Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

PPAA yaokoa Sh543 bilioni kwa wazabuni wasio na sifa

Naibu waziri wa Fedha, Hamad Chande akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya Mosuli ya kupokea na kushughulikia malalamiko kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa Manunuzi kielektroniki (NesT) jijini hapa leo.

Muktasari:

  • Wazabuni 27 walibainika kutokuwa na sifa za kutekeleza miradi ya manunuzi waliyokuwa wameomba na iwapo wasingebainika, Serikali ingepoteza zaidi ya Sh543.03 bilioni.
no

Dar es Salaam. Zaidi ya Sh543.03 bilioni zimeokolewa baada ya Serikali kuzuia utoaji wa tuzo kwa wazabuni 27 wasio na uwezo wa kifedha na waliokosa sifa za kitaalamu za kutekeleza zabuni za miradi mbalimbali nchini.

Fedha hizo zimeokolewa ndani ya miaka mitatu ikiwa ni baada ya Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) kushughulikia mashauri 129 yaliyowasilishwa kwao.

Mamlaka ya Rufani ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Fedha ikiwa na jukumu la kupokea, kusikiliza na kutoa maamuzi ya malalamiko au rufaa zitokanazo na maamuzi ya Maofisa Masuuli wa taasisi mbalimbali katika michakato ya ununuzi wa Umma.

Pia mamlaka hiyo ina jukumu la kupokea na kusikiliza malalamiko ya wazabuni ambao hawakuridhishwa na uamuzi wa kufungiwa (blacklist) na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

Hayo yameelezwa leo, Mei 29, 2024 katika mafunzo ya moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko kupitia mfumo wa Ununuzi wa Kieletroniki (NeST) kwa wataalamu walio chini ya PPRA na PPAA.

Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma, James Sando amesema katika mashauri yaliyosikilizwa na kutolewa uamuzi, Mamlaka ya Rufani imedhibiti  utoaji wa tuzo kwa wazabuni ambao walipendekezwa kupewa bila kuwa na sifa stahiki.

“Mamlaka ya Rufani ilizuia utoaji tuzo kwa wazabuni 27 wasio na uwezo wa kifedha pamoja na wale waliokosa sifa za kitaalamu za kutekeleza zabuni husika,” amesema Sando.

Amesema asilimia 23 ya mashauri 129 yaliyosikilizwa katika kipindi hicho, yalibainika kuwa na kasoro mbalimbali katika mchakato wake wa ununuzi na endapo mashauri hayo yasingeshughulikiwa Serikali ingepoteza Sh543.03 bilioni.

Amesema kama mamlaka imeendelea kudhibiti ukiukwaji wa taratibu za kisheria hasa katika kufanya tathimini ya zabuni huku akieleza kuwa katika baadhi ya mashauri, ilifanikiwa kubaini ukiukwaji wa taratibu za kufanya tathimini ikiwemo kutokuzingatiwa kwa vigezo vilivyowekwa katika kabrasha la zabuni au kuongezwa kwa vigezo vipya ambavyo havikuwepo awali.

Awali akifungua mafunzo hayo, Naibu waziri wa Fedha, Hamad Chande ameitaka PPAA kushirikiana na Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) katika maamuzi wanayotoa ili PSPTB iweze kuwachukulia hatua stahiki wataalamu wake wanaokiuka maadili ya taaluma yao.

“Pia bodi ya PSPTB ihakikishe kuwa wataalamu wa ununuzi na ugavi wanasajiliwa na kufanya majukumu yao kwa weledi. Kwa upande wa taasisi nunuzi zote nchini, zinatakiwa kuwa na wataalamu wa ununuzi na ugavi waliosajiliwa na PSPTB,” amesema Chande.

Amesema ikiwa taasisi nunuzi zitaajiri wataalamu ambao hawajasajiliwa na bodi zinapaswa kutambua kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria na watakapobainika watachukuliwa hatua.