Polisi yapiga ‘stop’ mkutano wa Mwabukusi, Dk Slaa

Mwanaharakati na Mwanasheria wa kujitegemea, Boniface Mwabukusi akiwahutubia wananchi waliojitokeza kusikiza Mkutano wa hadhara, (kulia) ni Dk Willbrod Slaa
Muktasari:
- Mkutano huo ambao uliandaliwa na Mwanaharakati na Mwanasheria wa kujitegemea,Boniface Mwabukusi ulipangwa kufanyika Leo Jumapili Oktoba 8,2023 katika Jimbo la Busokelo Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya .
Mbeya. Mwanaharakati na Mwanasheria wa kujitegemea, Boniface Mwabukusi amelazimika kuhairisha mkutano wa hadhara uliopangwa kufanyika eneo la Busokelo, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya baada ya polisi kudaiwa kuuzuia.
Hatua hiyo imefikiwa muda mfupi baada ya kuwasili kwenye viwanja vya mkutano akiwa ameambatana na mwanasiasa mkongwe, Dk Wilbrod Slaa kwa ajili ya kuhutubia mamia ya wananchi waliojitomeza kuwasikiliza.
Mwabukusi ambaye miezi michache iliyopita alifungua kesi ya kupinga mkataba wa uwekezaji wa bandari katika Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ambayo baadae ilitupiliwa mbali na mahakama ilibariki mkataba huo amedai polisi wamempa taarifa za kuhairisha mkutano huo kutokana na kupigwa nyimbo za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) eneo la mkutano.
“Ndugu zangu tumefika kwenye mkutano huu, lakini tumetakiwa kusitisha kwa sababu mlipiga nyimbo za Chadema sasa kwa atakayetaka kutusalimu aje nyumbani kwa wazazi pale,”amesema.
Mwabukusi amesema kuwa Polisi wana haki kisheria ya kuzuia mkutano ambao unaweza kuleta viashiri vya uvunjifu wa amani hivyo aliwataka wananchi hao warejee nyumbani kwao.
Baada ya kauli hiyo mamia ya wananchi walilazimika kusukuma gari lililowabeba wanaharakati hao mpaka nyumbani kwao huku wakiimba nyimbo za kuwasifia.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema kwa sasa hawezi kuzungumzia suala hilo kwasababu ana ugeni hivyo, apewe muda ataliongelea baadae.