Ripoti ya CAG yabaini magari 547 ya Serikali hayatumiki

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere
Muktasari:
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amebaini takribani magari mabovu 547 ya Serikali yalikuwa yamehifadhiwa na hayatumiki katika taasisi zilizotembelewa.
Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amebaini takribani magari mabovu 547 ya Serikali yalikuwa yamehifadhiwa na hayatumiki katika taasisi zilizotembelewa.
CAG Kichere amebaini hayo katika ripoti zake za ukaguzi kwa mwaka 2021/22 alizoziwasilisha Bungeni jijini Dodoma jana Alhamisi, Aprili 6, 2023.
“Idadi kubwa ya magari mabovu ambayo yamehifadhiwa na hayatumiki ilikuwa katika Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) iliyokuwa na magari 176 ikifuatiwa na Kampuni ya Simu Tanzania iliyokuwa na magari 86.
Taasisi nyingine ni Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) magari 19, Wizara ya Fedha na Mipango (51), Wizara ya Mambo ya Nje (39), Wizara ya Afya (14), Wakala wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) magari 44.
Nyingine ni Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) magari 37, Halmashauri ya Jiji la Tanga (18), Halmashauri ya Wilaya ya Meatu (15), Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro (13), Halmasahuru ya Wilaya ya Mpwapwa (12) na Mahakama ya Tanzania magari 23.
Sababu ya kutotumika magari hayo imetajwa kuwa ni pamoja na kupata ajali, kutofanyiwa matengenezo, kuegeshwa, na kusubiri vibali vya uondoshwaji.
“Sababu nyingine ni pamoja na tathmini duni ya magari yanayotakiwa kuondoshwa, kukosekana kwa uwazi wa magari yaliyoondoshwa mapema kwa watumishi, na usajili duni wa magari ya Serikali katika Mfumo wa Taarifa wa Usimamizi wa Mali za Serikali.”
Pia, imebainika kuwa magari yaliyopo Temesa na vituo vingine vya serikali yalihusishwa na uhakiki na ukaguzi hafifu wa kipindi kirefu cha magari unaofanywa na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mali za Serikali (DGAM).