Polisi wakumbushwa utii, kuheshimu viapo

Wakaguzi wa Jeshi la Polisi kutoka wilaya zote za Mkoa wa Pwani wakisikiliza maelekezo kutoka kwa Kamanda wa Polisi mkoani humo, Pius Lutumo (kulia) wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wakaguzi hao katika viwanja vya polisi mkoani, mafunzo yalitolewa kwa miezi miwili kuanzia mwezi Julai. Picha Julieth Ngarabali
Kibaha. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Pius Lutumo, amewataka wakaguzi wa Polisi kuwa na utii na kuheshimu kiapo chao katika utendaji kazi wao kwenye sehemu zao za kazi.
Kamanda Lutumo ameyasema hayo leo Jumapili Septemba 3, 2023 akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wakaguzi wa Jeshi la Polisi kwenye viwanja vya Polisi mkoani humo ambayo yalitolewa kwa muda wa miezi miwili.
Kamanda Lutumo amesema kuwa kiapo cha askari ni utii kwa Serikali iliyo madarakani na kuwaheshimu viongozi wote ikiwa ni pamoja na kuheshimu viongozi wa Jeshi katika kada ya vyeo mbalimbali.
"Tumeapa kuwatumikia wananchi lakini bado wapo baadhi ya askari wamekuwa wanasahau viapo vyao, hivyo muende mkawe wa kwanza kubadilika kifikra ili wale mnao wasimamia nao waweze kufuata nyayo zenu”.Alisema Lutumo
Aidha, Kamanda Lutumo amewakumbusha umuhimu wa kila mkaguzi kwenda kushirikiana na viongozi wa Serikali na wadau wengine kwenye kuzuia na kutanzua uhalifu kwenye Kata zao.
Aidha kuhusu jukumu la kuwalinda watoto na kupambana na vitendo vya ukatili. Lutumo amesema: “lipo kwenu nendeni mkashirikiane na taasisi zingine kwenye kupata matokeo chanya katika kesi zilizo kwenye himaya zenu za ukatili badala ya kesi hizo kumalizwa kienyeji,”.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo wakaguzi,Mkaguzi wa Polisi Rosemary Kamugisha akiongea kwa niaba ya wenzake amesema miezi miwili waliyokuwa kwenye mafunzo wameweza kujifunza mambo mbalimbali ambayo yameweza kuwaongezea uwezo katika kutekeleza majukumu yao.