Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia ashauri mbinu za kukuza mashirika ya Posta Afrika

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) lililopo eneo la Philips jijini Arusha.

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameutaka Umoja wa Posta Afrika (PAPU) kuwezesha mashirika ya posta barani Afrika ikiwa pamoja na kuhakikisha yanaongeza wigo wa usafirishaji wa vifurushi kwa kutumia mashirika ya ndege ya ndani ya bara hilo.

Arusha. Katika hatua za kukuza mitaji ya ndani, Rais Samia Suluhu Hassan ameutaka Umoja wa Posta Afrika (PAPU) kuwezesha mashirika ya posta barani Afrika ili yakuze utendaji ikiwa pamoja na kuongeza wigo wa usafirishaji wa vifurushi kwa kutumia mashirika ya ndege ya ndani ya Afrika. 

 Rais Samia amesema huduma za posta zikiimarishwa kutakuwa na safari za ndege za ndani ya bara la Afrika kwa ajili ya kusafirisha vifurushi kutoka nchi moja kwenda nyingine.

Samia ametoa maelekezo hayo leo Septemba 2, 2023 wakati wakati akizindua jengo la makao makuu ya PAPU lililopo jijini Arusha likihusisha nchi wananchama 43 waliojiunga na umoja huo.

Uzinduzi wa jengo hilo ulienda sambamba na uzinduzi wa stika mpya za posta kwa nchi za Tanzania, Algeria, Nigeria, Misri, Morocco, Senegal na Zimbabwe.

Akizungumza katika hafla hiyo amesema huduma za posta katika nchi nyingi zimepoteza mvuto licha ya umuhimu wake, hivyo ni kazi ya umoja huo kuhakikisha ufanisi wa huduma za posta unaongezeka na kuendana na mabadiliko ya sasa ya kidijitali ili kuwavutia watu wengi kutumia.

“PAPU iwezeshe mashirika ya Posta Afrika kwa kutumia mashirika yetu ya ndege ya ndani badala ya kutumia mashirika ya nje ya Afrika na hii itatulazimisha tuwe na muunganiko ndani ya bara. Posta itulazimishe ndege zetu zisafiri ndani ya Afrika kupeleka vifurushi,” amesema.

Pia ameeleza haja ya PAPU kuwa na mfumo mmoja wa biashara mtandao kupitia maduka ya mtandao yanayofanya biashara.

“Ni matarajio yangu kwa kufanya hivi mtakuwa mmefanikiwa kufikia maono ya umoja wa posta duniani kupitia mradi wa wa E-commerce ndani ya Afrika.

“Sina shaka Umoja wa Posta Afrika unaweza kuleta mageuzi makubwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa ya bara letu, kama ili play role (ilichangia) ya kuleta uhuru na sasa inaweza ku play role ya kuleta mabadiliko ya kidijitali katika huduma za posta.”

Sambamba na maelekezo hayo, Rais Samia ametaka jengo hilo litumike kujengeana uwezo na kubadilishana uzoefu kuongeza ubunifu na kufanya mageuzi ya utendaji wa posta za nchi wanachama.

Amesema mageuzi yanayofanyika kwa nchi wanachama yapo katika viwango tofauti vya mafanikio ambapo nchi nyingine zimepoteza matumaini ya huduma za posta.

“Jengo hili lifanywe uwiano wa maendeleo ya posta zetu Afrika sote tuwiane tuweze kutoa huduma zinazoweza kutegemewa na watu wetu. Mkiweza kufanya hivyo mtachangia katika ukuaji wa uchumi wa kidijitali na kuifanya umoja wa Afrika kujivunia uwepo wa posta Afrika,” amesema Rais Samia.

Jengo hilo la ghorofa 17 linamilikiwa na PAPU kwa asilimia 60 na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 40 na ujenzi wake umegharimu Sh54.8 bilioni. Ndani ya jengo hilo kuna chumba maalum kilichodhaminiwa na nchi ya Misri ambayo imeweka samani zinaoonyesha utamaduni wa nchi hiyo.