Rais Samia awapangia mabalozi vituo vya kazi, Dk Nchimbi arejea nyumbani
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan, amewapangia vituo vya kazi mabalozi, wamo wateule sita aliowateua Mei 10, 2023; huku akiwabadilisha wanne vituo vyao vya kazi.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amewapangia vituo vya kazi mabalozi, wamo wateule sita aliowateua Mei 10, 2023; huku akiwabadilisha wanne vituo vyao vya kazi.
Sambamba na hilo, Rais Samia amemrudisha nyumbani Balozi Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa akiiwakilisha Tanzania nchini Misri tangu Machi mwaka 2022.
Kwa mara ya kwanza, Rais wa awamu ya tano Hayati Dk John Magufuli, alimteua Dk Nchimbi kuwa Balozi akiiwakilisha Tanzania nchini Brazil, Desemba 3, 2016; kabla Rais Samia hajamhamisha kwenda kuwa Balozi nchini Misri.
Taarifa hiyo imetolewa leo Ijumaa, Agosti 11, 2023 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus, imewataja Mabalozi wateule waliopangiwa vituo vya kazi kuwa ni Balozi Fatma Mohammed Rajab kuwa Balozi nchini Oman.
Balozi Rajab anachukua nafasi ya Balozi Abdallah Abasi Kilima ambaye amestaafu.
Mwingine ni Balozi Joseph Edward Sokoine, ambaye sasa anakuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada, akichukua nafasi ya Balozi Dk Mpoki Ulisubisya ambaye amestaafu.
Balozi Naimi Sweetie Azizi amepangiwa kuwa Balozi wa Austria, huku Meja Jenerali Ramson Mwaisaka akipangiwa kuwa Balozi nchini Rwanda.
Meja Jenerali Mwaisaka anachukua nafasi ya Balozi Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanzo ambaye amehamishiwa Cairo, Misri.
Aidha Balozi Gelasius Byakanwa, amepangiwa kuwa Balozi nchini Burundi, akichukua nafasi ya Balozi Jilly Maleko ambaye amestaafu.
Balozi Habib Awesi Mohamed, yeye amepangiwa kuwa Balozi nchini Qatar, akichuka nafasi ya Balozi Mahadhi Juma Maalim ambaye amehamishiwa Kuala Lumpur, Malaysia.
Kwa upande mwingine Rais Samia pia amempangia Balozi Salum Njalikai, kuiwakilisha Tanzania nchini Algeria akichukua nafasi ya Balozi Meja Jenerali Jacob Kingu ambaye amestaafu.
Taarifa hiyo imesema kuwa, Balozi Hassan Mwamweta, amaepangiwa kuiwakilisha Tanzania nchini Ujerumani, akichukua nafasi ya Balozi Abdallah Saleh Possi, ambaye amehamishiwa Geneva, Uswisi.
Pia Rais ampangia Dk Mohamed Juma Abdallah, kuwa Balozi nchini Saudi Arabia, akichukua nafasi ya Balozi Ali Jabir Mwadini, ambaye amehamishiwa Ufaransa.
Kwa upande wa mabalozi ambao wamehamishwa vituo vya kazi, taarifa ya Ikulu imeelza kuwa, Balozi Alli Jabir Mwadini amehamishiwa Ufaransa, akichukua nafasi ya balozi Dk William Shelukindo, ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Masahariki.
Mwingine aliyehamishwa ni Balozi Meja Jenerali Richard Makanzo, kuwa Balozi nchini Misri, akichukua nafasi ya Balozi John Emmanuel Nchimbi ambaye anarejea nyumbani.
Balozi Abdallah Saleh Possi anakuwa mwakilishi wa kudumu katika ofisi za Umoja wa Mataifa Geneva, Uswis akichukua nafasi ya Balozi Maimuna Tarish ambaye amemaliza mkataba wake.
Balozi Dk John Simbachawene anakuwa Balozi nchini Uganda akichukua nafasi ya Balozi Dk Azizi Mlima ambaye amestaafu.
Taarifa hiyo imesema wateule hao wataapishwa Agosti 16 Ikulu Chamwino Dodoma.