Profesa Mkumbo: Tiseza italeta ufanisi zaidi

Muktasari:
- Wawekezaji watakuwa na uwezo wa kupata huduma katika eneo moja tofauti na zamani walipokuwa wakienda ofisi mbili.
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema kuanzishwa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (Tiseza) kunalenga kuwaondolea wawekezaji usumbufu.
Amesema sasa wawekezaji watakuwa na uwezo wa kupata huduma katika eneo moja tofauti na zamani walipokuwa wakienda ofisi mbili.
Profesa Kitila amesema hayo leo Jumamosi Julai 5, 2025 alipotembea banda la Tiseza na kuzungumzia maonyesho hayo ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF).
Amesema anaamini kuunganishwa kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Kukuza Mauzo ya Bidhaa Nje ya Nchi (EPZA) kutaongeza ufanisi katika kuvutia wawekezaji na kuwahudumia kwa urahisi.
“Hii itapunguza usumbufu kwa wawekezaji kwani tukiwa na taasisi moja mwekezaji akifika pale anamaliza kila kitu. Tunaenda kuvutia uwekezaji mkubwa wa ndani na nje ya nchi,” amesema.
Tiseza ilianza rasmi Julai mosi mwaka huu baada ya Bunge kutunga sheria ya kuunganisha mamlaka hizo mbili kabla ya kuanza utekelezaji wake mwaka huu.
Tiseza ilianzishwa kufuatia kutungwa kwa Sheria ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Na. 6 ya Mwaka 2025.
Haya yanasemwa wakati ambao tayari Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Gilead Teri kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tiseza akitoka kuwa Mkurugenzi Mtendaji TIC.
Februari 13, 2025, Bunge lilipitisha Muswada wa Sheria ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi, hatua iliyolenga kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
Alipokuwa akiwasilisha muswada huo, Profesa Mkumbo alisema mabadiliko hayo hayaathiri shughuli za uwekezaji zinazoendelea, bali yataimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji nchini na kusaidia kukuza uchumi kupitia uwekezaji wa kimkakati.
Mmoja wa wafanyabiashara, Samia Nshala amesema anatamani kuona kuunganishwa kwa mamlaka hizo kunaleta ufanisi zaidi.