Watu 56 wafa kwa kunywa pombe yenye sumu India

Baadhi ya waombolezaji wakiaga miili ya waliofariki dunia kutokana na kunywa pombe yenye sumu. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Taarifa zinasema pombe hiyo iliyotengenezwa kienyeji iliwekwa methanol yenye sumu
India. Watu 56 wamepoteza maisha kwa kunywa pombe haramu inayoaminika kuwa na sumu katika Jimbo la Kusini mwa India la Tamil Nadu.
Taarifa zinasema pombe hiyo iliyotengenezwa kienyeji iliwekwa methanol yenye sumu na kuwaua watu 37 ndani ya saa chache baada ya kuinywa Jumanne huku madhara yakiendelea kutokea hadi leo.
Tovuti ya The Hindu imesema idadi ya waliofariki katika mkasa huo imeongezeka hadi 56, baada ya mtu mmoja kupoteza maisha leo Jumapili, Juni 23, 2024.
Hadi sasa, watu 31 wamefariki katika Chuo cha Serikali cha Kallakurichi Medical College, 18 katika Chuo cha Serikali cha Mohan Kumaramangalam Medical College na Hospitali ya Salem huku wanne katika Chuo cha Serikali cha Villupuram Medical College na Hospitali.
Pia, watatu katika Taasisi ya Jawaharlal ya Elimu ya Tiba na Utafiti wa Uzamili (JIPMER) huko Puducherry, aidha jumla ya watu 159 ikiwa ni pamoja na wanawake saba wanaendelea na matibabu hospitalini.
“Polisi wa CB-CID wamemkamata mchuuzi Govindaraj, maarufu Kannukutty na mkewe Vijaya na ndugu wengine Damodaran, Chinnadurai, wanaotuhumiwa kusambaza pombe hiyo,” inaeleza tovuti hiyo.
Hata hivyo, vifo vinavyotokana na pombe zenye sumu zinazozalishwa kinyume cha sheria, mara nyingi hutokea nchini India, huku ikielezwa ni watu wachache wanaoweza kumudu pombe rasmi zenye chapa.
Ili kuongeza uwezo wake, pombe hiyo ya kienyeji mara nyingi hutiwa methanoli inayoweza kusababisha upofu, uharibifu wa ini na kifo.
Gazeti la Indian Express leo Jumapili limemnukuu diwani wa eneo hilo, Palraj akielezea jinsi vibarua masikini wakinunua mara kwa mara pombe hiyo kwenye mifuko ya plastiki waliyokunywa kabla ya kazi.
Pia, taarifa iliyochapishwa na Shirika la Habari la AFP inasema zaidi ya watu 200 walikuwa wakitapika, kuumwa matumbo na kuhara tangu Jumatano, hata hivyo maofisa wanaochunguza tukio hilo wamewakamata watu kadhaa hadi sasa.