Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi wasimulia kero ya barabara, matumaini mapya

Madereva bodaboda Kijiji cha Kibaoni "A" na "B" Kata ya Chokaa wakindelea na shughuli za usafirishaji baada ya Serikali kufungua miundombinu ya barabara zilizokuwa changamoto tangu nchi ipate uhuru. Picha na Hawa Mathias.

Muktasari:

  • Hatua hiyo imekuja baada ya Serikali kuanza mkakati wa kufungua barabara katika vitongoji vinne kati ya 19 vilivyopo Kata ya Chokaa, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, ambavyo imeelezwa kuwa tangu nchi ipate uhuru miaka 60 iliyopita havijawahi kuwa na miundombinu hiyo muhimu.

Chunya. Baada ya kusubiri zaidi ya miaka 60 tangu nchi ipate uhuru, hatimaye wananchi wa Kijiji cha Kibaoni A na B, Kata ya Chokaa, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, wameanza kuona mwanga wa matumaini baada ya Serikali kuanza kufungua barabara zilizokuwa hazipitiki.

Hata hivyo, wananchi hao pamoja na madereva wa bodaboda wameiomba Serikali kujenga mitaro na vivuko katika maeneo korofi ili kudhibiti mmomonyoko utakaotokana na mvua nyingi na kusababisha kukatika kwa mawasiliano.

Wamesema mbali na kufungua barabara hizo, kuna maeneo yenye makorongo ambayo wakati wa msimu wa mvua hujaa maji na kusababisha mawasiliano kukatika, hali inayozuia usafirishaji wa abiria kutoka sehemu moja kwenda nyingine, hususan wagonjwa na wanafunzi kushindwa kwenda mashuleni.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi, Julai 16, 2026, dereva wa bodaboda wa Kijiwe cha Chokaa, Bahati Mwile, amesema kwa mara ya kwanza tangu nchi ipate uhuru eneo hilo linaanza kupata barabara zinazoweza kupitika.

Kibao kinachoonyesha barabara ya kwenda Kijiji cha Simbilimwaya Wilaya ya Chunya ambayo Serikali imefungua ili kuchochea shughuli za kiuchumi. Picha na Hawa Mathias.

"Tunamshukuru Serikali kwa kuanza kufungua barabara hizi. Kwa miaka mingi tulikuwa tunapata shida kubwa, hasa wagonjwa na wajawazito waliokuwa wakipelekwa hospitalini. Kilichobaki sasa ni kujenga mitaro na vivuko ili barabara hizi zidumu hata kipindi cha mvua," amesema.

Amesema awali, kutokana na changamoto ya miundombinu, walilazimika kuwatoza abiria nauli kati ya Sh3,000 na Sh4,000 kwa safari za jirani, lakini maeneo ya mbali kati ya Sh10,000 na Sh20,000.

"Tunaamini barabara hizi zikiboreshwa kwa kiwango kizuri, sambamba na ujenzi wa vivuko na mitaro, gharama za usafiri zitashuka na wananchi wengi watanufaika, hususan wenye kipato cha chini," amesema.

Naye dereva wa bodaboda, Abdul Abdul wa Kijiwe cha Saganoti, amesema licha ya kufunguliwa kwa miundombinu hiyo bado kuna changamoto ya makorongo, ambayo ni kikwazo kikubwa wakati wa mvua. Endapo hayatazibwa mapema, kuna athari kubwa.

"Kata yetu imechelewa sana kupata barabara. Tunaiomba Serikali iweke nguvu katika ujenzi wa vivuko na mitaro ili wananchi wasipate changamoto ya kukatika kwa mawasiliano msimu wa mvua ukifika," amesema.

Mkazi wa Kijiji cha Chokaa, Kitongoji cha Simbilimwaya, Thomas Emmanuel, amesema awali ubovu wa barabara ulihatarisha maisha ya wagonjwa, hususan wajawazito, huku usafiri pekee ukiwa ni bodaboda.

"Kabla ya barabara hii kuchongwa tulikuwa tunatumia saa mbili hadi tatu kutembea kutoka Kijiji cha Mnazi Mmoja kwenda Simbilimwaya. Sasa tunatumia usafiri wa pikipiki kwa takribani saa moja kufika barabara kuu," amesema.

Diwani wa Kata ya Chokaa, Joshua Mwambalala, amesema kutokana na jiografia ya Wilaya ya Chunya, changamoto ya miundombinu imekuwa ikikwamisha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi.

Amesema katika kata yake kuna vitongoji 19, kati ya hivyo vitongoji vinne pekee vimefunguliwa miundombinu ya barabara, huku vitongoji 14 vikibaki na kuwekewa mikakati ya kufikiwa.

Ametaja vitongoji vilivyofunguliwa kuwa ni Kibaoni A, Kibaoni B, Simbilimwaya na Mnyolina, huku juhudi zikiendelea kufikia vitongoji vingine sambamba na kuomba Serikali kujenga vivuko na mifereji katika barabara.

"Kijiji cha Simbilimwaya awali kilitegemea shughuli za uchimbaji madini, lakini Serikali imesogeza huduma ikiwemo shule ya msingi na zahanati kutokana na ongezeko la wananchi," amesema.

Kaimu Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Simbilimwaya, Yusto Mathew, amesema kufunguliwa kwa barabara kutarahisisha wanafunzi kutoka vijiji vya Maili Tano na Mnazi Mmoja kufika shuleni na kupunguza utoro.

"Walikuwa wanatumia njia zinazopita porini na hazikuwa salama kwa watoto. Barabara hii itaongeza usalama na kuwafanya wafike shuleni kwa wakati," amesema.

Madereva bodaboda Kijiji cha Kibaoni "A" na "B" Kata ya Chokaa wakindelea na shughuli za usafirishaji baada ya Serikali kufungua miundombinu ya barabara zilizokuwa changamoto tangu nchi ipate uhuru. Picha na Hawa Mathias.


Historia ya Kijiji cha Simbilimwaya

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Simbilimwaya, Morris Mathias, amesema tangu kitongoji hicho kianzishwe mwaka 1995 hakijawahi kuwa na barabara, bali njia za miguu.

Amesema kilianzishwa baada ya kugunduliwa kwa shughuli za uchimbaji wa dhahabu ambapo mwaka 2000 wananchi walilazimika kuchimba njia kwa kutumia koleo na sururu ili waweze kupita.

"Sasa tunaomba Serikali ngazi ya wilaya kuboresha zaidi barabara, vivuko na mifereji ili kuwezesha kufikiwa na mabasi ya abiria, hivyo wananchi waweze kusafirisha mazao na kufanya shughuli za kiuchumi kwa urahisi," amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa Tarura Wilaya ya Chunya, Emmanuel Kayora, amesema barabara za mitaa zinasimamiwa na halmashauri, huku Tarura ikitenga Sh2.3 bilioni kuboresha miundombinu iliyoharibiwa na mvua.

Miongoni mwa miundombinu hiyo ni madaraja ya Chalangwa, Karungu na Mto Shinjilili yaliyoharibiwa na mvua za msimu uliopita.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Athuman Bamba, amesema halmashauri itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara baada ya kununua mtambo, hatua itakayorahisisha usafirishaji wa mazao na upatikanaji wa huduma za kijamii kwa urahisi.