Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Mwinyi sasa achoka kuandamwa

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi

Muktasari:

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametema nyongo kuhusu mambo saba aliyosema yamekuwa yakipotoshwa kwa makusudi ili kumkatisha tamaa, lakini akasisitiza kuwa hatarudi nyuma hata hatua moja.

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametema nyongo kuhusu mambo saba aliyosema yamekuwa yakipotoshwa kwa makusudi ili kumkatisha tamaa, lakini akasisitiza kuwa hatarudi nyuma hata hatua moja.

Dk Mwinyi alitoa kauli hiyo jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika utaratibu wake wa kuzungumza nao kila mwisho wa mwezi, huku akitaja makundi matatu yanayofanya upotoshaji huo.

Kwa mujibu wa Rais Mwinyi, kundi la kwanza ni la kisiasa, kundi la pili ni la watu aliosema wamezibiwa mirija yao ya alichokiita upigaji wa fedha, huku kundi jingine akisema analihifadhi.

Alisema kinacholeta shida kwa makundi hayo yanayompinga ni hofu ya kuingia kwenye mambo mapya wanayoona yanafanyika kwa sasa.

“Nimeamua kuyasema hayo ili kuweka rekodi sawa…nimevumilia sana ila nikaona leo niseme kidogo,’’ aliwaeleza wanahabari katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.


Ataja maeneo ya upotoshaji

Eneo la kwanza lililotajwa na Rais Mwinyi akisema linapotoshwa, ni ukodishwaji wa visiwa akisema jambo hilo limekuwa likisemwa tofauti na uhalisia.

“Serikali imeamua kukodisha visiwa vidogo 52 na mpaka sasa tayari visiwa 10 vimeshapata wawekezaji, lakini watu wanapotosha kwamba Serikali imeuza visiwa hivyo, jambo ambalo halina uhalisia,” alisema

Aliongeza; “Uhalisia ni kwamba tumewekeza kwa kuangalia uwezo wa mwekezaji, kiasi atakachotanguliza kwa Serikali na kiasi cha mtaji alionao. Na kuweka sawa ukodishwaji wa visiwa haujaanza kwenye Serikali hii, sema sisi tumeboresha zaidi na wananchi watanufaika,” alisema.

Ufafanuzi huo wa Dk Mwinyi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, umekuja kufuatia mjadala miongoni mwa Wazanzibari, akiwamo aliyekuwa kada maarufu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Baraka Shamte, ambaye hivi karibuni alionekana katika kipande cha video akimtuhumu Rais huyo kwa mambo mbalimbali, ikiwamo ukodishwaji wa visiwa. Hata hivyo, siku chache baadaye, Shamte aliomba radhi kwa kauli alizotoa dhidi ya Rais.

Sula la ukodishwaji wa visiwa, pia liliwahi kuelezwa na mbunge wa zamani wa Malindi, Ally Saleh katika ukurasa wake wa Facebook, akisema hana shida na suala la ukodishwaji wa visiwa kwa miaka 99, lakini hoja yake iko kwenye visiwa ambavyo vinakaliwa na watu.

Akifafanua maelezo hayo baada ya kupigiwa simu na Mwananchi, Saleh alisema: “Visiwa ambavyo havina watu, mimi niko okay (sina tatizo navyo), isipokuwa kisiwa cha Misali. Hoja yangu kwenye kisiwa cha Misali ni sehemu nzuri, ni kama Ngorongoro ya baharini, ni kama Loliondo ya baharini, jinsi kilivyo na rasilimali.’’

Saleh aliongeza kwamba ukijenga hoteli kwenye kisiwa hicho, maana yake shughuli za kibinadamu zitaongezeka na hatimaye matumbawe yatakatwa, samaki watakimbia na mazalia ya samaki yatatoweka.


Kuhusu Mji Mkongwe

Jambo lingine lililotolewa ufafanuzi na Dk Mwinyi ni ukarabati unaofanywa katika mji Mkongwe, akisema kwa jinsi mji huo ulivyo hivi sasa ukiachwa kama ulivyo, hauwezi kufika miaka 100 ijayo, hivyo Serikali imeamua kutafuta wawekezaji kwa ajili ya kufanyia marekebisho.

“Lakini kinachoongelewa ni tofauti na uhalisia. Tumesema kama mtu anaweza kufanya marekebisho mwenyewe bila kuathiri uhalisia wake, afanye lakini kwa mtu ambaye hawezi tunawapa wanaoweza, lakini yakifanyiwa marekebisho watapewa kipaumbele waliokuwamo awali,” alieleza Rais.


Viwanja vya michezo

Kuhusu viwanja vya michezo, ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakidai kuwa vinachukuliwa na kuuzwa kinyemela, Dk Mwinyi alivitolea ufafanuzi kwa kueleza: “Naambiwa kuwa navichukua viwanja vyote vya michezo nawapa wafanyabiashara. Lakini ukweli ni kwamba kwa sasa tunahitaji viwanja vya kisasa sio hivi tulivyonavyo na vile vinavyochukuliwa, tunawatengenezea viwanja vya kisasa”.

Alitolea mfano wa kiwanja cha michezo cha Malindi, akisema kiwanjani hapo kutajengwa maegesho ya kisasa kwa ajili ya eneo maarufu la biashara la Darajani, huku akisema lengo na dhamira ni kupata wawekezaji wazuri.


Miradi ya ujenzi

Dk Mwinyi alisema kumekuwapo na kauli nyingi kwamba miradi inayojengwa zabuni zake hazitangazwi, na kwamba amekuwa akiwapa marafiki zake. Hata hivyo, alisema kilichopo ni kwamba miradi mingi ni ile ambayo Serikali imeingia ubia na sekta binafsi.


Uwanja wa ndege

Kuhusu Serikali kuingia makubaliano na kampuni ya kimataifa ya Dnata kuendesha uwanja wa ndege kisasa, alisema yamekuwapo maneno mengi, wakiwamo watu wanaohoji kwa nini kazi hiyo isikabidhiwe kwa wazawa.

Hata hivyo, Rais Mwinyi alidai hilo haliwezekani, kwa sababu hakuna mzawa anayeweza kufanya uwekezaji kama huo.

“Zanzibar tunategemea utalii, ambao unaanzia kwenye uwanja wa ndege, kwa hiyo tunahitaji kampuni kubwa na tunahitaji huduma za kisasa, hakika kwa wanaotembea hakuna asiyejua uwezo wa kampuni hii duniani,” alisema.


Madai ya Serikali kufanya biashara

Kuhusu madai ya Serikali kuanza kufanya biashara, Rais Mwinyi alisema kikubwa kinachofanyika ni kufanya kazi na sekta binafsi na sio kuingiza Serikali kwenye biashara kama inavyodaiwa.

“Nchi inajengwa kwa fedha za Serikali, washirika wa maendeleo na sekta binafsi. Na sisi kipaumbele chetu tumesema lazima tufanye kazi na sekta binafsi na tutazidi kuwapa kipaumbele lakini sio Serikali kufanya biashara.”

Katika hili alitolea mfano wa kilomita 273 zitakazojengwa vijijini, ambazo Serikali imeingia mikataba na sekta binafsi katika ujenzi wake.