Bajaji za umeme Sabasaba zilivyorahisisha usafiri

Muktasari:
- Bajaji zanapatikana kwa Sh5,000 kwa safari ya dakika 30 au Sh2,000 kwa safari ya kawaida kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Dar es Salaam. Pikipiki za umeme za magurudumu matatu (bajaji) zilizoanza kutumika kwa mara ya kwanza katika Maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), zimerahisisha usafiri kwa wageni na washiriki huku zikihamasisha matumizi ya nishati safi na kukuza utalii wa jiji.
Tofauti na miaka iliyopita, wageni walitegemea huduma zisizo rasmi na zisizo na uhakika za usafiri wa ndani, maonyesho ya mwaka huu yameleta usafiri wa kisasa wa umeme kama mbadala.
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), kwa kushirikiana na Shirika la Posta Tanzania (TPC) na wadau binafsi, imeanzisha huduma hiyo ili kurahisisha mtu kutoka eneo moja kwenda lingine.
Kwa mujibu wa TPC, kuna zaidi ya pikipiki 20 na gari ndogo za kubeba mizigo na mabasi ya kifahari kwa ajili ya viongozi waandamizi.
Pikipiki hizi zanapatikana kwa Sh5,000 kwa safari ya dakika 30 au Sh2,000 kwa safari ya kawaida kutoka sehemu moja hadi nyingine, huku magari yakibeba mizigo au bidhaa za ununuzi.
“Hii ni nafuu kubwa,” amesema Diana Matiko, mshiriki kutoka Mwanza. “Miaka ya nyuma nilibeba bidhaa zangu kutoka getini hadi banda langu. Sasa kwa e-trikes kila kitu ni rahisi, naweza kuzingatia biashara yangu.”
Familia, wazee na watu wenye ulemavu pia wananufaika na huduma hiyo.
Mtembeleaji mwingine Joseph Mussa kutoka Bahari Beach amesema magari haya yameboresha uzoefu wake.
“Maonyesho ni makubwa na kutembea na watoto ni kazi kubwa. Huduma hii ni nafuu na bora.”

Waendeshaji wanasema mahitaji yamekuwa makubwa tangu maonyesho kufunguliwa.
“Tumejaa siku nzima,” amesema dereva Khafan Musa na kuongeza.
“Tunabeba watu na mizigo, Washiriki wanapendezwa kwa sababu inaokoa muda.”
Mkuu wa Banda la TPC, Khamis Swedi amesema kuanzishwa kwa magari haya ya umeme ni sehemu ya jitihada za mamlaka hiyo kuhamasisha ubunifu wa kijani.
Amesema lengo lao si tu kutoa urahisi, bali pia kuunga mkono ajenda ya Serikali ya nishati safi na wanataka huduma hiyo iwe ya kudumu katika DITF.
Magari haya yameonekana kuwa miongoni mwa ubunifu unaothaminiwa zaidi katika maonesho ya mwaka huu yanayoendelea kuvutia maelfu ya washiriki wa ndani na wa kimataifa.
“Tumeleta ubunifu huu ili kurahisisha usafiri kwenye maonesho. Nauli ni nafuu, bajaji ni ya umeme haina kelele, hivyo inafikika kirahisi na inaendana na ajenda ya nishati safi,” amesema Swedi.
Maonyesho ya mwaka huu yanatarajiwa kufunguliwa rasmi Julai 7 na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi tofauti na miaka iliyopita ambapo yalikuwa yakizinduliwa mapema zaidi.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amesema jambo kubwa mwaka huu litakuwa uzinduzi rasmi wa nembo ya “Made in Tanzania,” kama mpango wa kitaifa wa kutangaza bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.