Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Viongozi, wananchi watangaza vita mpya dhidi ya ‘dada poa’ Dodoma

Muktasari:

  • Unaweza kusema ni vita kati ya wakazi wa Mtaa wa Samora, ambao wameunda kikosi kazi kupambana na wanawake wanaofanya biashara ya ngono kwenye mtaa huo.

Dodoma. Unaweza kusema ni vita kati ya wakazi wa Mtaa wa Samora, ambao wameunda kikosi kazi kupambana na wanawake wanaofanya biashara ya ngono kwenye mtaa huo.

Kuundwa kwa kikosi kazi hicho, kumeelezwa na wakazi hao kwamba ni kuchoshwa na vitendo hivyo, huku wakiwashutumu polisi kulea uchafu huo.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi limekana kuwalea, likisema kazi yake ni kuwakamata na kuwapeleka mahakamani.

Kwa upande wao, ‘dada poa’ hao wametamba hawataiacha biashara hiyo, huku baadhi wakisema inawapa mafanikio kimaisha.

Mtaa wa Samora unahusisha eneo maarufu la Chako ni Chako lenye baa nyingi na maarufu kwa uchomaji wa kuku jijini hapa.

Mtaa huo unaelezwa kuwa na baa takriban 13, nyumba za kulala wageni 17.

Ni vita ambayo wakazi wake waliamua kufanya mkutano ulioshirikisha wakazi, diwani, mwenyekiti wa mtaa, mtendaji wa kata, mtendaji wa mtaa, polisi kata na wasichana wanaodaiwa kujihusisha na biashara ya ngono, ambao hata hivyo hawakuzungumza lolote kwenye mkutano huo.

Ulikuwa ni mkutano wa kupaza sauti. Wanawake wanapaza sauti, wanaume wanapaza sauti na viongozi wanalalamika kuhusu kundi waliloliita ‘madada poa’ wakisema biashara yao ya ngono imewaondolea heshima ya mtaa.

Mtaa wa Samora upo katikati ya jiji ukipakana na uwanja wa ndege wa Dodoma kwa upande wa kaskazini, magharibu ipo barabara ya Arusha, mashariki unapakana na Mtaa wa Makole wakati kusini ni ya barabara ya Dodoma–Singida.

Dada poa wameweka kambi hapo baada kambi yao kuu iliyodumu mtaa wa Tawfik kata ya Viwandani kusambaratishwa na polisi na aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi.

Wakazi wa mtaa huo chini ya mwenyekiti wao, Adelina Undili waliitisha mkutano wa hadhara uliolenga kuweka mkakati na mbinu za namna gani wanaweza kuwaondoa wanawake hao.

Katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na diwani wa kata, Jafari Mwanyemba, kuliundwa kikosi kazi kilichoshirikisha vijana waliotangaza mapambano na kundi hilo kwa namna yoyote hadi ushindi utakapopatikana.


Kauli za wananchi

Akizungumza katika mkutano huo, Emmanuel Maige alisema biashara ya kuuza miili inayofanywa na baadhi ya kina dada katika mtaa huo, imekuwa sasa ikifanyika hata nyakati za mchana, jambo alilosema wanatoa picha mbaya kwa watoto wadogo, kwani wanashuhudia madhambi hayo.

Maige alisema kumekuwa na juhudi za makusudi kutaka kukomesha biashara hiyo, lakini wanakwamishwa na polisi ambao mara nyingi huwakamata na kuwachukua, lakini muda mfupi wanawaona wakirejea mtaani.

Huku akishangiliwa na umati wa watu, alisema: “Sasa umefika wakati tutajilinda sisi na tutapambana nao wenyewe, tunaona polisi wamewashindwa kutokana na sababu ambazo hatuwezi kuzisema hapa hadharani.”

Kauli kama hiyo iliungwa mkono na Eliezer Mweda, akisema mapambano yao yakiwategemea polisi, dada poa watashinda, lakini akaeleza kuwa wananchi kwa umoja wao watamaliza na kurudisha heshima ya mtaa kwa mbinu wanazozijua.

Mweda alisema mtaa wa Samora umekuwa na sifa mbaya, hauthaminiwi na wengi wanatamani kuhama kutokana yanayotendeka, hivyo akatoa wito kwa vijana wenzake kujitokeza kwenye mapambano hayo.

Hata hivyo, alitaka Serikali ya mtaa kutokuwa na huruma wakati wa utekelezaji wa kazi hiyo, kwani inaweza kuwakumba watu wengi ambao baadhi watakuwa ni wamiliki wa nyumba zinazotumiwa na kina dada na hata vijana wa mtaani hapo.

“Kina mama wako sokoni, hapa kwetu ufuska unaanza kuanzia saa moja na mchana wako wanaoendelea ingawa si kama usiku, wengine wamekuwa watu wazima, lakini wanafanya mambo ya ovyo kabisa na kweli kina mama tumekosa thamani,” alisema Ashura Mohamed.

