Rais Samia akerwa rushwa, uzembe katika miradi

Rais Samia Suluhu Hassan
Muktasari:
Rais Samia Suluhu Hassan, amekerwa na vitendo vya rushwa na uzembe vinavyojitokeza mara kwa mara katika miradi maendeleo, huku akihoji uwepo wa Mamlaka za Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (Zaeca).
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amekerwa na vitendo vya rushwa na uzembe vinavyojitokeza mara kwa mara katika miradi maendeleo, huku akihoji uwepo wa Mamlaka za Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (Zaeca).
Vitendo vingine ni masuala ya uvujaji na matumizi mabaya ya fedha na vitendo vya wizi vinajitokeza na kuibuliwa na viongozi wa mbio za Mwenge wanapopita kwa ajili ya kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi.
“Kila mwaka tunapokea taarifa za kilele cha mbio au taarifa ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali) tunasomewa na kutajiwa maeneo ambayo Mwenge umekataa kuizindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi iliyopo katika baadhi ya halmashauri pia ile ambayo utekelezaji wake umekiuka kanuni za ujenzi au miradi kutumia fedha nyingi za umma ikiwa chini ya kiwango kinachokubalika.
“Hali hii inajirudi kila mwaka… Tunaposomewa taarifa za Mwenge wa Uhuru kila mwaka kuna miradi inayojirudia ni vitendo vya rushwa, uvujaji wa fedha na mambo mengine. Kila CAG anapokabidhi ripoti yake vitendo vinajirudia,” amesema Rais Samia.
Ameeleza hayo leo Ijumaa Oktoba 14, 2022 katika kilele cha maadhimisho ya mbio za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika mkoani Kagera zilizohudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango. Mbio za Mwenge zilianza Aprili 2 mwaka huu mkoani Njombe.
Katika maelezo yake, Rais Samia amesema, “hapa kuna swali kubwa la kujiuliza wakati miradi hii inajengwa, viongozi tupo na tunaona, lakini hakuna kinachozungumzwa wala kusema hadi Mwenge wa Uhuru upite, huu sio mtindo mzuri”
Kutokana na hatua hiyo, Rais Samia amewataka viongozi wote waliopo kwenye mamlaka kusimamia fedha za wananchi, akisema kodi zao zinazoshushwa chini kwa ajili ya maendeleo yao.
“Inasikitisha kuna watu wasiojali wala kuhurumia wananchi, wenye vitendo viovu ya kuwapa miradi wakandarasi wasiokuwa uwezo, waliotawaliwa na vitendo vya rushwa na wizi. Wengine wakiwa wazembe wanaosababisha miradi kutotekelezwa ipasavyo.
“Yanatokea haya viongozi tukiwa bado tupo, katika ngazi zetu tofauti, kuanzia taifa, mikoa, wilaya hadi halmashauri. Tunaona lakini tunasubiri vijana wakimbiza mwenge waje kusema miradi mibovu na haiendani na fedha zilizotumika,”amesema.
Rais Samia amesema licha ya kazi nzuri inayofanywa na PCCB na Zaeca, lakini bado zinahitaji kusaidiwa na vyombo vingine ili kuendelea kufanya kazi ya kudhibiti vitendo vya rushwa.
Hata hivyo, alitoa angalizo kabla ya Takukuru na Zaeca hazijaenda kushughulikia rushwa katika taasisi zijipekue kwanza kama zipo sawa. Amezitaka kujihakikisha kama zipo sawa na watumishi wake wa makao makuu na wale waliopo katika Serikali za mitaa wana sauti moja.
“Tungekuwa wote tunazungumza kauli moja vitendo hivi vingeonekana mapema na taasisi za kuzuia na kupambana na rushwa. Tunachokifanya ni kupambana na baada ya Mwenge kuibua kero katika kuzuia hatujafanya vizuri, ongezeni jitihada katika upande huu,”amesema Rais Samia.