Ripoti: Pombe huua watu milioni 2.6 kila mwaka duniani

Muktasari:
- Pombe imetajwa kusababisha vifo vya mamilioni ya watu duniani huku wengi wao wakiwa ni wanaume
Geneva, Uswisi. Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema pombe huua watu watu milioni 2.6 kila mwaka ulimwenguni kote.
Ripoti ya utafiti ya shirika hilo uliofanyika mwaka 2019 inasema pombe imechangia asilimia 4.7 ya vifo vyote duniani mwaka huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na Shirika la Habari la AFP leo Juni 25, 2024 ikiinukuu WHO, karibu robo tatu ya vifo hivyo ni vya wanaume.
Idadi kubwa zaidi ya vifo vilivyotokana na pombe mwaka huo wa 2019, asilimia 13 walikuwa watu wenye umri wa miaka 20 hadi 39.
Imeelezwa pombe husababisha kifo kimoja kati ya watu 20 duniani kote kila mwaka, kutokana na wahusika kuendesha gari huku wakiwa wamelewa, unyanyasaji unaosababishwa na pombe na utiriri wa magonjwa.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Ghebreyesus amesema kumepungua matumizi ya pombe na madhara yanayohusiana nayo tangu 2010.
Unywaji wa pombe kupita kiasi pia huwafanya watu kuathirika zaidi na magonjwa ya kuambukiza kama vile kifua kikuu, VVU na nimonia.
Inakadiriwa kuwa watu milioni 209 waliishi na utegemezi wa pombe katika mwaka 2019 sawa na asilimia 3.7 ya idadi ya watu wote ulimwenguni.
Vilevile katika ripoti hiyo imeeleza kati ya vifo vyote vilivyosababishwa mwaka huo, takriban milioni 1.6 vilitokana na magonjwa yasiyoambukiza.
“Kati ya vifo hivyo, 474,000 vilitokana na magonjwa ya moyo na mishipa, 401,000 saratani na 724,000 kutokana na majeraha yaliyotokana na ajali za barabarani na kujidhuru.”
Ripoti hiyo inasema Ulaya imechangia kwa kiwango kikubwa zaidi cha unywaji ikiwa ni kwa lita 9.2, ikifuatiwa na Amerika lita 7.5.