Ashura aliuambia mkutano huo kuwa katika kundi la dada poa, wapo watu wenye nguvu za kufanya kazi yoyote ya kuzalisha mali nje ya alichokiita umalaya wanaofanya, lakini akahoji wateja wao wanatoka wapi, kwani mapambano hayo yanatakiwa kutazama na upande huo.


Wenyewe wazungumza

Mmoja wa kina dada wanaofanya biashara hiyo, Salome Ashery aliliambia Mwananchi kuwa itakuwa ni ngumu kuacha biashara hiyo hata kama Serikali itakuja na mbinu za namna gani.

Salome (31) anasema kazi hiyo aliianza miaka nane iliyopita na kwake imemsaidia kiasi cha kujenga nyumba yenye vyumba vitatu kijijini kwao katika Wilaya ya Babati mkoa wa Manyara.

“Mimi nakuahidi hapa mchana kweupe hawatatuweza, mjini hapa nina miaka nane na yote nafanya kazi hii bila kupumzika, sasa unaachaje kuwa na wadau na mbinu za kupambana na makundi yanayotupinga tunazo,” anasema Salome.

Huku akiweka sharti la kutopigwa picha, anasema mara baada ya kumaliza elimu ya sekondari wakati akisubiri matokeo ya kidato cha nne, alipata ujauzito na kujifungua mtoto wa kiume ambaye anasoma darasa la tatu.

Anasema tatizo lilianzia hapo kwani wazazi wake walianza kumtenga na kumsema maneno mabaya, huku akinyimwa huduma za msingi na kila wakati walimwambia ni malaya asiye na heshima kwa jamii na wanaukoo.

“Matokeo yangu yalikuja nikawa na ufaulu wa daraja la tatu kwa alama 24, sasa nilipojifungua nilinyonyesha miezi tisa, wazazi wangu wakamchukua mtoto na kunitaka nikasome cheti cha sheria Mwanza ambako kweli sikuwa na wito huo, ndipo nilitoka nyumbani hadi leo ingawa huwa narudi mara moja kwa mwaka,” anasimulia.

Akizungumzia mkakati uliowekwa na mtaa, alisema hautakuwa na nguvu kutokana na baadhi wanaopambana nao wanawajua udhaifu wao, hivyo haitawapa ugumu huku akitaja alichokiita njaa kwa vijana zitawasambaratisha. Kwa upande wake Zamzam anasema vitisho walianza kuvipata siku nyingi, lakini mjini hawajawahi kutoka kwa kuwa watu wanahitaji huduma yao.

Zamzam ambaye wakati wote wa mahojiano alikuwa akitafuna vitu mdomoni, alisema kazi hiyo amedumu nayo miaka mitano akitokea wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro na mara kadhaa ameshakamatwa na polisi lakini anarudi mtaani na kazi inaendelea.

“Siyo lazima ujue jina langu la ukoo, hata huyo aliyekuleta halijui na sitaki alijue, lakini kwetu Kilosa mtaa wa Magomeni, sema lingine, hapa hatuachi pesa kiasi ulichonacho huduma utakadiriwa, lakini wanavyotunyanyasa wanatufanya tuwe na pesa nyingi maana tukiwa mafichoni dau hupanda,” anasema Zamzam.


Viongozi wa mtaa

Mwenyekiti wa mtaa wa Samora, Adelina Undili alisema tayari wameunda kikosi cha vijana ambao watatambulishwa polisi, ili walinde mtaa huo na kuwakamata wanawake wanaouza miili yao.

Undili alisema biashara hiyo inatia aibu mtaani kwake na kuharibu maadili kwani wanawake wa kundi hilo hawaoni aibu kumuita mtu hata kama ni mchana alimradi wapate pesa.

Kwa upande wake diwani Jafari Mwanyemba alisema nyumba wanazoishi dada poa zinajulikana hivyo akaagiza watendaji wake kuwa wakali katika vita hiyo na ikibidi milango ya nyumba hizo iombewe kibali ili ivunjwe.

Mwanyemba alizionyesha kwa kidole nyumba mbili zilizopo eneo la wazi karibu na msikiti akisema: “Nyumba hiyo na ile ziangaliwe kwani ndizo zinatajwa katika biashara hiyo, sasa mkakati ni kupambana na wenye nyumba badala ya kuwaangalia hao kina dada pekee.”

Mbali na biashara hiyo, Mwanyemba anasema mtaa huo unaongoza kwa uuzaji wa dawa za kulevya, jambo ambalo alitaka Jeshi la Polisi kutumia mbinu za kuwanasa wahusika, kwa kuwa lina mkono mrefu wa kuwakamata wahusika.


Polisi wajivua lawama

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Giles Muroto alisema mapambano kwa madada poa yamekuwa makali na amekuwa akiwakamata na kuwafikisha mahakamani kila wakati.

Alipinga tuhuma zinazotolewa na wananchi kuwa jeshi hilo ndilo linalowalea wanawake hao.

Muroto alisema hakuna ukweli kwamba Polisi wanawakamata na kumalizana nao, bali idadi kubwa wanapelekwa mahakamani ambako alisema hawezi kuingilia kuhusu mhimili huo, kwani si jukumu lake kuwafunga au kuwaachia.