Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Charles Hillary afariki, Rais Samia, wadau wamlilia

Muktasari:

  • Tanzania imempoteza nguli wa utangazaji, Charles Hilary aliyefariki dunia asubuhi ya leo Jumapili. Wadau mbalimbali wamemzungumzia jinsi walivyomfahamu.

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Ikulu ya Zanzibar na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Charles Hilary amefariki dunia alfajiri ya leo Jumapili Mei 11, 2025 jijini Dar es Salaam.

Charles pia aliwahi kuwa mtumishi mwandamizi wa kituo cha Azam Media Limited kati ya mwaka 2015 na 2023. Alihitimisha muda wake akiwa Mkuu wa Idara ya Redio ya UFM, baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Ikulu ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa ndugu wa karibu, Hilary amefariki baada ya kuugua ghafla na mauti yamemkuta akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tawi la Mloganzila.

Hilary pia amewahi kuvitumikia vituo mbalimbali vya habari ikiwemo Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) wakati huo likiitwa Redio Tanzania na Shirika la Utangazaji wa Uingereza (BBC) na DW Idhaa ya Kiswahili.

Katibu Mkuu Kiongozi wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Zena Ahmed Said amesema Hilary amefariki dunia leo Jumapili katika Hospitali ya Mlonganzila, Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

“Marehemu Charles Hilary atakumbukwa kwa uzalendo wake, uadilifu na mchango mkubwa alioutoa katika kusimamia mawasiliano ya Serikali kwa weledi na ufanisi mkubwa,” amesema Zena kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Regey Mohamed, Naibu Mkurugenzi, Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zanzibar.


Samia amlilia

Katika salamu zake, Rais Samia Suluhu Hassan amesema amepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Charles Hilary.

“Ninatoa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk Hussein Mwinyi, familia, ndugu, jamaa na marafiki na wadau wote wa sekta ya habari nchini kwa msiba huu.”

“Ndugu Charles Hilary atakumbukwa kwa mchango wake adhimu wa zaidi ya miaka 40 katika kukuza sekta ya habari nchini, tangu akiwa redioni hadi kwenye televisheni, pamoja na unasihi kwa wanahabari wachanga.”

Rais Samia amesema: “Namuomba Mwenyezi Mungu aijaalie familia yake uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu, na ailaze roho ya mpendwa wetu mahala pema. Hakika sote ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake tutarejea.”

Katika kurasa zake za mitandao  ya kijamii, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa ameandika: “Bwana Mkwanga WHY? Nimeumia sana na kifo cha Charles Martin Hilary Mkwanga (Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) kilichotokea leo.”

“Tumempoteza Mwandishi wa habari na mtangazaji mbobezi aliyejaa maarifa, umahiri, ubunifu, uchapakazi, uadilifu, nidhamu na aliyezingatia maadili ya kitaaluma kwa viwango vya juu.”

Msigwa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema: “Tumempoteza Mwalimu aliyependa usahihi wa mambo kuanzia kwenye taaluma yake ya uandishi wa habari na utangazaji, lugha ya Kiswahili, mtindo wa maisha na uongozi.”

“Tumempoteza binadamu aliyejaa upendo, ucheshi, ushirikiano na aliyejaa tabasamu lililosindikizwa sauti yenye viwango vya juu vya utangazaji. Lala salama Charles Hilary, Bwana Mkwanga, Mzee wa Charanga, mtangazaji mahiri wa Kandanda, Mwalimu wa Kiswahili, Mwana Mambomseto, Babu, Baba na Kaka.”

Amemalizia kwa kusema: “Poleni sana wanafamilia, pole Mheshimiwa Rais Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk Hussein Ali Mwinyi, Azam Media, BBC, IPP Media, TBC na wote mlioguswa na kifo cha Charles.”

Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Togolani Mavura yeye ameandika kwenye ukurasa wake wa X akisema: “Kwetu tulioanza fuatilia mpira miaka ya themanini na tisini wakati ambapo kumiliki luninga ilikuwa ni alama ya anasa na utajiri.

“Hayati Charles Hillary kwa sauti yake na ugani wake wa kipekee aliweza kutufanya tuutazame na tuuone mpira kupitia spika za redio bila kuona tofauti yoyote na kutokuwepo uwanjani ama kutazama luningani.”

“Kaka Charles Hillary ametimiza ujumbe wake kwa kuishi na kufikia kikomo cha juu cha kipawa chake na tasnia ya habari nchini. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mpendwa wetu Charles Hillary mahala pema, peponi,” amesema.

Mtangazaji maarufu nchini, Maulid Kitenge ameandika kwenye ukurasa wake wa X: “Nimepokea kwa mshtuko sana taarifa za kifo cha Mwalimu wangu Charles Martin Hillary Nkwanga. Nkwanga alinipokea na kunifundisha kazi akiwa bosi wangu wakati akiwa Mkurugenzi wa Radio One mwaka 1999.”

“Na aliendelea kunifundisha kazi hii hata alipoondoka Redio One na kwenda DW Ujerumani na BBC ambapo mara kadhaa nilikuwa nakwenda huko. Nkwanga moja ya ‘style’ yake ya ufundishaji kazi ilikuwa lazima ujue kazi hiyo maana alikuwa anakukosoa bila ya kukuonea haya halafu akijua umenuna kwa kukukosoa anakuchekesha kidogo.”

Kitenge amesema: “Ni mtu wa aina yake kuwahi kukutana naye hapa ulimwenguni. Kipaji cha hali ya juu cha utangazaji aliyejua lafudhi nzuri ya Kiswahili. Ukimuweka katika Kutangaza mpira yumo ukimuweka katika kutangaza habari,  kitu ambacho aliwahi kuniambia anakipenda mno na kuenjoy pia yumo.”

“Nkwanga ameondoka duniani akiwa anaipenda mno kazi ya utangazaji kuliko kitu chochote ulimwenguni. Hakika tumempoteza gwiji haswa la utangazaji, machozi yananitiririka wakati naandika haya. Pumzika kwa amani Nkwanga umeacha vijana uliotupika kisawasawa kwenye kazi hii na hakika hatutakuangusha. This is shocking loss. Rest in peace, Mzee wa Macharanga.”