Radi yaua mmoja akikinga maji, mtaalamu aeleza mbinu kujikinga

Suna Mpongoja enzi za uhai wake.
Muktasari:
- Mkazi wa Kitongoji cha Uvihangani Kata ya Marui,wilaya ya Kisarawe, Suna Mpongoja, amefariki dunia baada ya kupigwa na radi alipokuwa akiteka maji.
Kisarawe. Mkazi wa Kitongoji cha Uvihangani Kata ya Marui, Wilaya ya Kisarawe, Suna Mpongoja, amefariki dunia baada ya kupigwa na radi.
Akizungumza jana Ijumaa Machi 15,2024, Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Salimu Muadi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo jana saa tisa za jioni ambapo marehemu alikuwa akikinga maji ya mvua nyumbani kwake.
"Huyu mwananchi alikuwa anakinga maji pembezoni mwa msingi wa nyumba yake na hapo ndipo akakutwa na radi iliyompiga na kufariki papo hapo licha ya kutoonekana kuwa na jeraha lolote mwilini mwake,"amesema mwenyekiti huyo.
Muadi amesema marehemu tayari ameshazikwa katika mashamba ya kitongoji hicho. Kutokana na tukio hilo, mwenyekiti huyo ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari kutokana na mvua hizo ambazo bado zinaendelea kunyesha.
"Pamoja na kwamba tunasema ni kazi ya Mungu, lakini nasi wananchi tunapaswa kuchukua tahadhari pindi mvua zinaponyesha na tunapoona radi inapiga kwa kuwa ni matukio yanayokuja bila ya taarifa, "amesema.
Baba wa marehemu, Adam Mkongoja, amesema Suna amefariki akiwa ameacha watoto wawili, mmoja akiwa na miaka nane na mwingine miaka mitatu.
Mkongoja amesema marehemu alikuwa ni mtoto wake wa pili kati ya watoto watano aliojaliwa kuwapata, na kwamba kifo chake hicho kimemsikitisha.
Wito wake kwa mamlaka zinazohusika na maafa ni kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya radi na namna ya kujikinga nayo kwa kuwa hata wao wangekuwa na elimu hiyo, huenda wangemkataza marehemu asiende kukinga maji.
Radi ni nini, namna ya kuiepuka
Mtaalamu na mchambuzi wa hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA), Rose Senyagwa, amesema radi ni umeme unaotoka katika wingu linalojulikana kama wingu ng'amba.
Rose amefafanua zaidi kuwa aina hii ya wingu kwa kawaida hufanyika baada ya jua kali kupiga katika ardhi yenye unyevunyevu wa kutosha au vyanzo vya maji kama bahari, mito na maziwa.
"Kiasi kikubwa sana cha unyevunyevu huvukizwa ( mvuke) na kusafirishwa angani, na kutengeneza wingu zito lenye barafu ndani yake lijulikanalo kama wingu ng'amba.
"Wingu hili likiwa na uzito wa kutosha, mvua kubwa huanza kunyesha. Wingu hili pia hutoa chaji za umeme wakati mabarafu ndani ya mawingu yakigongana angani,"amesema Rose na kuongeza chaji hizi zinaweza kusafiri kutoka kwenye wingu moja hadi lingine, au zikaenda juu zaidi angani au zikatoka kwenye wingu hadi ardhini.
Ameendelea kueleza kuwa chaji zinazosafiri kuja ardhini ndizo huleta madhara makubwa na zinapokutana na kitu chochote mfano, miti, minara, wanyama, binadamu husababisha madhara ikiwemo vifo.
"Kwa kawaida chaji hizi hufuata vitu virefu kama miti mirefu au minara. Kunapokuwa na radi tunashauriwa kuepuka kukaa chini ya miti, minara mirefu,’’ amesema.
Ili kujikinga na madhara yake, Rose amesema unapaswa kuepuka kutumia vitu kama simu au vitu vya kielektroniki wakati wa radi.
Pia mtaalam huyo amesema ni vizuri kuepuka kutembea au kuogelea kwenye vyanzo vya maji kama mito, bwawa na hata kukanyaga maji yanayotiririka barabarani kwani yanaweza yakasafirisha umeme wa radi na kusisitiza kuwa ni vizuri kukaa ndani ya nyumba kwa utulivu wakati wa radi.
Kuhusu mwananchi aliyefikwa na umauti kutokana na radi amesema inawezekana imempiga moja kwa moja yeye kwa sababu alikuwa nje wakati radi inapiga au maji yaliyokuwa yanatiririka yana chaji za umeme ndio yamempiga shoti.