TCAA waonya aliyetengeneza video ajali ya Precision

Ndege ya Precision Air iliyopata ajali Ziwa Victoria Novemba 6, 2022 na kusababisha vifo vya watu 19 na majeruhi 24 ikitolewa kwenye maji.
Muktasari:
- Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini, Hamza Johari amesema timu ya watalaamu wa uchunguzi wa ajali na matukio ya ndege itatoa maelezo ya awali ndani ya siku 14 kuhusu ajali ya ndege ya Precision Air.
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari amesema video ya kubuni inayoonyesha ndege ya Precision ikiwa inakaribia kutua kabla ya kuanguka, ni kinyume cha mkataba wa Chicago huo unaotoa mamlaka ya uchunguzi wa matukio hayo.
Video hiyo imesambaa mitandaoni ikionyesha ndege hiyo ikiyumba angani kabla ya kuanguka kwenye maji.
Johari ameeleza hayo leo, Jumatano Novemba 9, 2022 wakati akizungumza na wanahabari jijini hapa, akisema kazi ya kufanya uchunguzi ni ya kitengo cha uchunguzi wa ndege kilichopo katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
“Jana kuna mtu ametengeneza ‘ghaphics’ yenye video inaonyesha mwenendo wa ndege ya Precision Air hadi ilivyoanguka, hili kosa kwa mujibu wa sheria na amesababisha taharuki, hadi jumuiya za nje zinatushangaa badala ya kuwaachia watalaamu kufanya kazi yao ya uchunguzi,” amesema Johari.
Akizungumzia uchunguzi wa ajali hiyo iliyoua watu 19 na wengine 24 kuokolewa, Johari amesema maelezo ya awali wa uchunguzi wa ajali ya ndege ya Precision Air itatolewa ndani ya siku 14.
Amesema uchunguzi ajali hiyo ulianza tangu siku ilipotokea Novemba 6 mwaka huu na kwa mujibu wa uchunguzi wa ajali na matukio ya ndege za mwaka 2017, Waziri mwenye dhamana ya sekta hiyo anaunda timu ya wataalamu wa kufanya mchakato huo.
Ajali ya ndege ya Precision Air ilitokea Novemba 6 saa 2 asubuhi ambapo ndege hiyo ilianguka katika Ziwa Victoria karibu na uwanja wa ndege wa Bukoba kusababisha vifo vya watu hao na 24 wakinusurika.
“Timu hiyo ipo eneo la tukio imeshaanza kazi na baada ya kukamilisha uchunguzi wao watatoa maelezo ya awali yatatolewa ndani ya siku 14 kwa mujibu wa sheria, labda kuwepo kwa vitu vingine vitakavyowachelewesha.
“Baada ya hapo itafuata ripoti kamili ya uchanguzi itakayotolewa ndani ya siku 30, labda kuwepo na vitu vitakavyowachelewesha, lakini kwa mujibu wa kanuni ya 18 ya sheria ya uchunguzi za ajali za ndege za mwaka 2017 ripoti kamili inatakiwa itolewe ndani miezi 12,” amesema Johari.
Johari amesema ajali hiyo ni miongoni mwa ajali kubwa kwa ndege za abiria.
Amesema ajali kubwa nyingine ya ndege ya abiria ilitokea mwaka 1955 katika kilele cha mlima wa Kilimanjaro ambapo ndege yenye ukubwa wa kubeba abiria 20 ilianguka katika eneo hilo na watu walifariki dunia.
“TCAA inaungana na Watanzania na Rais Samia Suluhu Hassan kutoa pole za dhati kwa familia, wazazi, wenza ndugu jamaa na marafiki na wadau wa sekta ya anga.
“Hadi ajali inatokea kapteni Rubaga (Buruani) alikusanya saa 23, 515 za kuruka alikuwa ni mmoja wa marubani bora nchini, lakini pia alikuwa mwanzilishi wa kwenda na ndege kubwa katika uwanja wa Bukoba na mwalimu wa marubani wenzake wa namna ya kutua na kuruka katika uwanja ule.
“Msaidizi wake kapteni Peter Omondi alikuwa amekusanya saa 2,109, wakati kapteni Rugaba kwa aina ya ndege ile ametumia saa 11,929 wakati msaidizi wake ni saa 1,700 kwa hiyo wanaijua vizuri ruti ile, kilichotekea ni bahati mbaya,” amesema.