Rais Samia: Wanawake vunjeni vikwazo, chukueni nafasi za uongozi

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wanawake nchini kuondoa hofu na kuvunja vikwazo vinavyowazuia kushiriki kikamilifu katika siasa, uchumi na uongozi, akisisitiza kuwa maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana bila ushiriki madhubuti wa wanawake.
Akizungumza katika mahafali ya 10 ya programu ya kuwaendeleza wanawake inayoendeshwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema wanawake wanapaswa kushirikiana, kusaidiana na kuthibitisha uwezo wao wa kufanya maamuzi makubwa yanayogusa jamii na maendeleo ya nchi.
"Wanawake tusibaki nyuma. Ni wakati wa kuamka, kuondoa hofu na kushiriki kikamilifu katika kufanya maamuzi. Tushikamane na kusaidiana ili tuwe sehemu ya mabadiliko tunayoyataka," amesema Rais Samia.
Amesisitiza kuwa wanawake wanapaswa kutambua thamani yao na kuwa tayari kupambana na changamoto zinazokwamisha ushiriki wao katika siasa, biashara na nafasi za maamuzi.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Benki ya Stanbic Tanzania, Violet Mordichai, aliangazia umuhimu wa wanawake kuwa na mipango madhubuti ya kuwawezesha kiuchumi na kuchukua hatua za kuimarisha nafasi zao katika biashara na ajira.
"Uongozi si kusubiri nafasi, bali ni kuzitengeneza. Wanawake wanapaswa kuwa na uthubutu wa kusimamia biashara na kazi zao kwa ufanisi, huku wakitumia fursa zilizopo kwa maendeleo yao na jamii kwa ujumla," amesema Mordichai alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika hafla hiyo.
Mahafali hayo yaliwaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya ajira na maendeleo, wakijadili changamoto na fursa zinazowakabili wanawake katika uongozi na uchumi. Katika miaka ya hivi karibuni, Serikali imekuwa ikihamasisha ushiriki wa wanawake katika nyanja mbalimbali za maendeleo, huku Rais Samia akiongoza juhudi hizo kwa mifano ya vitendo kupitia uteuzi wa wanawake katika nafasi nyeti za uongozi serikalini na sekta binafsi.
Wadau walihimiza wanawake kutumia elimu, maarifa na mitandao ya kijamii kama nyenzo za kuwainua kiuchumi na kijamii, ili kuhakikisha ushiriki wao unakuwa na mchango wenye tija kwa taifa.