Polisi: Baba wa watoto waliouawa alishikiliwa kwa mahojiano

Muktasari:
- Watoto Precious na Glory Evance wanadaiwa kuuawa na mama yao Juni 20, 2025 nyumbani kwao Kijiji cha Mungushi wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.
Hai. Polisi Mkoa wa Kilimanjaro imemuachia kwa dhamana Evance Kileka ambaye ni mume wa Mary Mushi anayedaiwa kuwaua watoto wake wawili.
Mary anadaiwa kuwaua wanaye Precious mwenye miezi sita na Glory wa miaka minne. Tukio hilo lilitokea Juni 20, 2025 nyumbani kwao Kijiji cha Mungushi wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro akidaiwa kuwakata na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za miili yao.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Abel Mtagwa akizungumza na Mwananchi leo Juni 25, 2025 amethibitisha Evance kuachiwa kwa dhamana.
Amesema alishikiliwa Juni 20 kwa ajili ya mahojiano na aliachiwa kwa dhamana jana Juni 24.
"Mume wa mtuhumiwa Mary Mushi alishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano, baada ya mahojiano ameachiwa kwa dhamana," amesema Kaimu Kamanda Mtagwa.
Mary yupo chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC. Anatibiwa majeraha yanayodaiwa yametokana na jaribio la kutaka kujiua kwa kijichoma na kitu chenye ncha kali.
Kwa mujibu wa ndugu, Evance jana alishiriki mazishi ya wanawe kijijini Mungushi akiwa chini ya ulinzi wa askari.
Akizungumza siku ya tukio Juni 20, mjomba wa watoto hao, Emmanuel Shija alisema baada ya kupata taarifa ya watoto hao kuuawa alifika eneo la tukio na kukuta miili imeondolewa.
"Hii taarifa nimeipata baada ya kupigiwa simu na baba mkwe wake na mdogo wangu kwamba kuna mauaji yametokea, wajomba zangu wawili, Glory na mdogo wake wameuawa," alisema.