Padri Nkwera kuzikwa kituo chake cha maombezi Ubungo Mei 18

Padri Felician Nkwera enzi za uhai wake
Muktasari:
- Padri Nkwera alifariki dunia usiku wa kuamkia Alhamisi Mei 8, 2025 katika Hospitali ya TMJ alipopelekwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Dar es Salaam. Mwili wa Padri Felician Nkwera unatarajiwa kuzikwa Jumamosi Mei 18, 2025 katika kituo chake cha Maombezi kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa jana Jumamosi Mei 10, 2025 na mwenyekiti wa huduma za maombezi wa kituo hicho, Deogratias Karulama alipozungumza na Mwananchi kuhusu ratiba za mazishi hayo.
Padri Nkwera alifariki dunia usiku wa kuamkia Alhamisi Mei 8, 2025 katika Hospitali ya TMJ alipopelekwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu baada ya kuzidiwa ghafla.
Mbali ya kutoa huduma za kiroho pia padri huyo ni mdau na mwalimu wa lugha ya Kiswahili ambapo enzi za uhai wake amewahi kuandika vitabu mbalimbali na makala.
Pia, aliwahi kuhudumu katika Kanisa Katoliki kabla ya kutengwa na uongozi wa kanisa hilo.
Akizungumzia kuhusu ratiba ya maziko yake, Karulama amesema watamzika Jumamosi kituoni hapo kwa kuwa ndipo aliacha wosia enzi za uhai wake kuwa akifa azikwe hapo.
"Suala la kuzikwa wapi halikutusumbua kichwa katika kikao kama azikwe lini kwa kuwa ni kitu ambacho alishaacha wosia akifa azikwe kituo hiki cha maombezi na sisi tunachofanya ni kutekeleza wosia huo," amesema mwenyekiti huyo.
Aidha ameeleza sababu ya kuamua kumzika Jumamosi imetokana na baadhi ya wageni wakiwemo mapadri kutoka bara la Ulaya, Marekani na Asia kuhitaji kuhudhuria maziko hayo.
"Hivyo tumeona tusiwanyime fursa wageni hawa ambao wameamua kuungana nasi katika kumsindikiza baba yetu huyu katika safari yake ya mwisho.
"Kwani tungeweza kumzika mapema zaidi lakini hatujaona sababu ya kufanya hivyo na badala yake tuwasubiri wenzetu nao wafike tujumuike pamoja katika shughuli hiyo," amesema Karulama.