Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

PPAA ilivyozuia zabuni 36 kwa kukosa vigezo

Muktasari:

  • Hatua hiyo, kwa mujibu wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), imewezesha kukoa utekelezaji usioridhisha wa miradi ya maendeleo na upotevu wa fedha za umma.

Dar es Salaam. Katika kipindi cha miaka minne kuanzia Machi 2021/25, Serikali ilizuia utoaji tuzo za zabuni 36 kwa wazabuni wasio na vigezo ikiwemo uwezo wa kifedha pamoja na sifa za kutekeleza miradi husika.

Hatua hiyo, kwa mujibu wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), imewezesha kukoa utekelezaji usioridhisha wa miradi ya maendeleo na upotevu wa fedha za umma.

Idadi hiyo ya tuzo za zabuni zilizozuiliwa, ni sehemu ya mashauri 171 yaliyotokana na michakato ya ununuzi wa umma yaliyoshughulikiwa na PPAA kama inavyoonyesha katika ripoti yake.

Katika taarifa yake, Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando amesema utekelezaji wa hayo umefanywa kwa kuzingatia falsafa ya R4 za Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema wanaamini usuluhishi wa migogoro hauwezi kupatikana penye ubaguzi na pale ambako kuna wanaokosa fursa na haki zao za kiuchumi na kiraia.

"Kwa PPAA kuzuia utoaji wa tuzo kwa wazabuni hao waliokosa sifa kinaweka uzito katika usuluhishi wa migogoro ambayo ni moja kati ya falsafa za Rais Samia," amesema.

Sambamba na hilo, amesema wanaendelea kudhibiti taasisi za ununuzi zinazokiuka taratibu za kisheria hasa katika kufanya tathmini ya zabuni.

Katika baadhi ya mashauri hayo, walibaini ukiukwaji wa taratibu za tathimini uliofanywa na taasisi za ununuzi ikiwemo kutozingatia vigezo vilivyowekwa katika kabrasha la zabuni au kuongeza vipya ambavyo havikuwepo awali.

Katika kipindi hicho, Sando amesema Serikali imewezesha kutungwa upya kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na kuruhusu hatua za mageuzi kuchukuliwa pale ilipobainika kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu katika mchakato wa ununuzi.

Kutokana na mageuzi hayo, amesema muda wa ushughulikiaji malalamiko au rufaa zinazotokana na michakato ya ununuzi wa umma umepungua kutoka siku saba hadi tano.

"Muda huo hautajumuisha njia za ununuzi ambazo hazihitaji ushindani, pia muda wa ofisa masuhuli kushughulikia malalamiko ya zabuni nao umepunguzwa kutoka siku saba za kazi hadi siku tano,” amesema.

Amesema sheria hiyo imeweka masharti ya lazima kwa taasisi nunuzi kufanya ununuzi kupitia mfumo wa kielektroniki na matumizi ya Tehama kwa moduli ya kielektroniki.

Katika kipindi hicho pia, amesema Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma zilitungwa.

Ili kuwezesha matumizi ya Moduli kwa ufasaha, Mamlaka ya Rufani iliweza kufanya mafunzo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa washiriki kutoka katika taasisi nunuzi na wazabuni 913 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro na Pwani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. Kanda ya Ziwa ikiwemo Mwanza, Shinyanga, Kagera, Musoma, Geita na Simiyu yaliyofanyika mapema Februari, 2025 jijini Mwanza yakiwahusisha maofisa ununuzi, wakuu wa vitengo vya ununuzi, wakuu wa vitengo vya sheria, maofisa sheria, maofisa Tehama, mawakili na wazabuni.

Kuhusu falsafa ya kujenga upya, amesema wameboresha usimamizi wa sekta ya ununuzi wa umma, hatua ambayo imewajengea uwezo wajumbe na watumishi na kuboresha mazingira ya kazi kwa kuwapatia vifaa muhimu.

Pamoja na athari za kiuchumi zilizoikumba na zinazoendelea kuikumba dunia na kutikisa uchumi kama Uviko 19, vita ya Russia na Ukraine pamoja na kuadimika dola za Marekani, amesema Serikali imeendelea kuiwezesha PPAA kustahimili athari hizo na kutekeleza majukumu yake ipasavyo.