Rais Samia ateua viongozi saba

Muktasari:

  • Leo Ijumaa, Februari 3,2023, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa viongozi saba wakiwemo makamishna wawili wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo Ijumaa Februari 3, 2023 amefanya uteuzi wa viongozi saba kushika nyadhifa tofauti katika taasisi za Serikali.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu imeeleza, Rais Samia amemteua Janet Mbene kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Amemteua James Mwainyekule kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).

Kabla ya uteuzi huo, Mwainyekule alikuwa Mhasibu Mkuu, Tume ya Pamoja ya Fedha, Wizara ya Fedha na Mipango, Dodoma.

Mbali na wawili hao, amemteua Rashid Mchatta kuwa Skauti Mkuu Tanzania kuchukua nafasi ya Mwantumu Mahiza ambaye muda wa kutumikia nafasi hiyo umemalizika.

Kadhalika, Rais Samia amemteua Gilead Teri kuwa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) huku Damasi Mfugale akiteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Kabla ya uteuzi huo, Teri alikuwa Mshauri Mwandamizi, Umoja wa Ulaya (EU), Copenhagen, Denmark na Mfugale alikuwa Mshauri Mwandamizi wa Kampuni ya Afrika Chapter EBI International Consulting Group, Canada.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amewateua Makamishna wa Tume wawili ambapo Caroline Mutahanamilwa ameteuliwa kuwa Kamishna wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania na Idd Mandi kuwa Kamishna wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania.