Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia amwaga vyeo Polisi

Muktasari:

  • Julai 2023, Tume ya kuangalia namna ya kuboresha Taasisi za Haki Jinai chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Othman Chande iliwasilisha ripoti kwa Rais Samia ikiwa na mapendekezo kadhaa.

Dar es Salaam.Ameandika historia, ndivyo unavyoweza kuelezea uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwapandisha vyeo maofisa wa juu wa Jeshi la Polisi 154 kwa mpigo, huku watano wakiruka cheo kimoja na kuwa manaibu kamishna.

Taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam na makao makuu ya Polisi jijini Dodoma, zinaeleza uamuzi huo wa Rais, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu, ni wa kwanza na wa kihistoria tangu aapishwe kuwa Rais Machi 19, 2021.

Julai 20, 2022, Rais Samia alimpandisha cheo Camilius Wambura kuwa Kamishna wa Polisi (CP) na baadaye kumteua kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi. Pia akampandisha cheo DCP Faustine Shilogile kuwa CP akishughulikia Polisi Jamii.

Hakuishia hapo, alimpandisha cheo ACP Ramadhan Kingai kuwa CP na kumteua kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).

Oktoba 2022, alimpandisha cheo SASP, Suzan Kaganda na kuwa CP.

Hatua ya kuwapandisha maofisa 154 kwa mpigo inatajwa kuvunja rekodi.

“Haijapata kutokea Rais akapandisha vyeo maofisa wengi kiasi hiki, kwa kweli anastahili pongezi,” kilidokeza chanzo kimoja cha habari.

Akizungumza juzi wakati wa hafla ya kuwaaga watumishi waliomaliza muda wao na kuwapongeza waliofanya vizuri mwaka 2023, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini (DPA), Dk Lazaro Mambosasa alisema amepandishwa cheo Februari 15, kutoka Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) kuwa Naibu Kamishna (DCP), akiwataka askari kuwa mabalozi wazuri wa Jeshi la Polisi ili kuwa watumishi wema.

“Mimi ni mstaafu mtarajiwa, likizo yangu ya kustaafu nitaianza Desemba mwaka huu na Februari mwakani nitaondoka rasmi, cheo hiki nimesafiria miaka minane, cheo si mapambo wala zawadi, ni stahili ya mtumishi anayetimiza wajibu wake na mwajiri akaona matunda yako,” alisema.

Vyanzo mbalimbali vimewataja miongoni mwa maofisa wa Polisi walioruka cheo kimoja kutoka Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) hadi kuwa Naibu Kamishina wa Polisi (DCP) ni pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa.

Wengine ni Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Zanzibar; Zuberi Chambera, Tatu mfaume, Adolfina Ngoso na Kombo Hamis Kombo, ambao wameruka cheo cha Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi nchini (SACP).

Katika kuwapandisha vyeo maofisa hao, Rais Samia pia amempandisha cheo Mkuu wa Wilaya ya Biharamuro na aliyewahi kuwa msemaji wa Jeshi hilo, Advera Bulimba kutoka cheo cha ACP hadi SACP. Bulimba alipata pia kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nzega.

“Hata msemaji wa sasa wa Jeshi la Polisi, David Misime naye amepanda kutoka SACP hadi Deputy Commissioner (Naibu Kamishna). Unajua tangu kipindi cha Magu (Rais John Magufuli) hakujapandishwa watu wengi hivi,” Mwananchi Digital imedokezwa.

Chanzo kutoka ndani ya jamii ya Polisi mkoani Mbeya, kimeeleza Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Benjamin Kuzaga aliamua kumpa gari lake  Kombo Hamis Kombo, ambaye amerushwa cheo kutoka ACP hadi DCP wakati yeye sasa ni SACP.

“Ni uungwana tu RPC amefanya maana Kombo ameruka cheo kimoja na kumpita RPC ambaye awali wote walikuwa na cheo sawa cha ACP. Ila kwa kweli Rais Samia amefanya jambo jema sana kuwakumbuka polisi,” kimeeleza chanzo hicho.

Kombo ni Mkuu wa Kitengo cha Intelijensia ndani ya Polisi Mkoa wa Mbeya.

Kulingana na vyanzo hivyo, wengine waliopanda vyeo na kuwa DCP ni msemaji wa sasa wa Jeshi la Polisi, David Misime, Ulrich Matei, Gustavus Babile, Johansen Kahatano, Andrew  Jumamosi, Fortunatus Muslim na Goyayi Goyayi.

Katika orodha hiyo wamo Dk Gabriel Makungu, Onesmo Lyanga, Robert Mayala, Lazaro Mambosasa, Mihayo Msikhela, Henry Saiyoki, Renata Mzinga, Kheriyangu Khamis, Neema Mwanga, Gemini Mushy, Mwamini Rwantale na Alute Makita.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhan Ng’anzi nao wameukwaa u-DCP.

Katika upandishaji huo wa vyeo, makamanda wa Polisi wa mikoa na vikosi hawakuachwa nyuma kwani kwa uchache, makmanda wa  mikoa takribani 17 wamepanda hadi  kuwa manaibu kamishna ( DCP) na Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP).

