Polisi yatangaza msako wa madada poa vyuoni

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga akizungumza na wanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo kikuu Mzumbe Kampasi ya Mbeya leo Alhamis Novemba 2, 2023. Picha na Hawa Mathias
Muktasari:
- Kauli hiyo imetolewa leo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga Leo Alhamisi, Novemba 2, 2023 wakati akizungumza na wanafunzi 1,500 wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Mbeya.
Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limesema limeanza oparesheni maalumu ya kuwasaka wanafunzi wa kike wanaojiuza katika vyuo vikuu na wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja kwenye kumbi za starehe na eneo la mataa ya kuongozea magari.
Oparesheni hiyo itahusisha wamiliki wa nyumba walizopanga kwa ajili ya kufanya biashara hizo nje ya vyuo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema Alhamisi, Novemba 2, 2023 wakati akizungumza na wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Mzumbe kampasi ya Mbeya.
Amesema Mkoa wa Mbeya kumeibuka na tabia hiyo kwa wanafunzi wa vyuo kufanya biashara za ngono, akionya kuwa watawakamata watakaobainika.
“Tunayafahamu maeneo yote wanayofanya hizo biashara zao. Ni jambo la kusikitisha wazazi wanajua vijana wanapata elimu, kumbe wao wamekuja kujiuza kwa kufanya vitendo vichafu,” amesema.
Kuzaga amesema kuwa msako huo hautawaacha salama, wahusika na wateja wao kwani umefika wakati vijana wa kiume wameharibika kwa kushindwa kujizuia huku wakilaghaiwa na chipsi mayai, kuku pindi wanapokuwa wameishiwa fedha za matumizi vyuoni.
“Wanaume acheni tabia hizo fuateni elimu na wanawake pia acheni kujiuza mnapokula chipsi mayai za watu mnatarajia nini kinafuata ndio hayo ya kufanyiwa vitendo vya kugeuzwa na kushindana na wanawake,” amesema.
Wakati huo huo ameonya wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe kuachana na vitendo vya uhalifu na kwamba kuna ripoti nyingi ambazo zimefunguliwa zikiwahusisha katika kituo cha Polisi.
Kwa upande wake mlezi wa Wanafunzi Chuo Kikuu cha Mzumbe Kampasi ya Mbeya, Florence Kalimbikulu amesema kuna watu wenye magari ya kifahari wamekuwa wakiwafuta wanafunzi na kusababisha kukamatwa mara kwa mara na askari wa doria usiku wa manane sijui wanakuwa wanatoka wapi na kufanya nini.
“Kamanda tunashukuru kwa ujio wako kuna watu wananyemelea watoto wangu, sijui wanawafanya nini kuna wakati napigiwa simu usiku wa manane kuwa kuna vijana wamekamatwa wakifanya vitu ambavyo havipendezi kwa kweli tunaomba msaada wako,” amesema.
Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Jamii na kaimu Mkuu wa Chuo, John Jorojick ameonya wanafunzi waliopata fursa ya masomo kwa mwaka wa kwanza kuepuka vitendo viovu ikiwepo ushoga, kujiuza miili na uharifu.
“Kuna wanafunzi 1,500 wa mwaka wa kwanza katika fani mbalimbali pia tuombe hali ya usalama kuimarishwa katika eneo la chuo kwani kipindi cha likizo kuna kuwa hakuna matukio ya uharifu lakini tukifungua uharifu unakuwa mkubwa ambao baadhi ya wanafunzi kuhusishwa,”amesema.
Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Jeshi la Polisi, Loveness Mtemi amesema kwenye taasisi za elimu ya juu kuna changamoto lukuki za ukatili wa kijinsia na kuwataka wanafunzi wa mwaka wa kwanza kutoa taarifa pindi yanapojitokeza na kuathiri masomo yao.