Rais Samia kugharamia watoto 20 upandikizaji uloto

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu
Muktasari:
- Gharama za upandikizaji wa uloto kwa wagonjwa wa selimundu zinatajwa kuwa kati ya Sh50 milioni kwa mgonjwa mmoja nchini wakati nje ya nchi matibabu hayo ni Sh120 milioni hadi 150 milioni.
Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan atagharamia matibabu ya kupandikiza uloto kwa watoto 20 wenye ugonjwa wa sikoseli katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa (BMH).
Mei 10 mwaka huu Hospitali ya BMH ilianza kutoa hudumaya kupandikiza uloto ambapo watoto watatu waishio na ugonjwa wa Sikoseli walipandikiziwa huduma hiyo.
BMH ni hospitali ya pili nchini kutoa huduma hiyo muhimu baada ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambayo yenyewe ilianza kutoa huduma hiyo rasmi mwaka 2021.
Gharama za upandikizaji wa uloto kwa wagonjwa wa selimundu zinatajwa kuwa kati ya Sh50 milioni kwa mgonjwa mmoja nchini wakati nje ya nchi matibabu hayo ni Sh120 hadi 150 milioni.
Matibabu ya uloto huhusisha uvunaji, uchakataji na upandikizaji wa chembe chembe hai mama za damu.
Akizungumza leo Jumatatu, Juni 19, 2023 jijini hapa katika maadhimisho ya Siku ya Sikoseli Duniani, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Rais ameahidi atagharamia watoto 20 wenye ugonjwa sikoseli kutokana na gharama za kuwa juu.
“Rais atagharamia kupandikiza uloto kwa watoto wenye sikoseli 20 kwa hiyo wataalamu wetu kazi kwenu. Kwa mwaka huu wazazi walezi ambao mnawatoto nimetoa changamoto kwa Benjamin Mkapa wapandikize watoto 20 ambao watadhaminiwa kwa asilimia 100 na Rais Samia Suluhu Hassan, hakutakuwa na kuchangia,”amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia wizara hiyo zaidi ya Sh5 bilioni kwa ajili ya huduma za ubingwa bobezi ikiwemo kupandikiza uroto.
Hata hivyo amewataka wazazi na walezi wenye watoto wenye ugonjwa wa sikoseli kuwapeleka kliniki wakafanyiwe uchunguzi kwani Serikali inataka kuona watoto wenye ugonjwa huo wanaishi bila kupata maambukizi ya bakteria, hawapungukiwi damu na maumivu ya mifupa.
Amesema Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuhakikisha huduma za upandikizaji uloto zinapatikana kwa watoto wengi.
“Kwa hiyo ninachoweza kusema wazazi nendeni kwenye kliniki za hospitali zetu za rufaa za mikoa na unaweza ukaanza katika kituo cha afya kama Makole (Dodoma) wao watakuunganisha na Benjamin Mkapa,”amesema Waziri Ummy.