Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia kukutana na Putin, kuimarisha ushirikiano Tanzania na Russia

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama wakati akipokea heshima ya wimbo wa Taifa mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Vnukovo, Jijini Moscow, jana Juni 2, 2026 kwa ajili ya ziara ya Kitaifa nchini Urusi.

Muktasari:

  • Rais Samia aliwasili mjini Moscow usiku wa kuamkia jana Jumanne Juni 2, 2026 kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu nchini Russia kufuatia mwaliko wa Rais Putin.

Moscow, Russia. Rais Samia Suluhu Hassan anakutana na kufanya mazungumzo rasmi wa pande mbili na Rais wa Russia, Vladimir Putin katika Ikulu ya Kremlin leo Jumatano Juni 3, 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi mataifa hayo mawili.

Rais Samia aliwasili mjini Moscow usiku wa kuamkia jana Jumanne Juni 2, 2026 kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu nchini Urusi kufuatia mwaliko wa Rais Putin.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Bakari Machumu, viongozi hao wawili watafanya mazungumzo rasmi kabla ya kutoa taarifa ya pamoja kwa vyombo vya habari.

“Rais anatarajiwa kufanya mazungumzo rasmi ya pande mbili na Rais wa Shirikisho la Russia, Vladimir Vladimirovich Putin. Baada ya mazungumzo hayo, viongozi hao watatoa taarifa ya pamoja kwa vyombo vya habari,” imeeleza taarifa hiyo.

Akiwa Moscow, Rais Samia pia anatarajiwa kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari (Honoris Causa) na Chuo Kikuu cha Peoples’ Friendship University of Russia (RUDN University).

Katika juhudi za kuvutia uwekezaji na kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Rais Samia atashiriki kikao cha majadiliano ya viongozi katika Kongamano la 29 la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF 2026).

Ujumbe wa Tanzania unaoongozwa na Rais Samia, unawajumuisha pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Kanda Maalum za Kiuchumi Tanzania (Tiseza), Gilead Teri.

Kupitia kongamano hilo, Tanzania inatarajiwa kutumia fursa hiyo kuonesha vivutio vya uwekezaji na biashara kwa watunga sera, wawekezaji na viongozi wa biashara kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Masuala ya uwekezaji na biashara pia yanatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya ajenda wakati Rais Samia atakaposhiriki Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Russia, litakalowakutanisha wafanyabiashara kutoka nchi hizo mbili.

Ziara hiyo inafanyika wakati kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Russia kikiwa bado chini ikilinganishwa na fursa zilizopo.

Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, mauzo ya bidhaa za Tanzania kwenda Russia yameongezeka kutoka Dola 7.5 milioni za Marekani (Sh19.5 bilioni)  mwaka 2020 hadi kufikia Dola 29.5 milioni (Sh76.7 bilioni) mwaka 2025.

Aidha, thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili imeongezeka kutoka Dola 178.8 milioni (Sh464.9 bilioni)mwaka 2020 hadi kufikia takribani Dola 307.5 milioni (Sh799.5 bilioni) mwaka 2025.

Tangu mwaka 1997, wawekezaji kutoka Russia wamewekeza katika miradi 70 nchini Tanzania yenye thamani ya uwekezaji wa moja kwa moja inayokadiriwa kufikia Dola 434.22 milioni (Sh1.13 trilioni), huku miradi hiyo ikizalisha ajira zipatazo 3,018.

Miongoni mwa bidhaa kuu zinazouzwa na Tanzania kwenda Russia ni chai nyeusi, tumbaku, nazi, korosho, maua ya waridi, ngozi, bidhaa za mapambo za mbao, madini ya risasi pamoja na mawe ya quartzite.

Kwa upande mwingine, Tanzania huagiza kutoka Russia karatasi za magazeti, nitrati ya amonia, bidhaa za chuma zilizochakatwa nusu, mbolea, ngano ngumu, aloi za alumini, maji ya madini, bidhaa za karatasi, aloi za zinki, salfa, mafuta ya petroli na malighafi mbalimbali za viwandani.

Uwekezaji mkubwa zaidi wa Russia nchini Tanzania ni Mradi wa Uranium wa Mkuju River wenye thamani ya dola 1.2 bilioni (Sh3.12 trilioni), unaotekelezwa katika Mkoa wa Ruvuma na Kampuni ya Mantra Tanzania Ltd, ambayo ni tanzu ya Shirika la Nishati ya Nyuklia la Russia (Rosatom).

Rosatom ni shirika la serikali la Russia linalojihusisha na uzalishaji wa nishati ya nyuklia, bidhaa zisizo za nyuklia pamoja na teknolojia za hali ya juu.