PPRA kumaliza changamoto ya mfumo wa manunuzi

Muktasari:
- Mfumo huo wenye lengo la kuongeza ufanisi katika sekta ya manunuzi, kudhibiti rushwa na kurahisisha mchakato wa zabuni kwa uwazi ulianza kufanya kazi octoba mwaka huu lakini umeonekana kuwa changamoto kwa maofisa manunuzi kwenye taasisi mbalimbali za umma na binafsi.
Arusha. Kutokana na malalamiko mengi ya changamoto juu ya mfumo mpya wa manunuzi wa kielekroniki (NeST), Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeanza kuwanoa Wataalamu wa ugavi kuufahamu vema na jinsi ya kukutumia.
Mfumo huo wenye lengo la kuongeza ufanisi katika sekta ya manunuzi, kudhibiti rushwa na kurahisisha mchakato wa zabuni kwa uwazi ulianza kufanya kazi Oktoba mwaka huu lakini umeonekana kuwa changamoto kwa maofisa manunuzi kwenye taasisi mbali mbali za umma na binafsi.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mafunzo ya maafisa ugavi na ununuzi kutoka wakala wa misitu Tanzania (TFS), leo Desemba 11,2023 mkufunzi kutoka PPRA, Jones Mapunda amesema kuwa changamoto za mfumo huo unatokana na wahusika kutoufahamu.
"Tuko katika mafunzo kwa maofisa ugavi na ununuzi kwenye sekta ya umma ambao tunawafundisha, namna ya kutafsiri sheria ya manunuzi na kuitekeleza kwa kuzingatia mfumo mpya wa ununuzi wa kieletroniki uliopitishwa na serikali hivi karibuni." amesema Mapunda.
Amesema mbali na hilo pia wanawafundisha jinsi ya kutathimini mikataba ya ununuzi na namna ya kuitekeleza kwa kufuata taratibu zote za kizabuni.
"Sheria ya manunuzi namba 10, ya mwaka 2023 iliyosainiwa na kuanza kutumika octoba 6, 2023 inataka matumizi ya mfumo mpya wa manunuzi wa kielekroniki (NeST) ndio utumike hasa kwenye taasisi za umma kwenye mambo yote ya uzabuni na ununuzi sio kutumia tena makaratasi" amesema Mapunda.
Ameeleza kuwa hata hivyo kumekuwa na changamoto kwa watekelezaji ndio maana wanatoa mafunzo hayo ili kuwawezesha utekelezaji wa sera, dira na makusudio ya taasisi iliyowekwa.
Awali akifungua mafunzo hayo, kaimu kamishna wa TFS, Emmanuel Wilfred aliwataka maofisa hao kuzingatia elimu wanayopewa ili wasaidie taasisi katika utekelezaji wa melengo yake katika sekta ya manunuzi.
"Sekta ya manunuzi inachukua zaidi ya asilimia 75 ya bajeti ya taasisi hivyo isaidieni katika kutimiza malengo yake kwa kuhakikisha mnafata misingi ya manunuzi mkitanguliza uzalendo na maadili" ameeleza Emmanuel.
Naye, meneja manunuzi na ugavi kutoka TFS, Fridoline Matembo amesema changamoto kubwa iko katika mfumo huo hivyo kuomba taasisi yake iendelee kutenga bajeti za kusaidia mafunzo kama hayo ili waweze kuisaidia taasisi kufikia dira na malengo iliyojiwekea.
"Huu mfumo ni mpya ndio maana Kuna baadhi ya taratibu zinashindwa kufanyika ndani yake kutokana na kutoufahamu na mkwamo mkubwa uko kwenye mtiririko wa uzabuni hivyo tusaidiwe mafunzo ya mara kwa mara naamini tutaufahamu na utakuwa rahisi kuutekeleza " amesema Matembo.