Rungu la Samia lilivyotua kwa ma-DC

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kuijenga safu ya uongozi ndani ya Serikali anayoiongoza kwa kuwateua wakuu wapya wa wilaya 37 na kuwahamisha vituo 47 na wengine 55 wakibakizwa kwenye vituo vyao vya kazi.

Hatua hiyo ya Rais Samia ni utekelezaji wa kauli aliyoitoa kwenye mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika Desemba 8 mwaka jana alipoomba kuipanga upya Serikali ili kujiimarisha zaidi na uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika mwaka 2025 kwa kuwaondoa watu ambao hawaendani na kasi yake.

Katika mkutano huo alisisitiza kuwa kuna safari ya miaka mitatu mbele ya kuendelea kuwatumikia Watanzania, hivyo anataka Serikali ifanye kazi ili wananchi wenyewe waseme mambo ambayo Serikali imeyafanya badala ya Serikali kulazimika kujisemea.

“Tayari tumeshapata safu nzuri ya kwenda na kazi za chama pamoja na kukabiliana na chaguzi zijazo. Naomba sasa mnipe baraka zenu nikaipange Serikali pia…kwa jinsi ninavyohisi, timu hii tunaweza kwenda na wakayatekeleza yale mliyoyasema hapa kwa vizuri zaidi,” alisema Rais Samia kwenye mkutano mkuu huo.

Katika orodha ya wakuu wa wilaya iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, Rais Samia amewaacha wakuu wa wilaya 37 na kuwateua wapya kujaza nafasi zao muda wowote kuanzia sasa pindi watakapoapishwa.

Pia, Rais Samia amewahamisha vituo vya kazi wakuu wa wilaya 47 na kuwabakiza 55 katika vituo vya awali.

Mabadiliko hayo yanatajwa kuwa ni mkakati wa Serikali kuongeza ufanisi na utendaji katika wilaya zilizoonekana kulegalega au kutokana na tuhuma zilizokuwa zikiwakabili baadhi ya viongozi hao waliotemwa.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa siasa wamesema huo ni mkakati wa Rais Samia kujiandaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kama alivyoahidi ndani ya chama chake siku chache zilizopita.


Wakuu walioachwa

Mkeka alioutoa Rais Samia jana umewaacha waliokuwa wakuu wa wilaya 37 aliowateua Juni 19 mwaka 2021, miezi mitatu tangu aapishwe kuliongoza Taifa akichukua nafasi iliyoachwa na Dk John Magufuli, aliyefariki siku chache tangu aapishwe kuongoza muhula wa pili.

Baadhi ya wakuu wa wilaya walioachwa katika mabadiliko ya jana ni Gabriel Zacharia (Busega) ambaye kabla ya kuteuliwa alikuwa mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na mwanahabari mwenzake, Jerry Muro aliyekuwa wilayani Ikungi. Muro aliwahi kufanya kazi na kituo cha runinga cha ITV kisha TBC.

Rais Samia pia amemwondoa Lupakisyo Kapange, aliyekuwa Bariadi, Frank Mwaisumbe wa Monduli, Jamhuri William wa Nyang’wale na Martha Mkupasi wa wilayani Chato.

Wengine ni Siriel Mchembe wa Handeni, Sezaria Makota wa Mbulu, Richard Ruyango wa Arumeru na Julieth Binyura wa Karagwe. Panga hilo limewapitia pia Simon Mayeka aliyekuwa Chunya, Ismail Mlawa wa wilayani Kyela na Sarah Msafiri wa Kibaha.

Wamo pia Andrea Tsere aliyekuwa Ludewa, Cosmas Nshenye wa Mbozi na Josephat Maganga kutoka Mpwapwa pamoja na Pololet Mgema wa Songea.


Waliohamishwa vituo

Wakuu wa wilaya 47 wamehamishwa kituo cha kazi ili kujiongezea uzoefu wa maeneo tofauti. Katika kundi hili, wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam zimebadilishiwa viongozi hao.

Wilayani Ilala, Rais amempeleka Edward Mpogolo kutoka Same, huku Halima Bulembo aliyekuwa Muheza akienda Kigamboni na Hashim Komba akitoka Nachingwea kwenda Ubungo na Mwanahamisi Mukunda akihamishiwa Wilaya ya Temeke kutoka Bahi. Katika mabadiliko hayo, Rais Samia amemhamisha Saadi Mtambule kutoka Mufindi kwenda Kinondoni.

Wakati wakuu hao wapya wakiingia, waliokuwapo wametawanywa mikoani. Aliyekuwa Ubungo, Kherry Denis James amehamishiwa Mbulu huku Ng’wilabuzu Ludigija wa Ilala akipelekwa Kwimba na Fatma Nyangasa akitolewa Kigamboni kwenda Kisarawe. Aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo amehamishwa Korogwe na wa Kinondoni, Godwin Gondwe akipelekwa Bahi.

Kwingineko, Suleiman Mwenda aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Monduli anakwenda Iramba, huku Sophia Kizigo akihamishwa kutoka Mpwapwa kwenda Mkalama. Veronica Kessy amehamishiwa Wilaya ya Iringa akitokea Misungwi wakati Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Advera Bulimba akitolewa Nzega kwenda Biharamulo na Majid Mwanga aliyekuwa Kilosa akipelekwa Wilaya ya Mlele.


