenga mali za muda mrefu.
Dhana hiyo ilianza kujadiliwa kwa kiwango kikubwa nchini Afrika Kusini, lakini sasa inaonekana katika nchi nyingi za Afrika, ikiwamo Tanzania ambako familia nyingi bado hutegemeana kutokana na kipato kidogo, ukosefu wa mifumo imara ya hifadhi ya jamii na ongezeko la gharama za maisha.
Kwa Tanzania, hali hiyo imeonekana zaidi kwa vijana wanaopata ajira za kwanza, hasa waliotoka katika familia zenye kipato cha chini.
Mara nyingi wao hubeba jukumu la kulipia ada za wadogo zao, kugharamia matibabu ya wazazi, kuchangia shughuli za kifamilia na kusaidia ndugu wengine wanaokabiliwa na changamoto za kifedha.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi wamesema utamaduni wa kusaidiana ni sehemu ya maisha ya Watanzania, lakini wakati mwingine unakuwa mzigo unaowafanya vijana washindwe kutimiza malengo yao binafsi.
Rehema Mallya, amesema tangu aanze kazi miaka minne iliyopita amekuwa akitumia sehemu kubwa ya mshahara wake kusaidia wazazi na ndugu zake, jambo ambalo limechelewesha ndoto yake ya kujenga nyumba.
"Kila mwisho wa mwezi kuna anayehitaji ada, mwingine matibabu au chakula. Siwezi kuwatelekeza kwa sababu walinisomesha, lakini ukweli ni kwamba mpaka leo sijaanza hata akiba ya maana. Wakati mwingine unahisi unaifanyia kazi familia nzima kuliko maisha yako mwenyewe," amesema Rehema.
Kwa upande wake, John Mhando amesema kusaidiana ni msingi wa utamaduni wa Kitanzania, lakini baadhi ya familia huzidisha matarajio kwa ndugu anayepata ajira.
"Ukishapata kazi, kila tatizo linaelekezwa kwako. Wengine hata hawajitahidi kutafuta suluhisho kwa sababu wanaamini upo. Hapo ndipo msaada unageuka utegemezi, na mwisho wake hata anayesaidia anaanza kulemewa," amesema Mhando.
Wakati hao wakisema hivyo Asha Msuya, amesema si sahihi kuiona hali hiyo kama mzigo pekee kwa sababu familia nyingi zimeendelea kutokana na mshikamano.
"Kama kaka yangu asingetusomesha baada ya baba kufariki, leo tusingekuwa tulipo. Tatizo si kusaidiana, tatizo ni pale ambapo mtu mmoja anabebeshwa majukumu ya kila mtu huku wengine wakikaa wakisubiri msaada," amesema.
Victor Nyoni amesema mhitimu wa chuo kikuu anayetafuta ajira, matarajio makubwa kutoka kwa familia huanza hata kabla mtu hajapata kipato.
"Unamaliza chuo tu tayari kila mtu anaamini utaajiriwa kesho na kuanza kuwasaidia. Hilo linaweka shinikizo kubwa kwa vijana na wakati mwingine linawafanya wakubali kazi yoyote au hata kutafuta fedha kwa njia zisizo sahihi ili kukidhi matarajio ya familia," amesema Nyoni.
Akizungumzia hilo, Mtaalamu wa Saikolojia, Mwalimu Cosmas Madulu amesema hata msaada kwa ndugu unapaswa kuutoa kwa kuzingatia uwezo wako.
“Usijibebeshe mzigo wa kupokea ndugu wakakaa nyumbani kwako unawasaidia. Ni vema ukawasaidia wakiwa mbali. Haina maana kutoa msaada huku unanung’unika,” amesema.
Wasemavyo wachumi
Akizungumza na Mwananchi, mtaalamu wa uchumi, Felix Masawe amesema kusaidiana ni sehemu ya utamaduni wa Kiafrika, lakini kunapaswa kufanyika kwa kuzingatia uwezo wa anayetoa msaada.
"Kijana anapotumia sehemu kubwa ya kipato chake kusaidia familia bila kuwa na mpango wa fedha, anachelewesha uwekezaji, anashindwa kuweka akiba na wakati mwingine anakopa ili kukidhi mahitaji ya wengine. Mwisho wake anabaki kwenye mzunguko wa kutegemea mshahara maisha yake yote," amesema Masawe.
Kwa upande wake, mchumi Restituta Madoshi amesema changamoto hiyo inapaswa kutazamwa pia kama suala la maendeleo ya uchumi wa kaya.
"Kama familia nzima inamtegemea mtu mmoja kwa muda mrefu, maendeleo yanakuwa ya polepole. Kinachotakiwa ni msaada unaowajengea wengine uwezo wa kujitegemea badala ya kuwafanya waendelee kutegemea ndugu yao," amesema Restituta.
Amesema elimu ya fedha inapaswa kuanza ndani ya familia ili kila mwanachama ajifunze kuweka akiba na kuwekeza badala ya kusubiri msaada kila inapojitokeza changamoto.
Mchambuzi wa masuala ya fedha, Gerson Msemo amesema vijana wengi hujikuta kwenye matatizo ya kifedha kwa sababu wanashindwa kuweka mipaka kati ya kuwajibika kwa familia na kujenga maisha yao.
Amesema vijana wengi wanaingia kwenye mikopo isiyo ya lazima kutokana na shinikizo la kifamilia.
"Wapo wanaokopa ili kulipa ada za ndugu, kuchangia harusi au matibabu huku mishahara yao ikiwa haitoshi. Hilo linaweza kuwa mwanzo wa madeni yanayodumu kwa miaka mingi. Ni muhimu mtu ajifunze kusema ukweli kuhusu uwezo wake wa kifedha.
"Kusaidia wazazi na ndugu si kosa. Changamoto inaanza pale unapokuwa chanzo cha kutatua kila tatizo. Ukikosa mipaka unaweza kujikuta huna akiba, huna bima, huna uwekezaji na hata ukipoteza ajira unakuwa katika mazingira magumu," amesema Msemo.
Chanzo cha msongo wa mawazo
Mwanasaikolojia na mshauri wa masuala ya kijamii, Loveness Bigwa amesema utamaduni huo unaweza kuwa chanzo cha msongo wa mawazo kwa vijana wengi.
"Kijana anajikuta ana wajibu wa kuwasaidia wazazi, ndugu, wakati huo huo anatakiwa ajenge familia yake, anunue nyumba na aweke akiba. Mzigo huo ukizidi uwezo wake unaweza kuathiri afya ya akili na hata mahusiano yake," amesema Loveness.
Naye Mhadhiri wa Sosholojia Mathew Mhagama amesema utamaduni wa kusaidiana haupaswi kupotea, lakini unahitaji kubadilika kulingana na hali ya uchumi wa sasa.
"Jamii yetu imejengwa kwenye mshikamano na huo ni mtaji mkubwa. Lakini tusifike mahali mtu mmoja ndiye anakuwa benki ya familia nzima. Hilo linaweza kuua ari ya wengine kutafuta suluhisho la changamoto zao," amesema.