RC Chalamila apiga 'biti' mgomo Kariakoo

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila wakati akizungumza na wafanyabishara wa sokola Kariakoo leo Jumatatu Juni 24, 2024.
Muktasari:
- Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo awahakikishia ulinzi watakaoendelea na bishara.
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema wafanyabishara waliofungua maduka yao leo Jumatatu Juni 24, 2024, licha ya kuwepo kwa mgomo wa baadhi ya wafanyabishara, atalinda biashara zao na hawatafanyiwa vurugu.
RC Chalamila amesema atakayejaribu kuwafanyia vurugu wafanyabiashara waliofunga maduka yao, atashughulika naye.
“Nataka niwathibitishie yule atakayemletea mkwara aliyekubali kufungua, naapa mbele ya Mwenyezi Mungu, hapo ndipo nitakapoonyesha ‘show’ nzima. Kwa sababu mtu anakubali kufungua na wewe unamchimba mkwara, mimi ntakuchimba mkwara na hautainuka tena,” amesema.
Aidha, Chalamila amesema kero zilizopelekwa na wafanyabishara hao serikalini zinaendelea kushughulikiwa.
DC Ilala awahakikishia ulinzi
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema wataendelea kuimarisha ulinzi wa mali na watu katika eneo la Karikoo.
Amesema wakati wafanyabiashara wengine wakizungumzia mgomo, wapo wafanyabiashara waliokwenda ofisini kwao kusema wanafanya biashara zao kwa mikopo, hivyo uwepo wa mgomo utawaathiri.
“Nikuhakikishie waliofungua tutawalinda, ili wafanye shughuli zao kwa amani,” amesema Mpogolo.
Akizungumza wakati akimkaribisha Chalamila kuzungumza na wafanyabiashara waliofunga biashara zao, Mpogolo amesema katika maelezo yao, baadhi ya wafanyabiashara walisema wamepanga na wenye jengo wanataka kodi, hivyo kufunga maduka kutawaondolea uwezo wa kulipa kodi.
“Baadhi ya wamiliki wa majengo nao na wanaojenga walisema wamejenga kwa mikopo, ili waweze kurejesha lazima waliopanga wapate nafasi ya kufanya biashara na kulipa kodi,” amesema Mpogolo.
Pia amesema wanafahamu uwepo wa wafanyabiashara wanaosaidiwa na Serikali, lakini wamekuwa wakiwazunguka na kuwatisha.
Wafanyabiashara hao wamegoma kuishinikiza Serikali kutatua changamoto zinazowakabili, ikiwemo kamatakamata inayofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mgomo huo umeibuka, baada ya Jumamosi Juni 22, 2024 kusambaa vipeperushi kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuwepo kwa mgomo huo utakaoanza leo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Karikaoo, Martin Mbwana akizungumza na Mwananchi Juni 22, 2024 alikiri kuona vipeperushi hivyo, akieleza hiyo ni hasira za kuchoshwa na wanayofanyiwa na TRA.