Raia wa Ukraine kortini kwa kukutwa na Kobe 116

Raia wa Ukraine, Orga Kryshtopa( kushoto) akisindikizwa na Askari kanzu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa kesi ya uhujumu uchumi. Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Kryshtopa anadaiwa kukamatwa na Kobe hao Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Dar es Salaam. Raia wa Ukraine, Orga Kryshtopa, amefikishwa katika Mahakamani ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kusafirisha Kobe 116 wenye thamani ya Sh18.9 milioni, bila kuwa na kibali.
Kryshtop amefikishwa Mahakama hapo na kusomewa mashtaka yake na Wakili wa Serikali, Judith Kyamba, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Amir Msumi.
Kabla ya kusomewa mashtaka yake, Hakimu Msumi alimueleza mshtakiwa kuwa hatakiwi kujibu chochote mahakamani hapo kutoka na kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali cha DPP.
Akimsomea mashtaka yake, Wakili Kyamba amedai kati ya Januari Mosi hadi Julai 30 2022 jijini Dar es Salaam, mshitakiwa alijihusisha na nyara za serikali kwa kununua, kuuza na kusafirisha kobe 116 wenye thamani ya Sh18.9 milioni mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Shtaka la pili, inadaiwa katika tarehe hizo, eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) uliopo Wilaya ya Ilala, Kryshtop alikamatwa akiwa na kobe hao bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyama Pori nchini.
Upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo wanaomba terehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Msumi ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 28, 2023, ambapo upande wa mashtaka unatarajia kuongeza mshtakiwa mwingine.
Mshtakiwa amerudishwa rumande hadi tarehe hiyo.