Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia: Bima ya afya sasa haiepukiki

Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi pamoja na wananchi mara baada ya kufungua Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Mjini Magharibi iliyopo Lumumba Zanzibar leo Januari 10, 2024.

Muktasari:

  •  Baada ya Bunge kupitisha Sheria ya bima ya afya na Rais Samia kuisaini, kumekuwa na mjadala mpana kuhusu namna bima hiyo itakavyofanya kazi, hata hivyo, Rais Samia amesisitiza kwamba suala la bima haliepukiki hapa nchini.

Unguja. Rais Samia Suluhu Hassan amesema suala la kuwa na bima ya afya kwa sasa haliepukiki kwa sababu linalenga kuwawezesha wananchi kupata huduma bora, badala ya kuendelea kusubiri kupata matibabu bure.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Januari 10, 2024 wakati akifungua Hospitali ya Mkoa ya Lumumba, Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo amesema licha ya kuwa moja ya malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar ilikuwa ni kutoa huduma za matibabu bure, lakini kwa sasa ni vema wakachangia huduma hiyo.

Novemba 2, 2023, Bunge lilipitisha muswada wa sheria ya bima ya afya kwa wote na kuwa sheria kamili. Baada ya mwezi mmoja, Bunge kupitisha sheria hiyo, Rais Samia alisaini na kuwa sheria kamili.

Hata hivyo, kabla ya sheria hiyo kupitishwa rasmi bungeni, iliibua maoni tofauti wengine wakisema wapo wasiokuwa na uwezo kulipia bima hiyo.

Kamati ya kudumu ya Bunge ya afya na masuala ya Ukimwi iliweka msisitizo wa umuhimu wa kuwa na mfuko kwa ajili ya kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo,  na Serikali iusimamie kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya.

“Ndugu zangu, pamoja na shabaha ya Mapinduzi ilikuwa ni kutoa tiba bure kwa wanachi, tumetoka mbali, sasa ni miaka 60 tumekwenda mbele mno kuliko tulipokuwa, kule hakukuwa na mwananchi mwenye uwezo wa kuwa na bima ya afya na tumefaidi kwa muda mrefu lakini tulipofikia ili tuweze kutoa huduma endelevu, bima ya afya haiepukiki,” amesema.

Hata hivyo, Rais Samia amesema jambo hilo anaiachia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuangalia sera na mipango yao “lakini kwangu mimi natanguliza kusema kwamba suala la bima ya afya haliepukiki.

Amesema wapo watakaosema kwamba hiyo sio dhamira ya Mapinduzi watu kuchangia huduma za afya, “sasa tuchague, tuchangie huduma za afya au tufe na hapa tulipofika na huduma za afya ziende chini.

Mkuu huyo wa nchi amesema kwa maoni yake kila mmoja ajipange kwa bima yake ili atibiwe vile ipasavyo.

Rais Samia amesema zinatumika gharama kubwa za miundombinu ya huduma za afya, hivyo wasipochangia itasababisha huduma hizo kurudi nyuma.

Amesema ili matibabu yaendelee ni gharama kubwa na kuiachia Serikali ibebe mzigo wote sio rahisi “tumejenga miundombinu mizuri vifaa vya kisasa lakini tusipochangia huduma zitarudi nyuma itakuwa kazi tuliyoifanya ni bure.

Magonjwa yasiyoambukiza

Kiongozi huyo wa nchi, pia alizungumzia kuhusu ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kwamba sio taswira nzuri katika sekta ya afya.

Amesema vifo vya magonjwa hayo vimeongezeka kwa asilimia 14 kutoka milioni 2.6 mwaka 2019 hadi kufikia milioni 3.1 mwaka 2023.

Amesema magonjwa hayo yanachangia asilimia 33 ya vifo vyote “hii ina maana kwamba kwa watu watatu mmoja ana ugonjwa usioambukiza ama kisukari, uzito kupitiliza na mengine kama hayo.

Amewataka wananchi kila mmoja kwa nafasi yake kuzingatia ushauri wa wataalamu kufanya mazoezi na kula vyakula vinavyozingatia mlo kamili kuepuka maradhi hayo.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amewataka wananchi kutunza miundombinu ya hospitali hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu, huku akiwataka watoa huduma kutoa huduma bora.

“Kuwa na majengo ni jambo moja lakini huduma inayotolewa ndani ni jambo lingine, kwa hiyo ndugu zangu tuzingatie hili na Wizara ya Afya hakikisha mnalisimamia,” amesema Rais Samia.

Kwa upande wa Waziri wa Afya wa Zanzibar, Ahmed Mazrui amesema kutokana na uboreshaji wa afya, kwa sasa kuna vitanda 2,645 kutoka vitanda 1,445 vya awali. 

Amesema kulikuwa na chumba kimoja cha wagonjwa mahututi (ICU) chenye vitanda vinane, sasa kuna ICU 14 zenye vitanda 80, kilikuwa na vyumba vya upasuaji 11, kwa sasa vipo 35 na kutoka cha dharura kimoja kufikia 13.

“Hii ni hospitali ya hadhi kubwa ikiwa na ICU nne, tulikuwa tunatumia gharama kubwa kupeleka wagonjwa nje sasa itapungua,” amesema Mazrui.

Amesema wakati Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja inayotegemewa kuvunjwa mwaka huu kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati mkubwa, hiyo ya Lumumba ndio itakuwa mbadala wake.

Naye Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Dk Amour Suleiman Mohamed amesema hospitali hiyo imegharimu Sh32.5 bilioni ikijumuisha vifaa na ununuzi wa magari mawili ya wagonjwa.

Amesema itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 893,000 kutoka shehia 121 na kulaza wagonjwa 220 kwa wakati mmoja.

“Itatoa huduma za kibingwa, uchunguzi maradhi tofauti, wagonjwa wa ndani, wajawazito, wodi ya wagonjwa wenye mahitaji maalumu na vyumba vinne vya wagonjwa mahututi," amesema.

Wananchi wafunguka 

Wakizungumzia kuhusu kauli hiyo ya kulipa huduma za afya, baadhi ya wananchi wamekuwa na mtazamo tofauti, wakikubalina nao na wengine wakipinga.

Mkazi wa Gulioni, Shuleina Issa amekubalina na kauli hiyo akisema kuchangia huduma za afya ni muhimu kwa sababu inasaidia utoaji wa huduma nzuri.

“Ndio maana unakuta hata hospitali binafsi, japo ni kweli wanakuwa na gharama kubwa lakini wanatoa huduma nzuri kwa sababu gharama zinarudi, lakini huduma za bure siku zote zina changamoto yake, kwa hiyo binafsi namuelewa, wananchi wanatakiwa kubadilika,” amesema.

Wakati Shuleina akisema hivyo, Mbarouk Ali Mbarouk amesema wananchi wamezoea huduma bure, kwa hiyo kuwabadilishia ghafla itakuwa ni kuwaongezea ugumu wa maisha.

“Gharama za maisha zipo juu katika kipindi ambacho watu hawalipii huduma, sasa zikianza kulipiwa na ni huduma muhimu itakuwaje, lakini ni kwenda kinyume na mapinduzi matukufu,” amesema Mbarouk.