Mikataba ya manunuzi kuonekana ndani ya mfumo

Muktasari:
- Serikali inakamilisha ujenzi wa mfumo mpya wa manunuzi kwa njia ya mtandao (NeST) ambapo pamoja na mambo mengine utaweka uwazi kwenye eneo hilo.
Dodoma. Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) amesema moduli ya kusimamia mikataba iliyomo katika mfumo mpya wa manunuzi wa NeST itakamilika mwishoni mwa mwaka 2023.
Hayo yamesemwa leo Julai 17,2023 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Eliackim Maswi wakati akitoa taarifa ya utekelezaji na mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo kwa mwaka 2023/24.
“Moduli ya kusimamia mikataba inataka lazima mikataba yote (ya manunuzi) tunayoifanya ionekane katika mfumo ili hata ukifanya mabadiliko ya vitu na bei ionekane katika mfumo. Tunategemea ikamilike kabla ya mwisho wa mwaka huu,”amesema.
Amesema lengo la kujenga mfumo huo wenye moduli sita, ni kuongeza uwazi kwenye ununuzi wa umma, usizi mzuri wa fedha za uma, kudhibiti vitendo vya rushwa na ufuatiliaji wa ukidhi wa sheria na uwajibikaji wa ununuzi,” amesema.
Aidha, amesema katika mfumo huo mpya ambao moduli zake mbili zimekamilika zimeanza kutumiwa na tangu Julai Mosi mwaka huu.
Maswi ametaja moduli nyingine ni E-Auction ambao unalenga katika kwenda kuongeza wazi kwenye mashindano kwa kuweka bei ya bidhaa na huduma ambazo watu wataweza kuziona huku moduli ya E-cataloge ikiweka wazi vitu walivyonavyo wazabuni na kutoa mawanda mapana ya uchaguzi.