Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bajeti ya uchukuzi itakavyotumika

Muktasari:

  • Bunge limepitisha bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka 2025/26, huku ikiainisha Sh2.75 trilioni zitakavyotumika. Wabunge wapongeza uwekezaji SGR na bandarini kwamba umeanza kuonesha mafanikio.

Dodoma. Wakati Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akielezea jinsi watakavyotumia Sh2.75 trilioni za bajeti ya mwaka 2025/26, wabunge wengi wamesifia utendaji wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Treni ya Kisasa (SGR).

Awali, akiwasilisha makadirio ya bajeti hiyo leo Alhamisi, Mei 15, 2025, Profesa Mbarawa ametaja baadhi ya miradi kuwa ni ujenzi wa SGR, wenye lengo la kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji katika ushoroba wa kati na kurahisisha biashara kati ya Bandari ya Dar es Salaam na nchi jirani.

Amesema mradi huo umetengewa Sh1.51 trilioni ambazo zitakwenda katika kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya reli hiyo katika maeneo mbalimbali na ununuzi wa vitendea kazi (vichwa vya treni, mabehewa, mitambo na mashine za matengenezo ya njia ya reli).

Profesa Mbarawa amesema Sh216.05 bilioni zitakwenda kwenye miradi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa ndege za Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).

“Mradi wa ununuzi wa ndege una lengo la kuboresha utoaji wa huduma za kusafirisha mizigo na abiria zenye kuhimili ushindani katika soko la kikanda na kimataifa na kuchagiza shughuli za utalii, kilimo na biashara ndani ya nchi,” amesema.

Amesema fedha hizo, pamoja na miradi mingine, zitatumika katika kuendelea na ulipaji wa madeni ya nyuma yaliyolimbikizwa kabla ya ufufuaji ili kuweka vizuri mizania ya vitabu vya hesabu za kampuni na kuimarisha imani miongoni mwa wadau wa ATCL.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa

Shughuli nyingine zitakazofanyika ni kukamilisha ununuzi wa ndege nne za masafa mafupi na moja ya mizigo yenye uwezo wa kubeba hadi tani 23; ununuzi wa injini moja ya ziada ya ndege aina ya Boeing 737-9 na ununuzi wa seti ya injini ya ziada ya ndege aina ya Q400.

Nyingine ni kuwezesha matumizi ya awali ya ndege nne zitakazonunuliwa aina ya Dash 8 Q400 kufika nchini kutoka kwa waundaji, pamoja na kuzinunulia vipuri muhimu vya awali kwa kuzingatia matakwa ya waundaji.

Pia amesema mradi mwingine ni kuimarisha uendeshaji wa ATCL, ambapo umetengewa Sh67 bilioni.

Amesema Mfuko wa Reli umetengewa Sh294.80 bilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Profesa Mbarawa ametaja miradi hiyo kuwa ni mradi wa uboreshaji wa usalama wa usafiri na usafirishaji katika bahari na maziwa makuu, ambao umetengewa Sh833.22 milioni.

Amesema mradi wa ujenzi na ukarabati wa meli katika maziwa makuu umetengewa Sh171 bilioni, na uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam (DMGP) umetengewa Sh24.08 bilioni.


Profesa Mbarawa amesema hadi kufikia Machi 2025, Serikali imeendelea na uboreshaji wa bandari hiyo, ikiwemo uboreshaji wa gati namba 8 hadi 11 na gati namba 12 hadi 15, ambapo upembuzi yakinifu wa kuboresha gati hizo umekamilika.

Aidha, ujenzi wa miundombinu ya kupokelea mafuta, pamoja na matanki 15 ya mafuta (tank farms) yenye uwezo wa kuhifadhi kiasi cha mita za ujazo 378,000, umeendelea na utekelezaji wake umefikia asilimia 25.

“Sambamba na uboreshaji wa bandari zilizopo katika Bahari ya Hindi, Serikali pia imeendelea kuongeza wigo wa huduma zake za kibandari kwa kujenga na kuboresha bandari zilizopo katika Maziwa Makuu nchini.

“Hadi kufikia Machi 2025, Serikali imekamilisha taratibu za kumpata mkandarasi wa kufanya maboresho ya Bandari ya Kigoma iliyopo katika Ziwa Tanganyika, unaohusisha ujenzi wa barabara ya kuingia bandarini na jengo la abiria,” amesema.

Aidha, waziri huyo amesema kumekuwa na faida za moja kwa moja kutokana na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika kuendeleza na kuendesha bandari nchini.

Pia amesema hatua hiyo imechochea shughuli nyingine za kiuchumi katika sekta mbalimbali na maeneo mengi, kutokana na kuimarika kwa utoaji wa huduma na hivyo kuleta ufanisi stahiki.

“Aidha, hatua hii imeendelea kuiwezesha Bandari ya Dar es Salaam kuwa lango la kibiashara kikanda na kimataifa,” amesema.

Miradi mingine ni ujenzi wa viwanja vya ndege vya Mwanza (Sh13.80 bilioni), Arusha (Sh4.57 bilioni), Mtwara (Sh6.57 bilioni), Kilimanjaro (Sh35 bilioni), na mradi wa uendelezaji wa viwanja vya ndege ambao umetengewa Sh20.59 bilioni.

