Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rose Kamili, Askofu Kilaini wamshukia Dk Slaa

Mbunge wa viti maalumu wa Chadema, Rose Kamili akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu kauli aliyoitoa aliyekuwa katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa . Kushoto ni binti wa Dk Slaa, Emiliana Slaa na Linus Slaa. Picha na Venance Nestory

Muktasari:

Alisisitiza kuwa japokuwa mihogo siyo chakula kibaya lakini watoto wake, Elimiana na Linus Slaa hawakuwahi kuishi kwa kutegemea chakula hicho ingawa walitelekezwa na baba yao tangu mwaka 2010.

Dar es Salaam. Kauli ya Katibu Mkuu wa zamani wa Chadema Dk Willibrod Slaa kuhusu hatma yake kisiasa imeendelea kutikisa baada ya mke wake wa zamani, Rose Kamili kuibuka na kusema amesikitishwa na kauli alizozitoa mume wake huyo alipozungumza na waandishi wa habari Septemba Mosi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kamili alisema wakati Dk Slaa  anatangaza kung’atuka kwenye siasa alisema amekuwa akila mihogo na familia yake, jambo ambalo si la kweli.

Alisisitiza kuwa japokuwa mihogo siyo chakula kibaya lakini watoto wake, Elimiana na Linus Slaa hawakuwahi kuishi kwa kutegemea chakula hicho ingawa walitelekezwa na baba yao tangu mwaka 2010.

Kamili ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa wa Chadema, alisema Dk Slaa aliwadanganya wananchi aliposema kuwa haongei na mgombea wa urais wa Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa na Waziri Mkuu wa zamani Frederick Sumaye kuwa siyo kweli kwa kuwa amekuwa akiwasiliana na viongozi hao.

Alisimulia kuwa mwaka 1995 wakati Dk Slaa alipoenguliwa na CCM kugombea ubunge Jimbo la Karatu, alikwenda nyumbani kwa Lowassa kuomba ushauri.

“Lowassa alisema ‘mimi nakushauri ujiunge na chama chochote’” alisema Kamili na kuongeza kuwa marafiki zake Dk Slaa nao walimshauri aingie chama chochote.

“Mimi namshangaa anavyosema haongei na Lowassa… hizo chuki anazosema yeye kama padri mstaafu zinatoka wapi?,” alisema Kamili.

Kuhusu Sumaye, Kamili alisema kuwa wiki tatu zilizopita alipigiwa simu na kiongozi huyo akimuulizia namba ya Dk Slaa, baada ya kumtafuta kwenye simu yake bila mafanikio.

“Aliniuliza mbona simu yake haipatikani, nikampa akampigia wakaongea,” alisema.

Mjini Bukoba, Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini amesema anamshangaa Dk Slaa kutoa tuhuma dhidi ya maaskofu kwa kuwa aliwahi kuwa Katibu wa Baraza la Maskofu na anajua wanavyofanya kazi.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi mjini Bukoba, Askofu Kilaini alisema Maaskofu hawanunuliki na kanisa halifungamani na upande wowote wa kisiasa huku akidai huenda kauli hiyo ilimponyoka.

Kauli ya Askofu Kilaini imetolewa ikiwa ni baada ya siku chache zilizopita aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Slaa kutangaza kustaafu siasa huku akiwatuhumu baadhi ya maaskofu kupokea rushwa kutoka kwa mmoja wa wagombea.

‘’Wanasiasa ni wachangiaji wazuri katika hafla mbalimbali za kanisa lakini hata siku moja huwezi kusema maaskofu wamenunuliwa Kanisa linashikilia maadili na kuombea amani kwa Taifa,’’ alisema Kilaini

Pia Askofu Kilaini aliongeza kuwa matamko kama yaliyotolewa na Dk Slaa yanaweza kusababisha mkanganyiko kwenye jamii, huku akionya hatari ya dini kutumika kwenye mijadala kuelekea Uchaguzi  Mkuu.

Aidha alirejea mwaka 2000 kuwa baada ya vurugu kuanza kutokea Zanzibar na wananchi kukimbia, waliitana viongozi wa madhehebu yote ya dini na kutoa tamko la pamoja wakionya dini zisihusishwe kwenye harakati za kisiasa.

Imeandikwa na Goodluck Eliona, Bakari Kiango na Phinias Bashaya