Rais Samia kukutanisha wataalamu mapambano ya ufisadi

Muktasari:
Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza mkutano wa mwaka wa kuhamasisha mapambano dhidi ya ufisadi, rushwa utakao kutanisha wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi.
Dar es Salaam. Chama cha Wataalamu wa udhibiti wa ufisadi, rushwa na ubadhirifu (ACFE), kimesema kimemwalika Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi kwenye mkutano wake wa mwaka utakaokutanisha wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi.
Mkutano huo utakao kuwa na mada kuu ya Kukuza Utawala Bora na mapambano dhidi ya ufisadi na rushwa utafanyika kuanza Novemba 14 hadi 18 Mwaka huu, mkoani Arusha.
Akizungumza Dar es Salaam leo, Novemba 10, Mkurugenzi Mtendaji wa ACFE, Musomi Maira amesema maandalizi yameshakamilika na kwamba mkutano huo pia unalenga kukutanisha wataalamu tofauti ili kupeana mbinu mpya za kukabiliana hali hiyo.
"Repoti yetu inaonesha kuwa taasisi hupoteza asilimia 5 ya mapato yake kutokana na vitendo vya ufisadi, rushwa na ubadhirifu na ukiachilia mbali ripoti yetu hata ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) imeendelea kuonesha vitendo hivyo," amesema Maira
Maira amesema kuwapa mbinu wataalamu hao kutasaidia kubaini na kuzuia viashiria vinavyoweza kusababisha vitendo hivyo kutendelea kutawala hususan kwenye taasisi za umma.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti, Mafunzo na Ubunifu (ENTAF), Dk Hadija Kweka amebainisha kuwa kutokana na kuongeza kwa vitendo vya rushwa nchini ni wazi Serikali inapaswa kushirikiana na wadau katika kuzuia.
"Taifa limekuwa likilia baada ya kutokea matokeo ya vitendo hivyo sasa taasisi binafsi zinapojitokeza kwa nia ya kutoa elimu na mafunzo namna ya kuzuia ni vizuri kuungana nao," amesema
Mbali na Rais Samia, mkutano huo utakuwa na watendaji wa Serikali akiwemo, Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu na Mdhibiti na Mkaguzi was Hesabu za Serikali CAG, Charles Kichere.