Viwanja vya ndege vingine vitakavyojengwa ni Serengeti (Sh3 bilioni), Bukoba (Sh1.90 bilioni), huku uboreshaji na upanuzi wa jengo la pili la abiria Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) umetengewa Sh87.01 bilioni.

Profesa Mbarawa amesema Mradi wa Ukarabati wa Reli ya MGR – Tanzania Intermodal Rail Project – TIRP II 216 umetengewa jumla ya Sh51.28 bilioni.

Amesema Mradi wa Uboreshaji wa Reli ya Tazara umetengewa jumla ya Sh12.32 bilioni, pamoja na mambo mengine ukiwa umeelekezwa katika ununuzi wa mabehewa 30 ya abiria.

Amesema mradi wa rada, vifaa na miundombinu ya hali ya hewa umetengewa Sh13.50 bilioni (fedha za ndani) na Sh1.99 bilioni (fedha za nje).


Bandari na SGR

Katika michango ya wabunge, wamegusia maendeleo ya bandari nchini na ujenzi wa SGR, wakisema uwekezaji huo awali ulipingwa, lakini sasa unaonekana kuzaa matunda.

Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Kilumbe Ng’enda, amepongeza utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa kuongeza mapato, ambayo yametokana na kampuni ya DP World.

“Watanzania mmeona tulisimama katika Bunge hili, tukawaambia kinachokwenda kufanyika ni kikubwa. Kutoka TICTS (Kampuni ya Kuhudumia Makontena Tanzania), iliyokuwa ikiendesha bandari ile, kuja DP World tumeongeza mapato ya Sh1 trilioni, ni karibu asilimia nne hadi tano ya bajeti ya nchi yetu,” amesema.

Pongezi hizo ziliungwa mkono na Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Timotheo Mzava, aliyesema kuwa wakati wa mchakato wa uwekezaji wa bandari hiyo kulikuwa na maneno mengi ya ovyo, kufikirika, uongo na mengine ya kusadikika, lakini Rais Samia Suluhu Hassan alisimamia maono.

“Muda wa meli kusubiri umepungua sana, lakini muda wa kuhudumia meli kutoka wastani wa siku saba hadi tatu. Haya ni mafanikio makubwa sana katika nchi yetu… Wizara na Serikali anzeni kuangalia namna ya kubuni biashara mpya katika bandari, biashara ya kufaulisha mizigo,” amesema.

Mbunge wa Mvumi (CCM), Livingstone Lusinde, amesema kumalizika kwa ujenzi wa SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kumerahisisha usafiri kwa abiria, kwani safari huchukua muda mfupi.

“Watu wanakwenda wanateleza… Tumeona jinsi gani treni yetu imekuwa ikisimamiwa kwa usafi na mabinti zetu wapo hapo juu, wanatunza mazingira, wana lugha nzuri, yaani ukisafiri unakuwa kama unasafiri Ulaya. Hili tunataka kuliona,” amesema.

Ameshauri kutolewa kwa elimu katika maeneo yote ambayo treni hiyo inapita, ili watu wafahamu kuwa treni hiyo ni mali yao na hivyo kuepusha hujuma za kuharibu treni.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mwantumu Haji, amesema treni hizo za kisasa zimekuwa zikifanya kazi vizuri, na kuwa watu wengi wamekuwa wakikimbilia usafiri huo, hata badala ya ndege.

“Uvutaji wa sigara unaambiwa hautakiwi, lakini pombe inanywewa, hatari. Sijui kama Serikali inalitambua hili jambo au vipi,” amesema.

Amewataka watendaji kuliangalia suala hilo, maana wanywaji hao wamekuwa wakipiga kelele na kucheza ngoma ambazo hazipo katika treni hiyo.

Aidha, amelalamikia kuchelewa kwa ndege, jambo ambalo limewafanya kuchelewa safari wanazokwenda.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Suleiman Kakoso akiwasilisha maoni ya kamati yake kuhusu bajeti hiyo, ameitaka Serikali kuongeza ufanisi na ubunifu katika utendaji kazi utakaochochea kuboresha huduma za sekta ya uchukuzi nchini.

Amesema ufanisi huo utachochea maendeleo ya uchumi katika utekelezaji wa miradi yote, ili iweze kuakisi viwango bora, uendelevu na kuwepo kwa thamani ya fedha, pamoja na kuongeza ufanisi na ubunifu katika kukusanya maduhuli kutokana na vyanzo vilivyopo na kubaini vyanzo vipya.

“Serikali ihakikishe kwamba huduma zitolewazo na taasisi zake zinakuwa bora ili kukidhi matarajio ya wadau muhimu wa sekta ya uchukuzi,” amesema Kakoso.

Kuhusu SGR, kamati hiyo imeshauri Serikali kuja na mpango utakaowezesha vipande hivyo vya reli ya SGR kukamilika kwa wakati, ili njia ya reli ya kati ianze kufanya kazi kwa ukamilifu wake.

Akihitimisha hoja yake, Profesa Mbarawa amesema wamechukua michango yote ya wabunge na watakwenda kuifanyia kazi, ili iendelee kuleta ufanisi katika sekta ya uchukuzi na usafirishaji.

Kuhusu suala la uchelewaji wa ndege za ATCL, Profesa Mbarawa amesema wamelichukua suala hilo na watakwenda kulifanyia kazi, huku akibainisha kuwa changamoto hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa.