Rais Samia afanya uteuzi, yumo Balozi Sirro

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali akimteua IGP mstaafu Balozi Simon Sirro kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Madini la Taifa (Stamico).
Balozi Sirro anachukua nafasi ya Meja Jenerali mstaafu, Michael Isamuhyo ambaye amemaliza muda wake.
Taarifa iliyotolewa leo Aprili 5, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi Dk Moses Kusiluka, imesema Rais amemteua Profesa John Kondoro kuwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), akichukua nafasi ya Profesa Makenya Maboko ambaye amemaliza muda wake.
Profesa Emanuel Mjema ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kwa kipindi cha pili.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga imesema mhandisi Mwanasha Tumbo ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), akichukua nafasi ya Profesa Esnat Chaggu aliyemaliza muda wake.
Rosemary Silaa ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Bohari ya Dawa (MSD) kwa kipindi cha pili.