Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nyuki wachelewesha uokoaji ajali ya basi ikiua watu 14 Lindi

Muktasari:

  • Watu 14 wamefariki dunia na wengine 26 kujeruhiwa katika ajali ya basi iliyoyokea Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi.

Mtama. Wakati Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi likithibitisha kutokea kwa ajali ya basi iliyoua watu 14 na majeruhi 26 eneo la Mtama mkoani humo, mashuhuda wamesema nyuki walichelewesha uokoaji baada ya kuzingira eneo la ajali na kuwang’ata waokoaji.

Kwa mujibu wa Polisi, ajali hiyo imetokea leo Novemba 26, 2023 asubuhi, baada ya basi la kampuni ya Baraka Classic lililokuwa likitokea Newala (Mtwara) kweda Dar es Salaam, kufeli breki na dereva kushindwa kulimudu gari hilo.

Akizungumza katika eneo la ajali, moja ya mashuhuda wa ajali hiyo, Juma Machalila amesema wakati uokoaji ukiendelea, nyuki waliokuwa karibu walitimka na kuanza kung’ata waokoaji, jambo lililochelewesha uokoaji.

"Nyuki hao wapo siku zote ila baada ya kutokea ajali walianza kung'ata watu, tulilazimika kununua dawa ya kuulia wadudu pamoja na kuchoma matairi.

“Vifo vilivyotoķea pia vinaweza kuwa vimesababishwa na majeruhi kuchelewa kupata msaada,” amesema shuhuda huyo.

Naye Diwani wa Kata ya Mtama, Maria Nyale amesema nyuki walisababisha uokoaji uchukue muda mrefu.

"Baada ya ajali kutokea, ghafla nyuki walianza kuruka eneo la ajali na kuwauma watu, jambo lilosababisha kushindwa kuwaokoa watu mapema, lakini polisi walifika mapema wakashirikiana na wananchi kuchoma mipira na nyuki walitokomea," amesema Maria.

Taarifa ya ajali hiyo iliyotokea leo na Kamanda wa polisi Mkoa wa Lindi, ACP John Makuri, imesema amesema chanzo cha ajali hiyo ni basi la Baraka Classic kushindwa kukamata breki.

Kamanda Makuri amefafanua kuwa vifo 12 ni vya abiria waliokuwa ndani ya basi hilo na vifo vya watu wawili ni vya watembea kwa miguu, huku kukiwa na majeruhi 26 waliopelekwa hospitali ya Nyangao kwa ajili ya matibabu.

"Watu hao 14 waliofariki, 12 ni abiria waliokuwa wanasafiri na basi hilo na wawili walikuwa watembea kwa miguu, dereva wa basi hilo anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Nyangao akiwa chini ya ulinzi," amesema Kamanda Makuri.

Pia kamanda Makuri ametoa wito kwa madereva wazembe kuwa makini kwani sheria kali zitachukuliwa dhidi yao wanaposababisha ajali.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Telack, amewashukuru wananchi waliosaidia kuokoa wakati wa ajali licha ya kuwapo kwa nyuki.

"Niwashukuru sana wananchi wa Mtama kwa juhudi mliyoifanya ya uokoaji wakati ajali ilipotokea licha ya uwepo wa nyuki wengi," amesema Telack.