Ofisi ya CAG yakana kuficha dosari za Serikali

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere. Picha na Maktaba.
Muktasari:
- Ofisi ya Taifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hufanya ukaguzi wa hesabu za Serikali, mashirika ya umma na miradi ya maendeleo kila mwaka na kukabidhi ripoti yake kwa Rais, naye huipeleka bungeni kwa ajili ya kujadiliwa.
Dar es Salaam. Ofisi ya Taifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imesema hakuna dosari zozote zinazofichwa kwenye ripoti za ukaguzi zinazotolewa na ofisi hiyo kwenye mashirika ya umma.
Kauli hiyo ni jibu la maswali ya wawakilishi wa asasi za kirai waliopatiwa mafunzo ya ukaguzi na ofisi hiyo ambao waliohoji madai ya kufichwa kwa taarifa mbaya zaidi zinazobainika wakati wa ukaguzi ndani ya Serikali, badala yake baadhi tu ndiyo hutolewa.
Akijibu swali hilo, Mei 12, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini, Ofisi ya CAG, Focus Mauki amesema ukaguzi ni mchakato mrefu na hakuna haja ya kuwa na wasiwasi ya kinachofanywa na ofisi hiyo.
“Ukaguzi ni mchakato mrefu, hadi kupeleka ripoti kwa Rais, bungeni na baadaye kutolewa kwa umma, kinachoelezwa kupitia ripoti ni sahihi na hakuna taarifa inayoondolewa au kufichwa kabla ya kutolewa kwa umma,” amesema.
Kutokana na hilo, Mauki amesema mafunzo ambayo Ofisi ya CAG imetoa kwa wawakilishi wa mashirika ya kiraia, yatakwenda kubadili fikra ya jamii kuhusu namna ofisi hiyo inavyofanya kazi.
Amesema asasi za kirai zitapewa kila moja toleo la wananchi la ripoti ya ukaguzi wa CAG ambayo imeandikwa kwa lugha rahisi na yenye michoro kuwezesha wananchi kuelewa nini kimeandikwa kwenye ripoti ya CAG.

Kwa upande wake, Mkaguzi wa Nje wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alfa Stanley, wakati akifungua mafunzo hayo, amewataka wananchi na asasi za kiraia kuzisoma ripoti za CAG ili kuchangia uwajibikaji.
Amesema ofisi ya CAG imekuwa ikitumia jitihada mbalimbali kuimarisha uelewa wa wananchi kupitia ripoti zake akisisitiza toleo la ripoti ya CAG kwa wananchi litaongeza uelewa.
“Toleo la wananchi ni nyenzo muhimu kwa wadau kutumia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ripoti zetu, wito wangu wadau na wananchi wajenge tabia ya kusoma ripoti za CAG ili kudumisha uwajibikaji,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Ofisi ya CAG, Emmanuel Lazaro amesema mpango mkakati wa ofisi hiyo umesaidia utekelezaji wa ukaguzi wenye tija unaolenga matumizi ya rasilimali kwa matokeo bora.
Pia, kuongeza uwazi kupitia ripoti za ukaguzi zinazopatikana kwa umma, kuweka vigezo na viashiria vya kupima uwajibikaji wa taasisi pamoja na taarifa za ukaguzi kuwasilishwa kwa Bunge na kuchochea mijadala ya uwajibikaji wa viongozi wa umma.
“Kupitia ukaguzi wa fedha na utendaji, CAG hutoa mapendekezo yenye lengo la kuboresha matumizi ya rasilimali,” amesema.
Lazaro amesema mpango mikakati huo umesaidia kuwepo kwa majukwaa ya kupokea mrejesho kuhusu ripoti za ukaguzi na ofisi inafanya vikao vya majadiliano na wadau kabla na baada ukaguzi, ili kuelewa changamoto na kutoa mrejesho.
Naye mwakilishi wa asasi ya Agenda Participation, Kamala Dickson amesema ripoti ya CAG mara nyingi huibua maswali mengi kwenye jamii na kupitia mafunzo hayo wamepata elimu namna ofisi hiyo inavyofanya kazi.
“Kuna haja ofisi ya CAG na wananchi kuwa na mjadala wa mara kwa mara kupitia asasi za kiraia kufahamu kwa nini wananchi wanapaswa kupata taarifa, hasa ya wale wanaotajwa kupitia ripoti hizi wawe wamechukuliwa hatua,” amesema.
Mshikiri mwingine wa mafunzo hayo, Arifa Kaluta amesema hatua ya CAG kuwajengea uwezo wawakilishi wa asasi za kiraia juu ya namna ofisi hiyo inavyofanya kazi, kutaongeza uelewa kwa wananchi juu ya umuhimu wa ripoti zinazotolewa na ofisi hiyo.