Wanaoendelea

Kwenye orodha ya mabadiliko, wakuu 55 wa wilaya wanaendelea na kazi katika vituo vyao, akiwamo Dadi Kolimba wa Karatu, Raymond Mangwala (Ngorongoro), Dk Khamis Mkanachi (Kondoa) na Remedius Mwema (Kongwa).

Wengine ni Jabir Shekimweri (Dodoma), Gift Msuya (Chamwino), Said Nkumba (Bukombe), Peres Magiri (Kilolo), Kanali Wilson Sakullo (Misenyi), Kanali Mathias Kahabi (Ngara) na Jamila Kimaro (Mpanda).

Pia, yumo Onesmo Buswelu (Tanganyika), Kanali Michael Ngayalina (Buhigwe), Kanali Evance Mallasa (Kakonko), Kanali Aggrey Magwaza (Kibondo), Kanali Issac Mwakisu (Kasulu) na Kanali Hamis Maiga (Rombo).

Abdallah Mwaipaya amebakishwa wilayani Mwanga na Shaibu Ndemanga wa Lindi sawa na Hassan Ngoma wa Ruangwa.


Uwiano wa kijinsia

Katika uteuzi wa wakuu 139 wa wilaya, Rais Samia amewateua wanawake 42 na wanaume 97. Idadi hiyo imepungua ikilinganishwa na uteuzi kama huo alioufanya Juni 19 mwaka 2021 uliokuwa na wanawake 44 na wanaume 95.

Katika orodha ya wateule 37 wapya, Rais Samia amewateua wanawake 14 na wanaume 23 na kwa wakuu 47 wa wilaya aliowahamisha vituo vya kazi, wanawake ni 16 na wanaume 31.

Vilevile, katika wakuu 55 wa wilaya wanaoendelea kwenye vituo vyao vya kazi, wanawake ni 12 na wanaume ni 43.

Kwenye uteuzi wa Juni 19 mwaka 2021 uliokuwa wa kwanza kwa Rais Samia, wakuu wapya walikuwa 56 na walioendelea walibaki 83, kati yao wanaume walikuwa 57 na wanawake 26.


Wasomi wachambua

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Faraja Kristomus alisema Rais Samia aliomba kibali ndani ya chama chake kuisuka Serikali baada ya kubaini kubadilisha mawaziri pekee haitoshi, bali anahitaji kuanzia ngazi za chini kwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri na wakuu wa wilaya ili kuongeza ufanisi katika kusimamia ajenda zake.

“Hizi ni ngazi muhimu za utendaji serikalini ambako anahitaji watu wazuri wa kusimamia uamuzi, dira na maono yake (Rais) katika ngazi hizo za chini, ndiko mambo yanaonekana dhahiri kwa wananchi,” alisema Dk Kristomus. Alisema mabadiliko hayo yanaweza kuwa na maana mbili, kwanza ni kuimarisha utendaji wa Serikali kwenye ngazi ya chini na pili ni kuimarisha safu ya makada wa CCM kwa sababu, kihistoria nafasi hizo zimekuwa zikitolewa kwao.

“Kwa ujumla anaimarisha safu ya ushindi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Kwa hiyo, kuna mambo mawili ndani yake, wakati Serikali ikijipanga, chama nacho kinajipanga ili kuleta taswira nzuri ya CCM na Serikali yake kwa mwaka 2025,” alisema.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie alisema mabadiliko hayo ya wakuu wa wilaya yanaweza kuwa na sababu kadhaa, ikiwamo kufanikisha malengo ya utawala na kuandaa njia kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Dk Loisulie alisema uamuzi wa Serikali kufanya mabadiliko hayo unaweza kuathiriwa na umuhimu wa nyadhifa za wakuu wa wilaya katika kufanikisha mipango ya maendeleo na ustawi wa raia.

“Wananchi wana matarajio makubwa na Serikali yao, ikiwa walio madarakani watashindwa kufanikisha mipango fulani ipasavyo, mabadiliko hayaepukiki,” alikumbusha Dk Loisulie.

Mwanazuoni huyo alieleza kwamba mabadiliko hayo yanaweza pia kuhusishwa na uhuru mpya wa kisiasa uliorejeshwa nchini, ikiwamo ruhusa ya kufanya mikutano ya kisiasa.

“Timu imara ya watendaji, hasa katika ngazi za chini inahitajika kwa wale walio madarakani ili kukabiliana na vuguvugu la kisiasa linalokuja kutokana na mabadiliko ya uendeshaji wa shughuli za siasa nchini,” alisema na kuongeza kuwa umuhimu ni mkubwa zaidi kwa kuwa chama tawala kinatarajia kuendelea kubaki madarakani.

Akiwa na mtazamo kama huo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Buberwa Kaiza alisema mchakato mzima wa mabadiliko hayo ni sehemu ya mageuzi ambayo Rais Samia aliahidi kuyafanya katika hotuba zake kadhaa alizowahi kuzitoa ndani ya chama hata mbele ya kadamnasi.

“Mara kadhaa, (Rais) alionyesha nia ya kurekebisha muundo wa Serikali. Amebakiza miezi michache amalize mwaka wake wa pili ofisini na tayari mabadiliko yamefanyika,” alisema na kuongeza kuwa:

“Mageuzi ya Serikali yanaanzia ngazi za chini kabisa na kwa mujibu wa uteuzi wa Rais, wanaanzia katika ngazi ya wilaya hivyo amekusanya timu ya watu ambao anaamini watamsaidia kufanikisha mipango yake ya maendeleo kwa wananchi.”