Rais Samia awataka Watanzania kujiunga bima ya afya kwa wote

Rais Samia Suluhu Hassan akiwasalimia wananchi wa Katoro mkoani Geita wakati alipowasili mkoani humo kufanya ziara ya kikazi ya siku moja leo Jumamosi Oktoba 15, 2022.
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kujiunga na bima ya afya kwa wote pindi itakapoanza ili waweze kupata huduma bora za afya pamoja na kuiwezesha serikali kuboresha huduma za afya nchini.
Geita. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kujiunga na bima ya afya kwa wote pindi itakapoanza ili waweze kupata huduma bora za afya pamoja na kuiwezesha serikali kuboresha huduma za afya nchini.
Rais Samia ameyasema hayo leo Oktoba 15, 2022 alipotembelea hospitali ya Kanda Chato na kusema kwa sasa Serikali inahamia kwenye mfumo wa bima ya afya kwa wote hivyo ni vyema wananchi wakajiunga.
Akizungumzia ujenzi wa hospitali hiyo Rais Samia amesema serikali itaendelea kuijenga kama ilivyokusudiwa na tayari wataalamu wa kutosha wameletwa kwenye hospitali hiyo.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwasalimia wananchi wa Katoro mkoani Geita wakati alipowasili mkoani humo kufanya ziara ya kikazi ya siku moja leo Jumamosi Oktoba 15, 2022.
“Hospitali hii ina vifaa vya kisasa kabisa kuchukua vipimo vyote ambavyo mwanzo mlikua muende Bugando sasa vinapatikana hapa,” amesema.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa hospitali ya kanda Chato, Mtendaji mkuu wa wakala wa Majengo nchini (TBA) Daudi Kondoro amesema hospitali hiyo inajengwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza yenye majengo matano yaliyogharimu Sh13bilioni yamekamilika na tayari yanafanya kazi.
Amesema awamu ya pili itajengwa kwa gharama ya Sh18.5 bilioni na itahusisha wodi yenye vitanda 210 pamoja na kazi za nje na mpaka sasa ujenzi ni asilimia 65 na tayari serikali imetoa Sh12.8 bilioni.
Amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na mkoa imetenga eneo la hospitali lenye ukubwa wa ekari 248 lililotengwa kwa huduma za kibingwa, nyumba za watumishi pamoja na chuo, ambapo hadi sasa zimetumika ekari 18 tu.
Akizungumza hospitali hapo Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema wakati Rais Samia akiingia madarakani hospitali hiyo ilikua haijaanza kazi lakini kwa fedha zilizotolewa na serikali pamoja na watumishi kumewezesha huduma kuanza kutolewa.
Amesema kupitia fedha za tozo mkoa ulipokea Sh3 bilioni zilizowezesha vituo vitatu vya afya kujengwa na sasa wanaendelea na ujenzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa ambayo inajengwa kwa gharama ya Sh22 bilioni.
Mkurugenzi wa hospitali hiyo, DK Brian Mawala amesema wagonjwa 15,000 mbao wangelazimika kwenda hospitali ya rufaa ya Bugando kupata matibabu ya kibingwa wamehudumiwa hospitalini hapo toka julai 2021 ilipoanza kufanya kazi.
Naye Enock Elias, mkazi wa Chato ameishukuru serikali kwa gospitali hiyo, akisema imewaondolea adha ya kusafiri hadi jijini Mwanza walikokuwa wakilazimika kutumia zaidi ya siku mbili ili waweze kumuona daktari bingwa.