Rais Samia aita Baraza la Mawaziri kujadili ajali ya ndege

Muktasari:
Ndege ya Precision Air 5H-PWF, ATR 42-500 ambayo ilikuwa na watu 43 ilianguka Jumapili Novemba 6, 2022 asubuhi katika Ziwa Victoria karibu na uwanja wa ndege wa Bukoba na kusababisha vifo vya watu 19 na 24 wakinusurika
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameitisha kikao cha dharura cha Baraza la Mawaziri kujadili ajali ya ndege ya Precision Air 5H-PWF, ATR 42-500.
Ndege hiyo iliyoanguka Jumapili Novemba 6, 2022 asubuhi katika Ziwa Victoria karibu na uwanja wa ndege wa Bukoba, Mkoa wa Kagera na ilisababisha vifo vya watu 19 na 24 wakinusurika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumamosi, Novemba 12, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam katika mkutano wa mafanikio ya ziara ya Rais Samia katika nchi za China na Misri, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais- Ikulu, Zuhura Yunus alisema kikao hicho kitafanyika kesho Jumatatu jijini Dodoma.
“Kutakuwa na mkutano wa dharura jijini Dodoma kuhusu ajali tuliyoipata hivi karibuni, ni mkutano wa Baraza la Mawaziri,” alisema Yunus.
Ndege hiyo ambayo ilikuwa na watu 43 ambao abiria walikuwa 39, wahudumu wawili na marubani wawili ilikuwa inatoka Dar es Salaam kwenda Bukoba.
Hata hivyo, mamlaka zimesema kuwa uchunguzi umeshaanza kufuatia ajali hiyo.
Novemba 8, 2022, Serikali ilisema timu tatu zinatarajia kufanya uchunguzi ajali ya ndege ya Precision Air yenye namba za usajiri ATR 42-5H PWF iliyotokea Bukoba mkoani Kagera.
Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa alizitaja timu tatu zitakazochunguza ajali ya kampuni ya Precision iliyotokea Novemba 6 Bukoba, mkoani Kagera, kuwa ni pamoja na Kitengo maalum cha uchunguzi cha ajali za anga, kampuni iliyotengeneza ndege na Kampuni iliyotengeneza injini.
Jana Jumamosi, Mkuu wa mkoa wa Kagera, Albert Chalamila akizungumza na waandishi wa habari alisema kampuni ya ATR ya Ufaransa iliyotengeneza ndege ya Precision Air iliyopata ajali Novemba 6, 2022 tayari wamewasili katika mkoa wa Kagera na wamechukua vifaa vinavyohitajika katika ndege kwa ajili ya uchunguzi.
“Swala la ajali ya ndege naweza kusema ni suala mtambuka, ni suala ambalo limekaribisha watu wengi. Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi inaendelea na kazi kuhusiana na maswala haya, nini hasa kimesababisha ajali hiyo na nini kinaweza kuja kufanyika baada ya matokeo ya uchunguzi wa ajali hiyo.
“Ajali inapotokea waliotengeneza ndege hizo huwa wanaamka haraka kutaka kujua ajali imetokanana na nini, hivi ninavyozungumza wenzetu Wafaransa ambao ndio wametengeneza ndege hiyo au injini hizo wameshafika katika mkoa wa Kagera na wamefungua vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya maswala ya uchunguzi,” alisema Chalamila.
Kuhusu chanzo cha ajali hiyo, Chalamila alisema tayari hatua za msingi zinaendelea na taarifa ya uchunguzi itakuwa chini ya Wizara na wao watautaarifu umma pale itakapofaa kuhusu chanzo sahihi cha ajali hiyo.
Novemba 9 mwaka huu akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ajali hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari alimtaja Buruhani Rubaga ambaye ndiye alikuwa rubani wa ndege hiyo, kuwa miongoni mwa marubani bora nchini.
Johari alisema hadi ajali hiyo inatokea kapteni Rubaga alikuwa amekusanya saa 23, 515 za kuruka na alikuwa mwanzilishi wa kwenda na ndege kubwa katika uwanja wa Bukoba.
“Hadi ajali inatokea kapteni Rubaga (Buruani) alikusanya saa 23, 515 za kuruka alikuwa ni mmoja wa marubani bora nchini, lakini pia alikuwa mwanzilishi wa kwenda na ndege kubwa katika uwanja wa Bukoba na mwalimu wa marubani wenzake wa namna ya kutua na kuruka katika uwanja ule” alisema Johari