Afariki kwa kupigwa na radi akitokea mazikoni

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, ACP Nicodemus Katembo
Muktasari:
- Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, ACP Nicodemus Katembo amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kuwasihi wananchi kuendelea kuchukua tahadhari hasa kipindi hiki cha mvua.
Mtwara. Mkazi wa Kijiji cha Mtimbwilimbwi katika Halmashauri ya Mji Nanyamba, mkoani Mtwara, Dadi Linyata amefariki dunia kwa kupigwa na radi akitokea mazikoni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, ACP Nicodemus Katembo amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kuwasihi wananchi kuendelea kuchukua tahadhari hasa kipindi hiki cha mvua.
Awali akizungumza na Mwananchi Digital leo Januari 23, 2024, makamu mwenyekiti kijiji hicho, Jamal Nalyogo amesema siku ya tukio Linyata alikuwa akitokea kwenye maziko na baada ya mvua kunyesha alisimama kujikinga kibarazani na ndiporadi ilipompiga.
“Marehemu alikuwa anatokea mazikoni, mvua kubwa ilinyesha ghafla na alikimbia kibarazani ili ajikinge, lakini ghafla ilipiga radi na kusababisha watu wanne kujeruhiwa na yeye alionekana kuwa na hali si nzuri, hivyo akakimbizwa hospitalini,” amesema Nalyongo.
Kwa upande wake, Baraka Mwema, mkazi wa kijiji hicho, amesema: “Nilikuwa mmoja wapo kati ya watu waliojikinga na mvua, nilikuwa karibu na mlango, ile radi ilitukuta hapo na kutupiga, sijaumia wala sijajeruhiwa, ingawa nilipata kama ganzi, lakini baadaye nilipata nafuu ingawa bega la kushoto lilivimba.”
Naye Hamisi Baisa (mjomba wa marehemu) amesema: “Tulikuwa makaburini baada ya maziko mvua ikanyesha tukakimbia kujikinga na hapo ndipo radi ilipiga kwa nguvu, mmoja wetu alidondoka akarushwa mbali, tulimuwahisha hospitali lakini tuliambiwa kuwa tayari amefariki.”