Miongoni mwao waliopanda vyeo na kuwa DCP ni Mutabihirwa wa Singida, Mambosasa na Kahatano ambaye kwa sasa yuko Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra).

Kulingana na vyanzo vya kuaminika ndani ya polisi, Ma-RPC waliopanda kutoka ACP hadi SACP na mikoa yao ikiwa kwenye mabano ni Benjamin Kuzaga (Mbeya), Simon Maigwa (Kilimanjaro), Janeth Magomi (Shinyanga) na Richard Abwao (Tabora).

Wegine katika orodha hiyo ni Blasius Chatanda (Geita), Sophia Jongo (Geita), Casta Ngonyani (Katavi), George Katabanzi (Manyara), Mtatizo Kitinkwi (Kinondoni), Mark Ngere (Tarime/Rorya), Nicodemus Katembo (Mtwara), Theopista Mallya (Songwe), Justine Masejo (Arusha), Richard Ngole (Temeke), Marco Chillya (Ruvuma) na John Makuri (Lindi).

Kwa mujibu wa taarifa za upandishaji huo, wateuliwa wote wa cheo cha DCP na SACP waliopo Dodoma, Iringa, Morogoro, Singida na Manyara, wametakiwa kuwepo Dodoma Februari 20, 2024 kwa ajili ya kula kiapo rasmi na kupewa maelekezo mbalimbali.

Rais Samia amewapandisha vyeo maofisa hao wakati ambao Jeshi hilo limekuwa likinyooshewa kidole na wadau wa haki jinai kwa kukiuka haki za binadamu, hali iliyomsukuma Rais Samia kuunda Tume ambayo ilipewa jukumu la kuangalia namna ya kuboresha taasisi za haki jinai likiwamo Jeshi la Polisi.


Mapendekezo ya Tume

Julai 2023, Tume ya kuangalia namna ya kuboresha Taasisi za Haki Jinai chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Othman Chande iliwasilisha ripoti kwa Rais Samia ikiwa na mapendekezo kadhaa.

Kuhusu Jeshi la Polisi, tume ilisema kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusu vitendo vinavyochafua taswira ya jeshi hilo.

Malalamiko hayo dhidi ya Jeshi la Polisi yanahusu kushindwa kuzuia uhalifu, matumizi ya nguvu kupita kiasi, kubambikia kesi, vitendo vya rushwa, mali za watuhumiwa kupotea vituoni na kuchelewa kufika kwenye maeneo ya matukio.

Kutokana na hali hiyo tume ilisema inasababisha wananchi kupoteza imani kwa Jeshi la Polisi na kutotoa ushirikiano unaotakiwa.

Tume ilipendekeza Jeshi la Polisi lifanyiwe tathmini ya kina na  lifanyiwe maboresho makubwa na kuundwa upya ili kuondoa kasoro za kiutendaji zilizopo.

Pia, ilipendekeza Jeshi la Polisi libadilishwe kisheria, kimuundo na kifikra na kuwa Polisi Tanzania ili kutoa taswira kuwa Jeshi la Polisi ni chombo cha kuwahudumia wananchi; kubadilisha mitalaa ya mafunzo na mtazamo wa askari wa Jeshi hilo ili kutoka katika dhana ya ujeshi kuenda dhana ya kuhudumia wananchi.

Mapendekezo mengine ni jeshi liboreshe mfumo wa ndani wa kushughulikia malalamiko ya wananchi, liimarishe huduma za intelijensia ya jinai, huku kitengo cha  Polisi Jamii kikishauriwa  kuanzisha programu za kujisogeza zaidi kwenye jamii.

Kwa mujibu wa maelezo yaakliyomo kwenye tovuti ya Jeshi la Polisi, Jeshi la Polisi la Tanzania lilianzishwa rasmi 25 August 1919 kwa tangazo la Serikali ya Kiingereza lililotoka katika  Gazeti la Serikali No.Vol.1 No.21-2583 kwa wakati huo likaitwa Jeshi la Polisi Tanganyika.


Ilichobaini Tume ya Haki Jinai katika kufanya tathmini juu ya Jeshi la Polisi, tume ilipitia sheria, kanuni na  miongozo mbalimbali inayoliongoza Jeshi la Polisi.

Tume ilibaini kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi kupitia kifungu cha 7(2) cha Sheria ya Jeshi la Polisi  na Huduma Saidizi, amepewa mamlaka ya kutunga amri kuu za Jeshi la  Polisi kwa kuzingatia maelekezo na amri za waziri mwenye dhamana ya  mambo ya ndani ya nchi.

Uchambuzi wa tume umebaini kuwa PGO iliyotangazwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 351 la Mwaka 2021 imetengenezwa pasipo kuzingatia masharti na wigo wa kisheria uliopo katika  kifungu cha 7(2) cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi na Sheria  nyingine.

Baadhi ya maeneo yaliyoonekana kuwa na changamoto kubwa ni  masuala ya posho za askari, mamlaka za nidhamu, uchunguzi wa vifo vyenye  utata, gwaride la utambuzi wa mhalifu, mafao ya kustaafu kwa makamishna  wa Jeshi la Polisi na ukokotoaji wa mafao ya kustaafu kwa askari, wakaguzi  na maofisa.